Ukiona kitabu kimeandikwa siri kumi za mafanikio, utavutiwa kukinunua na kukisoma.
Lakini ndani ya kitabu hicho, hutakutana na vitu vipya ambavyo huvijui. Zile unaambiwa ni siri, utakuta ni mambo yale yale ambayo unayafahamu. Kuwa na maono makubwa, kujitoa kufanya kazi, kuwa na nidhamu, kujifunza na kushirikiana na wengine ni mambo ambayo hutayakosa kwenye siri hizo.

Sasa inakuwaje mafanikio yanakuwa siri wakati vitu vingi tunavijua? Ina maana unahitaji mtu akuambie kwamba ili ufanikiwe unahitaji kuweka juhudi kwenye kazi? Halafu wewe unamshukuru sana kwa kukupa siri ambayo hukuijua?
Kila kitu kuhusu mafanikio karibu kila mtu anakijua, lakini mafanikio yanaendelea kuwa siri, yanaendelea kuwa kwa wachache.
Kinachoyafanya mafanikio kuwa siri siyo kujua, bali kufanya. Kujua kuhusu mafanikio ni rahisi, lakini kufanyia kazi yale unayojua, kujitoa kweli ili kupata kile unachotaka ndipo ugumu ulipo.
SOMA; UKURASA WA 999; Unapoukaribia Ukweli, Hofu Inaongezeka…
Ni watu wachache sana ambao wapo tayari kujitoa kwa ajili ya mafanikio, wapo tayari kuweka juhudi kubwa, kujitesa ili kupata wanachotaka. Ni watu wachache sana ambao wapo tayari kubeba majukumu ya maisha yao, ambao hawatafuti mtu wa kumlaumu au kulalamika.
Kila kitu kuhusu mafanikio kipo wazi, ni kuishi maisha yanayokupeleka kwenye mafanikio ndiyo siri kubwa. Na siyo siri kwa sababu hujui utaishije, ni siri kwa sababu mateso yake ni wachache wanaoweza kuyavumilia. Wengi wanapenda raha, hasa za muda mfupi, ambazo zinaharibu kabisa mipango ya muda mrefu.
Unaweza kujua kila unachotaka kujua kuhusu mafanikio, lakini kama hutachukua hatua ya kuishi kile unachojua, hutaweza kuyafikia mafanikio makubwa unayotaka kufikia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog