“The greatest remedy for anger is delay” – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari DAWA KUU YA HASIRA…
Kwenye maisha yako ya kila siku, watu watakukasirisha..
Watu watakuambia maneno ambayo siyo mazuri,
Watu watakuahidi kitu fulani lakini wasifanye,
Watu watakudanganya,
Watu watajaribu kukuibia au kukutapeli,
Watu watakatisha mbele yako wakati unaendesha gari barabarani,
Watu watapitiliza na kwenda mbele wakati wewe umesubiri kwenye foleni,
Watu watajaribu kutumia kazi zako kujipatia sifa na manufaa mengine,
Yote haya yanaleta hasira,
Yanakufanya utake kumwonesha yule aliyekufanyia kitu hicho kwamba anakosea,
Unasukumwa kumfundisha adabu, kumfundisha jinsi anavyopaswa kufanya mambo kwa usahihi.
Unaweza kuwa unaona unafikiria vizuri, lakini tatizo ni moja, unapokuwa na hasira ni sawa na hufikirii kabisa,
Hivyo unapokuwa kwenye kilele cha hasira, hatua bora kabisa kwako kuchukua ni kusubiri.
Usifanye wala kusema chochote wakati una hasira kali.
Kwa sababu chochote utakachofanya au kusema wakati huo hakitakuwa sahihi na kitatengeneza matatizo zaidi.
Subiri kwanza, ondoa akili yako kwenye jambo hilo, lipuuze kwa muda na wakati mwingine mpuuze yule aliyekutendea kile kilichokukasirisha.
Baadaye utaweza kufikiria vizuri na kuona kipi sahihi kufanya, lakini siyo wakati bado una hasira.
Unapopandwa na hasira, tulia, subiri, usikimbilie kusema au kufanya chochote.
Ukimya wenyewe ni dawa tosha kwenye hasira, na badaye utaweza kufikiri vizuri zaidi.
Huwezi kujizuia usipate hasira kabisa, kwa sababu watu hawataenda kama unavyotaka wewe. Ila unaweza kujizuia usitawaliwe na hasira zao, na hili ndiyo zoezi tulilojifunza hapa leo.
Ukawe na siki bora leo, siku ya kutulia pale hasira zinapokuwa juu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
Asante sana cocha makirita kwa tafakari ya leo na ubarikiwe sana
LikeLike
Karibu Kasanda
LikeLike