Siku ya kwanza ya kitu chochote, ni siku ambayo watu huwa wanakuwa na hamasa kubwa sana.
Si unaikumbuka siku ya kwanza kwenda shule, huenda hukulala, ulisubiri kwa hamu kuamka na kwenda shule. Kadhalika siku ya kwanza kusafiri kwenda mahali ambapo hujawahi kwenda.
Kumbuka pia siku yako ya kwanza ya biashara, au siku ya kwanza ya kazi. Hakika ilikuwa siku ya hamasa, siku uliyojiahidi utafanya makubwa kupitia kazi au biashara yako.

Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda, hamasa ilipungua na ikafika hatua ikawa siyo tena kitu unachopenda kufanya, bali ni kitu ambacho inakubidi tu ufanye. Umefikia hatua ya kuchoka, hutaki hata kufanya lakini huna namna. Mwili wako unakukataza kabisa usifanye, maana kila wakati hukosi uchovu, kuumwa hakuishi na sababu za kuahirisha mambo hazikosekani.
Kinachotokea mpaka hamasa inaisha, ni marudio ya kile unachofanya. Unapokuwa unaanza, kinakuwa ni kitu kipya kufanya, hivyo unakuwa na hamasa, unapoendelea kufanya unajikuta unarudia kufanya yale yale ambayo umekuwa unafanya kila siku, hivyo hamasa inashuka.
SOMA; UKURASA WA 1092; Badili Njia, Usibadili Maono…
Unaporudia kufanya kitu kile kile kila siku, lazima utakichoka, hiyo ni asili ilivyo. Kunywa soda moja utapata utamu wa soda, kunywa soda hiyo mara kumi na utakuwa ni mzigo.
Kwa maana hii basi, ili kuhakikisha hamasa tuliyonayo haifi au kupotea, tunahitaji kuwa na kitu kipya tunachoangalia kila siku. Kila siku kwenye kile tunachofanya, tunahitaji kuwa na upya, tunahitaji kuwa na kitu kipya tunachofanyia kazi, tunahitaji kuwa na tumaini jipya linalotuongoza na unahitaji kuwa na malengo makubwa sana tunayoyafanyia kazi.
Bila ya msukumo wa upya, hatutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu, maana chochote tunachofanya tutakizoea na hatutakuwa na hamasa ya kupiga hatua zaidi.
Kila unapojiona umezoea kile unachofanya, ni wakati wa kukaa chini na kuangalia vitu gani vipya unaweza kufanyia kazi. Na vipo vingi sana, kama utakuwa tayari kutafuta na kufanyia kazi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog