Habari za leo rafiki yangu?

Jana tarehe 28/05/2018 ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa, kwa sasa nimetimiza miaka 30 ya kuwa hai hapa duniani.

Miaka 30 ni michache kwa wengi na mingi kwa wengine. Kwa upande wangu miaka hii 30 imekuwa miaka ya kujifunza mambo mengi sana kuhusu maisha, watu na mafanikio.

Kila ninapofikia tarehe ya kuongeza mwaka mwingine kwenye maisha yangu, huwa natenga muda wa kuyatafakari maisha yangu, kuangalia nilipotoka, nilipo na ninapoelekea. Huwa nafanya tathmini ya kina ya kila ninachofanya na kuona ni kwa jinsi gani kinachangia au kukwamisha kufika kule ambapo ninataka kufika.

Na kipindi hichi pia nimepata nafasi ya kutafakari kwa kina kuhusu maisha yangu na kila ninachofanya. Katika tafakari hiyo, nimefikia maazimio mengi, ambayo nitakuwa nakushirikisha wewe rafiki yangu kidogo kidogo kadiri tunavyokwenda.

Kwa sasa ninakwenda kuanza muongo mpya kwenye maisha yangu, muongo wa nne wa uhai wangu hapa duniani. Huu ni muongo ambao kwenye maisha ya kila mtu una maana kubwa sana. Katika umri wa miaka 30 mpaka 40 ndiyo kipindi ambacho kila mtu anakuwa na ufanisi mkubwa sana kwenye maisha yake, kipindi ambacho mtu anakuwa ameshajifunza mengi kwa kujaribu jaribu mengi kwenye muongo uliopita na hivyo anakuwa ameshajua nini anataka kufanya na maisha yake.

Happy-30th-Birthday

Kwenye miaka hii 10 inayokuja ya maisha yangu, ni kipindi ambacho nitakwenda kujisukuma zaidi, nitakwenda kuweka juhudi kubwa mno kwenye maisha yangu ili kuweza kupiga hatua kubwa zaidi ya nilivyotarajia kupiga.

MALENGO MAKUBWA MAWILI NINAYOENDELEA KUFANYIA KAZI.

Malengo yangu makubwa kwenye maisha bado ni yale mawili ambayo kwa mara ya kwanza nilikushirikisha miaka mitano iliyopita.

Lengo la kwanza ni kuwa bilionea, bilionea kwa thamani ya dola za kimarekani. Ni lengo kubwa, lengo ambalo kwa wengi linaonekana gumu kufikia au lisiloweza kufikiwa, na kwa wengine wamekuwa wanasema ili nini. Lakini ni lengo ambalo sitaliacha na wala sina wasiwasi kwenye kulifikia, kwa sababu najua ninaweza na ninajua njia sahihi za kufikia lengo hili. Na kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha, sijaweka lengo hili kwa sababu ya fedha, bali nimeliweka kama kiwango cha juu kabisa cha kutoa huduma kwa wengine, kwa sababu imani yangu kwenye fedha ni kwamba fedha ni zao la thamani, kadiri unavyotoa thamani kubwa kwa wengine, ndivyo unavyolipwa fedha zaidi. Pia kwa kufikia lengo hilo, na hata kabla ya kulifikia, nitaweza kutoa mchango mkubwa kwa wengine, kupitia mchakato wa kuelekea kwenye lengo hilo. Mfano kutoa ajira, kutoa misaada kwa wenye uhitaji na kadhalika. Nikuhakikishie rafiki yangu lengo hili nitalifikia na sitalifikia mwenyewe, lazima wale ninaoambatana nao wafikie hatua kubwa kiasi hicho, nina imani na wewe utakuwa mmoja wao.

SOMA; Mambo 29 Niliyojifunza Kwenye Miaka 29 Ya Maisha Yangu Hapa Duniani.

Lengo kubwa la pili ni kuwa raisi wa nchi yangu Tanzania, mwaka 2040. Hili ni lengo jingine ambalo watu wamenieleza kwa kila namna kwa nini siwezi kulifikia au kwa nini nisijisumbue nalo. Lakini lengo hili lipo hai leo na litaendelea kuwa hai kila siku mpaka nitakapolifikia. Iwe nitalifikia kwenye mwaka huo 2040, iwe ni kabla ya mwaka huo au baada ya mwaka huo, lengo hili halitakufa na sina mashaka juu ya kulifikia.

Rafiki yangu, nilishaacha kusikiliza watu kuniambia nini naweza kufanya au siwezi kufanya, hii ni baada ya kugundua vitu vingi ambavyo watu walikuwa wananiambia siwezi kufanya siyo kwamba haviwezekani, ila ni kwamba wao hawajawahi kufanya na hawajawahi kuona mtu mwingine akifanya.

Kila siku ninapoamka ninayaandika malengo hayo makubwa mawili kwenye kijitabu changu, pamoja na malengo mengine ninayoyafanyia kazi. Kila siku najifunza na kuchukua hatua za kunifikisha kwenye malengo hayo mawili, na mengine makubwa. Na sitakuja kumsikiliza yeyote anayeniambia kuna kitu siwezi kufanya, na huu ni ushauri muhimu sana ninaoutoa kwako, bila ya kujali unataka nini na upo wapi.

Rafiki, katika kujumuisha miaka kumi ijayo ya maisha yangu, kwenye huu muongo muhimu sana wa maisha yangu, ninakushirikisha kauli hizi mbili muhimu sana, ambazo zilinifanya nitafakari sana siku za nyuma, na nitakuwa najikumbusha kila siku ili kuchukua hatua kubwa kwa kila siku ya maisha yangu.

KAULI YA KWANZA; NAJIWASHA MOTO, NJOO UNIANGALIA NIKIUNGUA.

“Set yourself on fire with passion and people will come for miles to watch you burn.” – John Wesley

Ukiwa mahali halafu kwa mbali sana ukaona moto unawaka, lazima utapata hamasa ya kwenda kuangalia moto huo unatokana na nini. Ukiwa unaendelea na shughuli zako ukasikia kuna mtu amejiwasha moto, utaacha kila unachofanya na uende kuangalia nani amejiwasha moto, na kwa sababu gani.

Hichi ndiyo ninachokwenda kufanya na maisha yangu, ninajiwasha moto, na ninakualika utoke popote ulipo, uje uniangalie nikiungua. Na ninaposema najiwasha moto simaanishi kwamba najiweka kwenye moto kweli, au najiunguza, bali namaanisha hatua ninazokwenda kupiga, zitakuwa hatua za tofauti kabisa, hatua ambazo hakuna aliyezizoea na hivyo utapata hamasa ya kutaka kujua ni kwa namna gani hatua hizo zinapogwa.

Ninaposema najiwasha moto, namaanisha kwamba hakuna kitakachonirudisha nyuma kwenye malengo ninayofanyia kazi, hakuna nitakachojali kwa yeyote atakayenisema vibaya au kunikatisha tamaa. Maana unapokuwa unawaka moto, chochote anachosema yeyote hakina maana kwako. Nitaendelea kujifunza kila siku, nitaendelea kupiga hatua kubwa kila siku na kuhakikisha kila siku mpya, nimefanya kitu kipya na cha kunisogeza mbele zaidi ya kile nilichofanya kwenye siku iliyopita.

Kujiwasha moto inamaanisha kutokujionea huruma au kujibembeleza, kwa sababu nilichojifunza kwenye haya maisha, lazima kutakuwa na mtu wa kukutawala. Hivyo unapaswa kuchagua kujitawala mwenyewe, au kama huwezi basi uchague mtu wa kukutawala. Kwa malengo makubwa niliyonayo, nikichagua yeyote anitawale sitaweza kuyafikia, hivyo nitajitawala mwenyewe, na nitajiendesha kwa kila linalopaswa kufanyika ili kufika pale.

Najiwasha moto, njoo unione nikiungua.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

KAULI YA PILI; NASAMBAZA NISHATI YA UPENDO, UKIJA UTALIPIA.

“Generate so much loving energy that people want to just come and hang out with you. And when they show up, bill them!” — Stuart Wilde

Kitu kimoja ambacho nashukuru sana kwenye maisha yangu ni kujifunza mapema sana msingi wa fedha. Ambapo fedha ni zao la thamani ambayo mtu unatoa kwa wengine. Na tangu nimejifunza msingi huu, umekuwa unafanya kazi kila wakati. Katika kipindi ambacho mapato ninayoingiza ni madogo, unakuta pia thamani ninayotoa ni ndogo. Na kila ninapoongeza thamani ninayotoa, fedha zinaongezeka, bila hata ya kuhangaika sana.

Maisha ni nishati, na nishati huwa haipotei, kwa kanuni za kisayansi. Nikukumbushe kidogo sheria ya nishati, ambayo inasema nishati huwa haitengenezwi, wala haiharibiwi, bali inabadilishwa kutoka mfumo mmoja kwenda mfumo mwingine. Kwa mfano jua linapowaka, linatoa nishati ya manga na joto, mwanga ukifika kwenye mimea unabadilishwa na kuwa nishati ya kemikali, sisi tunapokula mimea, tunapata nishati hiyo ya kemikali. Hivyo unapokula ugali, wali au mboga, unakula nishati ambayo imetoka kwenye jua, lakini kwa mfumo mwingine. Tunaweza kusema wote tunakula jua.

Hivyo fedha pia ni nishati, kadiri unavyotoa nishati kubwa, ndivyo unavyopata fedha zaidi. Ni sawa na mtu anaposema kadiri unavyotokwa jasho zaidi, ndivyo unavyolipwa zaidi. Maana kutokwa jasho ni kubadili nishati, kutoka kwenye kemikali kwenda kwenye nguvu unazoweka kwenye kazi unayofanya.

Katika kipindi cha miaka kumi inayokuja ya maisha yangu, nasambaza nishati kubwa sana ya upendo. Nitafanya kila kinachopaswa kufanya ili kutoa thamani zaidi kwa wengine, kwa sababu ninapenda kuona wengine wakitoka kwenye magumu, napenda kuona wengine wakipiga hatua na ninapenda kuona wengine wakiwa bora zaidi kila siku.

Nitasambaza nishati hii kwa kiwango cha juu sana, kiasi kwamba popote ulipo utataka kuungana nami, na utakapokuja sasa, utalipia.

Nikueleweshe vizuri hapo rafiki yangu, nitaweka juhudi kubwa sana kukushirikisha maarifa bora sana kupitia mtandao wa AMKA MTANZANIA, ambao ni bure kabisa kuusoma. Utakaposoma maarifa hayo, utatamani sana kukutana na mimi, utatamani sana kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu na pia utatamani sana kupata maarifa zaidi kutoka kwangu. Na hapo sasa, utakapotamani zaidi kutoka kwangu, itakubidi ulipie.

Hivyo rafiki yangu, chochote cha ziada utakachohitaji kutoka kwangu, utahitaji kwanza kuwa umejiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni huduma ya kwanza muhimu sana ninayoitoa kwa wale ambao wanataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao. Lakini haimaanishi kwamba usipojiunga hutajifunza, utajifunza sana, tena kwa asilimia 99, ila ukitaka asilimia 1 inayobakia, utahitaji kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Hii ina maana kwamba, kama umesoma chochote nilichoandika, kisha ukataka kuniuliza chochote au kukutana na mimi, au kuhitaji ushauri wangu, hutaweza kuupata kama hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Ninafanya hivi siyo tu kwa sababu nahitaji fedha, bali pia kupunguza matumizi mabaya ya muda wangu. Maana nilichojifunza kwa miaka mitano iliyopita, kadiri ninavyoweka thamani kwenye kazi zangu, ndivyo watu wengi wanataka kupata zaidi kutoka kwangu, lakini ninapowapa wengi muda wangu, hawafanyii kazi vizuri yale tunayojadili, na wakati huo muda ninaotumia nao nawapunja wale ambao wangeweza kujifunza na kuchukua hatua.

Rafiki yangu, ninakupenda sana, ndiyo maana kila siku nakushirikisha maarifa bora sana, ambayo yataweza kukukwamua hapo ulipo sasa. Lakini utakapohitaji zaidi, unahitaji kulipia.

Ada ya KISIMA CHA MAARIFA mpaka sasa ni shilingi elfu 50, ambayo imekuwa hivyo kwa miaka minne sasa, lakini itapanda. Wapo ambao wamekuwa wanasema ada hiyo ni kubwa na hawawezi kulipa. Kama na wewe ni mmoja wao rafiki, basi ni kitu kizuri sana. Iko hivi rafiki yangu, KISIMA CHA MAARIFA siyo huduma ya kuanzia unapojihusisha na huduma zangu, unapaswa kuanzia kwenye AMKA MTANZANIA, ujifunze, ufanyie kazi yale unayojifunza, kisha uone matunda yake mazuri. Kipato chako kiongezeke, uwe mtu bora na uweze kulipia huduma zaidi. Hapo sasa ndiyo unaweza kulipia ada ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo kadiri siku zinavyokwenda, itazidi kuongezeka.

Hii ina maana kwamba, kama maarifa ninayokushirikisha hayajawa na manufaa yoyote kwako, hupaswi kulipia chochote ninachokuambia ulipie. Unakuwa hujafikia vigezo bado. Ndiyo maana kama umewahi kuniandika kwamba ada ni kubwa, sijawahi kukujibu vibaya, bali nimekuwa najibu endelea kutembelea www.amkamtanzania.com kila siku, ujifunze na kufanyia kazi yale unayojifunza, kisha utapiga hatua na ikitokea hivyo, karibu ulipie na kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kama huduma ninazotia bure hazijakusaidia, usipoteze muda wako kulipia chochote ninachosema ni cha kulipia, hakitakusaidia pia. Jukumu langu ni kusambaza nishati ya upendo, ni kutoa maarifa bora sana, kukazana kwa kila linalopaswa kufanya kuhakikisha natoa thamani kubwa kwa wengine. Utakapovutiwa na nishati hii, ukataka zaidi kutoka kwangu, basi jiandae  kulipia.

Nikushukuru sana rafiki yangu kwa namna ambavyo tumeendelea kuwa pamoja. Ninajua ni kwa namna gani unaniamini na kufuata kile ambacho tunajifunza kila siku. Nakuahidi tutaendelea kuwa pamoja, na miaka hii kumi inayofuata, itakuwa miaka ya kupiga hatua kubwa sana, miaka ambavyo kama na wewe unaweza kujitoa, nakukaribisha sana twende pamoja.

Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA niseme kwamba kuna vitu unakosa na utakwenda kukosa vingi zaidi, karibu ujiunge na KISIMA ili tuendelee kuwa pamoja.

vitabu softcopy

MAENEO MANNE MUHIMU NINAYOKWENDA KUJIWASHA MOTO.

Nihitimishe kwa kukuambia maeneo manne ambayo nakwenda kuweka maisha yangu yote, nakwenda kujiwasha moto na ninakwenda kusambaza nishati kubwa ya upendo, ili uje popote ulipo, na uwe tayari kulipia.

MOJA; NITATIBU, mimi ni daktari wa binadamu, na kwa kipindi kifupi ambacho nimetoa huduma ya utabibu, nimeona ni kwa jinsi gani huduma hii inakosekana kwa wengi wenye uhitaji. Hivyo nimejitoa kutibu kwenye maisha yangu yote, ni nitafanikisha watu kuweza kupata matibabu bora zaidi na huduma bora za kiafya, kwa sababu afya ndiyo msingi mkuu wa maisha.

MBILI; NITAWAKOCHI WATU, Napenda kufanya kazi na watu, napenda kuona watu wakipiga hatua kwenye maisha yao, napenda kuona watu wakijifunza kupitia mimi. Hivyo nitaendelea kuwa KOCHA WA MAFANIKIO kwa wale wote ambao wanapenda kupiga hatua kwenye maisha yao, na wapo tayari kujitoa zaidi ya walivyozoea.

TATU; NITAANDIKA. Kila siku ninayoamka, kitu cha kwanza ninachofanya ni kuandika. Nimejiahidi kuandika kila siku ya maisha yangu, mpaka nitakapokufa. Yaani kama nikiamka nipo hai, nitaandika. Nimeweza kufanya hivi kwa miaka mitano sasa, na nitaendelea kufanya maisha yangu yote yaliyobakia. Uandishi wangu nitaegemea zaidi kwenye makala, vitabu na mafunzo (semina).

NNE; NITAENDELEA KUWA MJASIRIAMALI. Mjasiriamali ni mtu anayeona tatizo ambalo watu wanalo, kisha anakuja na suluhisho ambalo litawatatulia watu tatizo walilonalo, na anatengeneza fedha kupitia suluhisho hilo. Mara nyingi suluhisho linakuwa jipya na hatari, yaani siyo kitu kilichozoeleka. Haya ndiyo maisha ambayo nimechagua kuishi, maisha ya ujasiriamali, maisha ya kujaribu vitu vipya, vitu ambavyo vinaweza kuwa hatari. Hivyo ninatendelea kuwa mjasiriamali, nitaendelea kuja na suluhisho kwenye matatizo ambayo wengi wanapitia.

Ni hayo rafiki yangu, na nina imani tutaendelea kuwa pamoja, nategemea kukuona ukiwa karibu zaidi kwa miaka huu kumi inayokuja, na ninategemea wewe pia uweze kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi hichi.

Maana kama Zig Zigler alivyowahi kusema; unaweza kupata chochote unachotaka kupata, kama utawapa watu wengi zaidi kile wanachotaka. Hivyo ili mimi niwe bilionea, lazima nisaidie katika kutengeneza mabilionea na mamilionea zaidi. Je wewe hutaki kuwa sehemu ya mabilionea na mamilionea hao? Kama unataka, karibu sana tuambatane pamoja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji