Rafiki yangu,

Hongera sana kwa juma hili namba 20 tunalomaliza.

Ninachoamini ni kwamba, hili limekuwa juma la ushindi kwako, limekuwa juma ambalo umepiga hatua kubwa, pia limekuwa juma ambalo umejifunza.

Na kama ambavyo nimekuwa nakusisitiza rafiki yangu, naamini hili ni juma ambalo umeendelea kujenga urafiki wako na kazi, kwa sababu rafiki yako wa kweli, baada ya mimi ni KAZI. Ipende sana kazi na kila siku weka kazi zaidi ya wengine kuhakikisha unapiga hatua zaidi na kuongeza thamani kwa wale wanaokuzunguka.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kumaliza wiki na kuanza wiki mpya. Pitia haya matano, ondoka na kitu au vitu unavyokwenda kufanyia kazi na anza juma jipya kwa kufanyia kazi vile ulivyojifunza. Hiyo ndiyo njia pekee ya kunufaika na unachojifunza, kuchagua kitu cha kufanyia kazi na kuanza kufanyia kazi.

vitabu softcopy

Twende kazi sasa rafiki yangu, na haya ndiyo matano muhimu niliyokuandalia juma hili la 20 tunalolimaliza.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUMILIKI MAISHA YAKO.

Rafiki, unajisikiaje pale unapoianza siku, unahangaika nayo, unafika mwisho wa siku, umechoka kweli lakini hakuna kikubwa ambacho unaona umekamilisha?

Vipi pale unapofanya kazi miaka 10, au 20 lakini siku moja unaangalia kipi kikubwa umefanya na huoni?

Hali hii inaumiza sana, kwa sababu unakuwa hujui wapi ambapo umekosea, kila siku umekuwa mtu wa kujituma, lakini hupigi hatua kubwa.

Unaweza kufika mahali ukafikiri labda huna bahati, au una kisirani, au kuna watu wamekuchezea vibaya.

Mwandishi Aubrey Marcus analo jibu kwa nini mtu unafikia hatua hiyo. Na jibu lake ni moja, ni kwa sababu unamilikiwa na watu au vitu vingine. Tatizo ni kwamba hujamiliki maisha yako ndiyo maana hata ukijituma sana, unaishia kutokuona matokeo makubwa.

Kwenye kitabu chake cha OWN THE DAY, OWN YOUR LIFE, Aubrey anatupa njia ya kurudisha umiliki wa maisha yetu, ambayo siyo ngumu, haihitaji uwe na elimu kubwa, fedha nyingi au uwe mtu wa hadhi fulani.

Aubrey kwenye kitabu chake, anatufundisha jinsi ya kuimiliki siku, ili kuweza kuyamiliki maisha yetu. Unachohitaji ili kumiliki maisha yako, ili kufanikiwa na kufika unakotaka, ni kumiliki siku yako moja, kuiishi siku kwa namna unavyopanda wewe na siyo kwa namna dunia inavyotaka uende.

Kwenye kitabu hichi, Aubrey anatushirikisha jinsi ya kuiendea siku yako, tangu unapoamka mpaka unaporudi kulala.

Kwa mfano kwenye kuamka, Aubrey anatuambia tufanye vitu vitatu muhimu sana, bila ya vitu hivi, unachagua kuipoteza siku yako, na kuishia kumilikiwa na wengine. Vitu hivyo vitatu ni KUNYWA MAJI, KUPATA MWANGA WA JUA NA KUUWEKA MWILI KWENYE MWENDO.

Kuna vitu vingine viwili ambavyo tunapaswa kuvifanya asubuhi tunapoianza siku, vitu hivyo ni kupumua kwa kina na kuoga maji ya baridi sana. Aubrey amekwenda kwa kina na kwa mujibu wa tafiti, kutuonesha faida ya kila anachoshauri tufanye.

Hichi ni kitabu ambacho kila mtu anayetaka kufanikiwa, anapaswa kukisoma, na siyo tu kukisoma, bali kuweka kwenye matendo yale anayojifunza. Kwa mfano Aubrey anatuonesha kosa kubwa tunalofanya asubuhi, ambalo ni kutumia sukari. Kwa namna alivyoelezea, nimejikuta ni mhanga wa hali hii. Anasema ukitumia kifungua kinywa chenye sukari, mwili unapokea sukari nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuzalisha homoni ya insulin ambayo inaondoa sukari kwenye mwili, sasa inaweza kupelekea mwili ukawa na sukari ndogo kwa haraka na hivyo kujikuta unachoka sana saa moja au mawili baada ya kutumia kifungua kinywa chenye sukari. Badala ya sukari Aubrey anatuonesha kwa tafiti za kisayansi kwamba ni bora kifungua kinywa kiwe na mafuta zaidi kuliko sukari na wanga, na kama huwezi kukwepa sukari, basi bora usipate kifungua kinywa.

Hapa Aubrey amenifundisha mambo mawili makubwa sana ambayo sikuwahi kuyaangalia kwa kina. La kwanza ni hatari ya mafuta, tumekuwa tunaogopa mafuta kwamba ni hatari, lakini Aubrey ameonesha kwa tafiti kwamba sukari ni hatari kuliko mafuta. Pia amenifundisha kitu kuhusu kifungua kinywa, nilikuwa nikiamini kifungua kinywa ndiyo chakula muhimu sana kwenye siku, kwamba ni bora usile mchana au usiku lakini upate kifungua kinywa. Lakini kwa tafiti amenionesha kwamba kifungua kinywa siyo chakula muhimu cha siku. Na ametufundisha njia bora ya kula ni kuhakikisha unapata chakula bora saa sita mchana, kisha unakula tena kabla ya saa mbili usiku na baada ya hapo usile tena mpaka kesho yake mchana.

Yapo mengi sana kwenye kitabu hichi, na kwenye kila sura, kuna mengi nimejifunza ambayo sikuwa nayajua, au nilikuwa nayajua kwa mtazamo potofu.

Nitakushirikisha zaidi kuhusu kitabu hichi kwenye makala ya uchambuzi wa kitabu, lakini nakusisitiza sana, pata na usome kitabu hichi. Maana Aubrey hajaacha kitu, kuanzia matumizi mazuri ya muda unaoenda kwenye kazi zako, jinsi ya kuzifanya kazi zako kwa hamasa kubwa, mpaka kufanya mapenzi, kila kitu kwenye siku yako ameeleza jinsi ya kukifanya kwa ubora. Kama utasoma kitabu kimoja kwenye maisha yako, basi OWN THE DAY, OWN YOUR LIFE kinapaswa kuwa kitabu hicho. Nimekuwa nasema hili kwenye vitabu vingi, lakini hichi naongeza msisitizo, KISOME.

#2 MAKALA YA WIKI; NIMEONDOKA KWENYE MITANDAO YOTE YA KIJAMII.

Nimeondoka rasmi kwenye mitandao yote ya kijamii niliyokuwa naitumia, na sina mpango wa kurudi kwa sasa, japo siwezi kuahidi ni lini nitarudi au kusema sitarudi tena. Kwenye makala niliyoandika wiki hii nimeeleza kwa kina kwa nini nimefikia maamuzi hayo na wapi ninapatikana kwenye mtandao wa intaneti.

Pia kwenye makala hiyo, nimeeleza hasara mbili kubwa za mitandao ya kijamii ambazo kila mtumiaji anapaswa kuwa makini nazo. Nimeeleza pia njia ya kuondokana na hasara hizo ili zisiwe kikwazo kwako.

Unaweza kuisoma makala ya wiki hapa; Hasara Mbili Kubwa Unazopata Kwenye Mitandao Ya Kijamii (Na Kwa Nini Sipo Tena Kwenye Mitandao Ya Kijamii) (https://amkamtanzania.com/2018/05/16/hasara-mbili-kubwa-unazopata-kwenye-mitandao-ya-kijamii-na-kwa-nini-sipo-tena-kwenye-mitandao-ya-kijamii/)

#3 TUONGEE PESA; UNAZIJUA HESABU ZA MICHEZO YA KAMARI?

Nani asiyependa kuondokana na matatizo ya kifedha?

Michezo mingi ya bahati nasibu (ambayo mimi yote naiweka kwenye kundi la KAMARI) inayoibuka kila siku, ni kwa sababu waanzishaji wanajua kitu kimoja, watu wanapenda fedha lakini hawapo tayari kujiumiza kuzipata, hivyo wanaanzisha mitego hiyo, ya kuwashika watu kutumia tamaa zao.

Ambazo watu wanaoshiriki michezo hii hawaelewi ni kwamba kampuni zinazoendesha biashara hizi hazitoi fedha zao na kugawa kwa watu. Na pia kampuni hizi hazipati hasara. Hivyo zinakusanya fedha za wengi ambao wana tamaa ya kupata fedha, kisha kugawa kiasi kidogo sana kwa wachache, halafu kubaki na faida kubwa.

Kwa mfano kampuni inapokuambia kwa shilingi mia tano utapata milioni 10. Watu milioni moja wenye tamaa ya fedha, wakashiriki kwa kutuma mia tano, kampuni inakusanya milioni mia tano. Kisha inaweza kuchagua washindi kumi, wa kuwapa milioni 10 kila mmoja, hivyo milioni 100 zinarudi kwa wachezaji, na milioni 400 zinaenda kwenye kampuni inayochezesha mchezo huo. Nani mwenye hasara hapo?

Kama una akili zako timamu, na siyo za kuvuka barabara pekee, usije kucheza kamari kwenye maisha yako, na kama ulishawahi kucheza basi niandikie ujumbe ukiniambia sitarudia tena kucheza na usicheze tena. Hata kama unacheza kwa kujifurahisha, ni bora hiyo fedha upeleke kwenye mambo mengine, saidia hata wasiojiweza, kuliko kuwafaidisha watu ambao wanatumia vibaya ujinga na uvivu wa wengine.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KUIANZA SIKU NA TAFAKARI CHANYA.

Kama ambavyo nimekushirikisha kwenye kitabu cha wiki hii, kuyamiliki maisha yako, unahitaji kuimiliki siku yako.

Sasa ukiacha yale ambayo Aubrey ametushirikisha kwenye kitabu chake, kuna njia moja ambayo nimeona watu wanaitumia kupoteza siku zao.

Njia hiyo ni kuianza siku wakiwa wamekata tamaa.

Watu wengi wamekuwa wanaianza siku wakiwa wamechelewa kuamka, hawataki kuamka na kazi wanazoziendea hawazipendi na haziwalipi vizuri.

Kibaya zaidi wanachochea hali hiyo kwa kusikiliza habari na kusoma magazeti mwanzo kabisa wa siku, hapo ndipo kukata tamaa kunapozidi na hawapati hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Njia bora kabisa ya kuianza siku yako, ni kuwa na fikra chanya, fikra za kukupa hamasa ya kupiga hatua, huku ukiwa na matumaini ya kufika mbali zaidi.

Hivyo ndiyo ninachokupa kwenye KISIMA CHA MAARIFA kila asubuhi. Unapokuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, asubuhi unapata tafakari nzuri ya kuianza siku, tafakari inayokufanya uwe na mtazamo chanya na uwe na hamasa ya kwenda kuweka juhudi kubwa hata kama mambo ni magumu kiasi gani.

Kama bado haupo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unakosa njia hii bora kabisa ya kumiliki siku yako. Jiunge sasa ili upate njia bora ya kuianza siku yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717396253 wenye neno KISIMA CHA MAARIFA na nitakutumia maelekezo. Ujumbe utumwe kwa njia ya wasap tu.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HATARI KUBWA YA MALENGO UNAYOJIWEKEA.

“The greater danger for most of us is not that our aim is too high and we miss it, but that it is too low and we reach it” – Michelangelo

Michelangelo anatuambia kwamba hatari kubwa kwenye maisha yetu siyo kuweka malengo makubwa na kushindwa kuyafikia, bali tunaweka malengo madogo na kuyafikia.

Unaweza kuona hiyo ni kauli rahisi, lakini imebeba ujumbe mkubwa sana ndani yake.

Hivi unafikiri kwa nini watu wanakaa kwenye kazi ambazo haziwalipi na hawazipendi, miaka 10, 20 mpaka 30 halafu hawana kikubwa ambacho wamefikia? Unafikiri hao watu ni wajinga sana?

Watu hao siyo wajinga, bali wamepata kile walichokuwa wanataka. Malengo yao yanakuwa madogo sana, lengo kuu linakuwa kula na kuishi, hivyo wakishapata hayo, wanaacha kukazana, wanaridhika na kukubali mambo yaende. Laiti kama wangekuwa na malengo makubwa zaidi, ambayo wanaweza kushindwa, lakini wakayafanyia kazi, kwa miaka yote hiyo wangepiga hatua.

Ndiyo maana wewe rafiki yangu, nimekuwa nakuambia ufanye kile ambacho Grant Cardone ametufundisha kwenye kitabu chake cha 10X RULE, kuchukua malengo yako na kuzidisha mara kumi, kisha kufanyia kazi malengo hayo mapya.

Fanya hivyo sasa, kama bado hujafanya, fanyia kazi malengo ambayo ni mara kumi na uliyonayo sasa. Zidisha kipato unachopata sasa mara kumi, na fanya hilo kuwa lengo lako ndani ya mwaka mmoja, fanya kila kinachopaswa kufanywa (kiwe halali) kuhakikisha unafikia lengo hilo. Hata kama hutalifikia, yaani hutapata mara kumi, utapata mara tano, au hata ukipata mara mbili, huoni ni bora kuliko mara moja? Kama sasa unapata milioni moja, baada ya mwaka ukawa unapata milioni 2 huoni 2 ni bora kuliko 1?

Anza sasa rafiki, ni MARA KUMI na KUFANYA KILA KINACHOPASWA KUFANYIKA.

Rafiki, hizo ndiyo nondo tano za juma hili la 20 la mwaka 2018. Nikukumbushe kulipangilia juma namba 21 tunalokwenda kuanza. Na hapo ulipo sasa, andika mambo yasiyopungua matano utakayofanyia kazi kwenye juma linaloanza, na mwisho wa siku, ukipenda, nishirikishe jinsi juma lako limekwenda kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz Na kama yapo uliyojifunza juma lililopita, ukayafanyia kazi juma hili, unaweza kunishirikisha pia kwenye email hiyo. Nitafurahi kusikia kutoka kwako, namna unavyofanyia kazi haya ninayokushirikisha kwenye TANO ZA JUMA na matokeo unayoyapata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji