Ugonjwa mkubwa wa siku hizi, zama hizi za mitandao ya kijamii ni hofu ya kupitwa. Watu wanataka kuwa kila mahali kwa kila wakati, kujua kila kinachoendelea na kutokupitwa na chochote. Ndiyo maana wengi wamekuwa watumwa wa mitandao hii ya kijamii.

Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba watu wanagusa simu zao mara nyingi mno, na mtu akikaa nusu saa hajagusa simu yake na kuona nini kinaendelea, anaona kama dunia inamwacha, kama anakosa makubwa yanayoendelea.

Mitandao

Hali hii pia ndiyo imekuwa inawanasisha watu kwenye habari, sehemu kubwa sana ya habari za kila siku siyo kweli au zimetiwa chumvi, na siyo muhimu sana kwenye maisha ya kila siku. Lakini watu hawathubutu kukosa habari kwa sababu wanaona kuna kitu wanakikosa.

Sasa rafiki, unapaswa kujua kitu kimoja, mambo yanayoendelea hapa duniani ni mengi mno. Habari za kila siku ni nyingi sana. Na mambo watu wanaweza kuweka kwenye mitandao ya kijamii ni mengi.

SOMA; UKURASA WA 978; Mambo Mawili Muhimu Kuhusu Fursa.

Muhimu zaidi unachopaswa kujua ni kwamba huwezi kumaliza kila kitu, huwezi kujua kila kitu, na huhitaji kujaribu kila kitu. Unahitaji kujua hilo na kuridhika nalo kwa sababu kinyume chake utateseka na kuwa mtumwa wa vitu.

Jua ni mambo gani muhimu zaidi kwako, jua ni kipi cha tofauti unataka kufanya hapa duniani, kisha kazana na hicho, jua maarifa na taarifa zake na jua fursa zinazopatikana kwenye kitu hicho.

Na kwa vile tumegusia fursa basi pia nikukumbushe hili nimewahi kukuambia siku za nyuma. Linapokuja swala la fursa, acha kukimbizana na kila fursa inayopita mbele yako, au kila ambacho wengine wanaita fursa. Hutaweza kufanya kila kitu na ukijaribu utachoka sana na hutakamilisha chochote.

Muda wako ni mfupi, nguvu zako zina ukomo, chagua kwa makini ni vitu vya aina gani utajihusisha nacho, na usiwe na hofu kwamba unapitwa, hakuna chochote kinachokupita, labda kama unaahirisha kuishi ndoto kubwa ya maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog