Habari za watu waliofanikiwa, walioanzia chini na kuweza kupanda mpaka juu sana ni habari nzuri, zinazovutia na zinazosisimua.

Ni habari rahisi kufuatilia na kuelewa, alianzia hapa sifuri na sasa ni shujaa.

Ni habari zenye matumaini, kwamba huyu ambaye alianzia chini, bila ya chochote kwenye mazingira ambayo sisi pia tupo, ameweza kufanikiwa, ni kiashiria kwamba na sisi tutafanikiwa.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho hakionekani wazi kwenye hadithi hizo za mafanikio, zinaonesha mwanzo na mwisho, alipoanzia na alipofikia.

Hadithi hizi hazioneshi mchakato mzima wa mtu aliopitia kutoka sifuri mpaka kileleni. Hadithi zinaonesha katoka hapa na kafika hapa.

Hadithi hizo hazitakuonesha kwamba mtu huyo kwa zaidi ya miaka kumi alikuwa akiteseka, akipitia magumu, lakini alivumilia na kutokukata tamaa.

Hadithi hizo hazitakuonesha kwamba mtu huyo alikuwa anachelewa kulala na kuwahi kuamka, hakuwa anatumia muda wake kwa mapumziko na anasa.

Hadithi hizo hazitakuonesha muda mwingi ambao mtu huyo alikuwa mbali na familia yake. Hazitakuonesha kipindi ambacho mtu huyo alikuwa anakula chakula cha hovyo, au wakati mwingine hana chakula kabisa.

SOMA; UKURASA WA 822; Badili Hadithi Unayoishi…

Na kuna sababu moja kwa nini hadithi hizi hazioneshi yote hayo. Kwa sababu zikionesha hayo yote, wasiofanikiwa watachukia, wataanza kukosoa, wataanza kuhukumu na kujiona wao ni watakatifu sana, kwa sababu japo hawajafanikiwa, basi wana vingi ambavyo wale waliofanikiwa hawana.

Sasa kama wasiofanikiwa, ambao ni wengi watachukia habari hizo za mafanikio, zitakosa wasomaji, na watoaji wa habari hizo watashindwa kupata wanachotaka.

Hivyo rafiki, usiwe kama kundi la wengi wasiofanikiwa, ukisikia habari ya mtu ametoka sifuri mpaka kileleni, swali la kwanza uliza gharama kiasi gani amelipa? Ukiweza kuchunguza na kujifunza hilo, utajifunza mengi ambayo unaweza kufanyia kazi na kufanikiwa pia.

Hutafanikiwa kwa kujua mtu ametoka sifuri mpaka kwenye mafanikio, utafanikiwa kama utajua njia aliyopita na wewe ukaipita pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog