Ukingo wa maisha ya kila mmoja wetu ni kifo, ambacho kitatokea kwa wakati ambao hata hatuujui, na huenda hatutajua kama ndiyo ukingo.
Lakini mambo mengi tunayosumbuka nayo kwenye maisha, yale tunayofikiri kwamba maisha yetu hayataenda kama tutakosa mambo au vitu hivyo.
Unafikiri maisha yako yatafika ukingoni kwa sababu hujavaa nguo fulani ambayo kila mtu anavaa? Au unafikiri maisha yako yatafika ukingoni kwa sababu hujaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu na hujui kinachoendelea? Unafikiri maisha yako yatafika ukingoni kwa sababu aliyekuambia anakupenda hakupendi tena?

Kwa hakika mambo mengi unayotegemea sana, unayotumia muda mwingi wa maisha yako kuyasumbukia, hayatasababisha maisha kufika ukingoni iwapo utakosa mambo hayo.
Badala yake utaziona fursa zaidi, utajifunza mengi zaidi na utaona uwezo mkubwa uliopo ndani yako, ambao hukuwahi kuuona huko nyuma.
Maisha hayatafika ukingoni kwa kukosa vingi unavyojiambia sasa kwamba ni muhimu zaidi kwako. Unajiambia vingi ni muhimu kwa sababu ndiyo kila mtu anaona ni muhimu, ndivyo ulivyozoea kufanya na huna uzoefu wa maisha bila ya vitu hivyo.
SOMA; UKURASA WA 1053; Kadiri Uimara Unavyokuwa Mkubwa, Ndivyo Udhaifu Unakuwa Mkubwa Pia….
Lakini pale vinapokosekana, ndipo unajifunza mengi zaidi kuhusu maisha, ndipo unagundua kwamba ulikuwa na nguvu kubwa ambazo hujawahi kuzitumia. Na kama kile ambacho unasema muhimu ni muhimu kweli, basi utakapokikosa maisha yako ndiyo yatakuwa yamefika ukingoni, lakini siyo kwa vingi.
Yote haya ni kujikumbusha kwamba, tunapaswa kuishi maisha yetu kwa uhuru, kwa kufanya kile ambacho ni sahihi na kutokuwa na hofu ya kupoteza chochote ambacho tunajiambia ni muhimu. Vingi tunavyohofia kuvipoteza, hata tukivipoteza maisha yetu yatakwenda kawaida tu, na mara nyingi yatakuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog