Kuna mabaya, majanga mbalimbali yanayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Ni mambo ambayo hatukutegemea yatokee, lakini pia hatuwezi kuyazuia yasitokee.
Mfano ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko na kadhalika. Yapo mabaya na majanga mengi ambayo tumewahi kukutana nayo na tutaendelea kukutana nayo.
Unaweza kuomba sana usikutane na mabaya hayo, lakini kama wanavyosema dua la kuku halimpati mwewe, maombi yako hayataifanya dunia iende kama unavyotaka wewe iende.

Hivyo mambo yatatokea, mambo mabaya ambayo hukutegemea yatokee. Na huwezi kuyazuia, ila una njia mbili za kukabiliana nayo;
Moja; hakikisha una njia mbadala. Kwenye maisha yako, epuka sana kuwa na njia moja tu ya kufanya mambo, epuka kutegemea kitu kimoja pekee. Majanga yanapotokea na ukawa na tegemeo moja, yatakumaliza kabisa. Unahitaji kuwa na njia mbadala za kufanya mambo, unahitaji kuwa na uwezo wa kuchukua hatua pale kile unachotegemea hakifanyi kazi tena. Na kwa sehemu kubwa ya majanga ya kimaisha, unahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ya dharura.
SOMA; UKURASA WA 189; Matatizo Yote Ya Mahusiano Yanaanzia Hapa… Sehemu Ya Pili(2)
Mbili; hakikisha majanga yanakuacha ukiwa imara kuliko ulivyokuwa awali. Usikubali majanga yakupite, halafu unabaki kwenye hatari ya kusumbuliwa tena na majanga ya aina hiyo. Hakikisha yanakuacha ukiwa imara zaidi, ukiwa na uwezo wa kukabiliana na majanga ya aina hiyo na hata makubwa zaidi. Kwa kifupi kaa chini na orodhesha yale uliyojifunza na hatua unazokwenda kuchukua ili kuwa imara zaidi wakati mwingine.
Majanga utakutana nayo, tena na tena, utayari wako wa kuyakabili na kutoka ukiwa imara ndiyo mambo muhimu kwako kwenye majanga unayokutana nayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog