Una simu ambayo ina chaji asilimia 10, umeme umekatika siku nzima, halafu kuna simu ya muhimu sana unaisubiri, je unatumiaje ile asilimia kumi ya chaji iliyobaki?
Je utaanza kusikiliza miziki au kuangalie video ulizonazo kwenye simu hiyo? Je utaingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kuperuzi, uone wengine wanafanya nini?

Kwa akili timamu, hutatumia chaji kidogo ya simu uliyonayo kufanya mambo ambayo siyo muhimu. Tena hata akikupigia mtu ukaona anaongea muda mrefu mambo yasiyo muhimu, utamwomba muongee baadaye kwa sababu kwa muda huo huna chaji.
Hivi ndivyo tunavyoheshimu simu zetu chaji inapokuwa adimu.
Lakini tunafanya kosa kubwa sana kwenye nguvu zetu binafsi, tunazitawanya hovyo, kama vile haziiishi.
SOMA; UKURASA WA 942; Kinachokupoteza Ni Vipaumbele…
Nguvu za miili yetu ni kama chaji kwenye simu, unauchaji mwili unapolala, hivyo ukiamka mwili unakuwa umejaa chaji, asilimia 100. Kila unachofikiria kinapunguza chaji yako, kila unachofanya kinapunguza chaji yako.
Sasa hapa ndipo unaweza kutumia nguvu za mwili wako kupima vipaumbele vyako. Je kile unachofikiria au kufanya ndiyo kitu muhimu kabisa? Je ndiyo matumizi sahihi ya nguvu zako?
Kama ingekuwa ni simu, na unasafiri hivyo huna nafasi ya kuchaji, ungeituma kwa hicho unachofanya?
Sasa fikiria unapoianza siku yako kwa kufuatilia habari, ambazo kesho yake zote zitakuwa hazina maana tena. Au muda wa kazi wewe unazurura kwenye mitandao ya kijamii, ukifuatilia maisha ya watu, ambayo hata siyo halisi. Au unaacha kufanya muhimu kwako kwa sababu unafuatilia wengine wanaendeleaje.
Haya siyo matumizi sahihi ya nguvu zako, ambazo hazidumu milele. Hivyo kuwa mchoyo sana wa nguvu zako, kama unavyokuwa mchoyo kwenye matumizi ya chaji ya simu yako pale unapokuwa huna uhakika wa kuongeza chaji. Kama kitu huwezi kukifanya kwenye simu iliyobakiza chaji kidogo basi pia hustahili kupoteza nguvu za mwili wako kukifanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog