“You have power over your mind – not outside events. Realize this, and you will find strength” – Marcus Aurelius
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UIMARA WAKO UKO HAPA…
Huwa tunapenda dunia iende kama tunavyotaka sisi wenyewe,
Tunataka yatokee yale tunayopenda sisi na changamoto zisiwepo kabisa.
Tunapenda kila mtu awe kama tunavyotaka sisi, kila mtu asikie na kufuata tunachosema.
Lakini matakwa yetu hayo yanashindwa, na yanashindwa vibaya.
Dunia inaendelea kwenda kama inavyoenda yenyewe,
Na watu wanaendelea kuwa kaka wanavyoamua kuwa wenyewe, licha ya kuwapigia kelele.
Hili linaweza kutukasirisha, na kutufanya tukate tamaa juu yetu, juu ya wengine na hata dunia kwa ujumla.
Lakini kukata tamaa siyo suluhisho, na wala siyo hatua sahihi.
Unachopaswa kujua ni Uimara wako uko wapi na uweze kuutumia.
Uimara wako uko ndani yako, ndani ya mawazo yako, kwenye mtazamo wako.
Kitu kingine chochote nje ya hapo siyo uimara wako, hivyo kukazana nacho kiwe kama unavyotaka ni kujiandaa kushindwa.
Unaweza kubadili kile unachofikiri,
Unaweza kubadili mtazamo wako juu ya hali, vitu au watu.
Hapo ndipo uimara wako ulipo, na ukiweza kuutumia vizuri, hakuna yeyote atakayekusumbua.
Hatua ya kwanza ya kutumia uimara wako ni hii; jua kwamba huna nguvu ya kubadili mambo ya nje, mengi yanatokea kama yanavyotokea na yataendelea kutokea iwe unataka au la.
Ila una nguvu kubwa ya kubadili fikra zako, mtazamo wako na hata hatua unazochukua kila siku.
Tumia uimara wako na achana na yale ambayo hayapo kwenye uimara wako.
Uwe na siku bora leom siku ya kuwa imara zaidi kwa kutumia uimara wako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha