Tunaweza kuyaelewa maisha kwa kuangalia nyuma, ni kwa kuangalia yale yaliyotokea ndiyo tunaweza kuelewa kwa nini yalitokea na matokeo yake yalikuwaje.
Lakini hatuwezi kuyaishi maisha yetu kwa kuangalia nyuma, bali tunaishi maisha kwa kuangalia mbele. Hivyo tunayaishi maisha yetu kwa kuangalia mbele.
Changamoto ya kuangalia mbele ni moja, hatuna uhakika na mengi ya mbele, hatuna uhakika nini kitatokea, na pia hakuna anayeweza kutabiri kesho.

Wale ambao hawathubutu kuishi kwa kuangalia kesho, ndiyo hutumia muda wao mwingi kueleza jinsi nyuma kulivyokuwa vizuri.
Utawasikia wakisema enzi hizo mambo yalikuwa vizuri, enzi zetu tulifanya vizuri na kadhalika. Ni rahisi kuongelea enzi hizo kwa sababu ukiangalia nyuma ndiyo unaona maana ya kila kilichotokea.
SOMA; UKURASA WA 1019; Kama Huwezi Kuona Ubaya, Huwezi Kuona Uzuri Pia…
Hii ina maana kwamba, enzi za kesho ni leo. Yale utakayofanya leo, licha ya kutokuwa na uhakika, ndiyo ukiyaangalia kesho utasema enzi hizo.
Kwa kuwa kesho haina uhakika, lakini kwa kuwa pia njia pekee ya kuishi maisha ni kuangalia mbele, tunahitaji sana kuwa na mwongozo wa kutuwezesha kufanya maamuzi. Tunahitaji kuwa na kitu cha kutuwezesha kufanya maamuzi hata kama hatuna uhakika wa matokeo. Na ni maamuzi haya, ambayo kwa kuyaangalia baadaye, tunaona jinsi ambavyo yalikuwa na maana kwetu.
Tuangalie nyuma kupata maana ya yale yaliyotokea na kujifunza pia, lakini tuangalie mbele kuyaishi maisha yetu ya kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog