Tumekuwa tunafikiri kwamba kinachotuzuia kufanikiwa na vile vitu ambavyo hatuvijui, hivyo kama tutajua vitu hivyo, kikwazo cha mafanikio kitaondoka.

Ni kweli tusichojua ni kikwazo kwetu kufanikiwa, lakini pia tunachojua kinaweza kuwa kikwazo kikubwa zaidi.

Na kwa wengi, kinachowazuia kufanikiwa siyo wasichojua, bali kile ambacho tayari wanajua.

Jua

Unakuta kile ambacho mtu anajua, na anakiamini kama ukweli kinatofautiana na msingi sahihi wa mafanikio.

Hivyo hata mtu anapojifunza mambo mapya kiasi gani, kama kile alichokipokea mwanzo kama ukweli na kukiamini hakijaondoka, mapya aliyojifunza hayatakuwa na maana.

Kwa mfano mtu anaweza kujifunza mengi kuhusu kupata fedha na utajiri, lakini kama ndani yake anaamini utajiri ni mbaya na matajiri ni watu wabaya, chochote alichojifunza kuhusu fedha hakitamsaidia.

SOMA; UKURASA WA 1106; Wale Unaowavumilia, Ndiyo Wanaokutengeneza…

Hivyo kabla hujajifunza kitu kipya, jiulize kwanza ulichojifunza mwanzo kuhusu eneo hilo bado ni sahihi? Anza kwanza kuhoji na kuchunguza kile unachojua tayari, maana kama kinapingana na maarifa mapya unayopata, maarifa hayo hayatakuwa na msaada kwako.

Kile unachojua, kinaweza kuwa hatari kubwa kwako kuliko unachojua, kwa sababu kinazuia chochote kipya kisifanye kazi.

Jifunze mambo mapya kila wakati, lakini pia usisahau kuondoa yale ambayo yameshapitwa na wakati au hayaendani na kile unachotaka kufikia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog