Gharama halisi ya kitu ni kiwango cha maisha ambacho mtu umekipoteza kupata kitu hicho – Henry David Thoreau

Pablo Picasso (kuzaliwa; October 25, 1881, kufa; April 8, 1973) alikuwa mchoraji bora sana kuwahi kuishi hapa duniani.

Kuna hadithi kwamba siku moja Picasso alikuwa amekaa kwenye mgahawa, mama mmoja akamfuata na kumpa leso yake akimwambia, Picasso, naomba unichore sura yangu kwenye hii leso, nitakulipa chochote unachotaka. Picasso akatoa penseli kwenye mfuko wake, akachukua leso na kuchora sura ya mwanamke yule, alipomaliza alimkabidhi mchoro huo, mwanamke yule alifurahia sana, picha yake ilikuwa nzuri sana.

Baada ya kupokea picha, mwanamke yule akamuuliza Picasso, unanidai kiasi gani? Picasso akamjibu dola elfu 10 (tsh milioni 20). Mwanamke akashtuka na kupigwa na butwaa na kumuuliza, unanitozaje fedha nyingi hivyo wakati umetumia dakika moja tu kuchora picha hii? Picasso akamjibu, ndiyo imenichukua dakika moja kuchora picha yako, lakini ilinichukua miaka 40 ya kuchora kuweza kufikia kiwango kikubwa cha uchoraji. Hivyo hulipii dakika moja  ya mchoro, bali unalipia miaka 40 ya uzoefu.

Rafiki, leo tumeanza na hadithi hiyo fupi ya mchoraji Picasso ili tuweze kuelewana vizuri, kwa sababu tunachokwenda kujifunza leo, ni kizito kidogo na ni rahisi kutokuelewa dhana nzima.

nipe pesa au nipe muda.jpg

Siku za nyuma nilikuandikia makala kwamba unastahili kulipwa (unaweza kwa kubonyeza maandishi haya), nikieleza umuhimu wa watoa huduma mbalimbali za mafunzo na ushauri kutokuogopa kuwatoza watu fedha kwa huduma zao. Makala hiyo ilipokelewa vizuri sana na waandishi na washauri wengi, kiashiria kwamba tatizo hilo ni kubwa kwa wengi.

Kuna swali ambalo nimekuwa napata kwa wengi, likiuliza vipi kwa wale wanaosema gharama ni kubwa na hawawezi kuzimudu? Swali jingine ambalo limekuwa linaulizwa ni vigezo gani vya kutumia katika kuweka gharama za huduma hizi? Na swali la tatu vipi kwa wale wanaobeza kwamba gharama unazotoza hazistahili au wanakuita tapeli au mwenye njaa kwa kutaka ulipwe kwa ushauri?

Makala ya leo, inakwenda kujibu maswali hayo na kukupa msingi sahihi wa kuendesha huduma zako kwa mipango yako mwenyewe na siyo kwa kusikiliza maoni ya wengine, ambao hawajui ni ugumu kiasi gani unapitia katika kuandaa huduma zako.

Swali la kwanza; gharama zipo juu na siwezi kuzimudu.

Kwa wale wanaokuambua gharama unazotoza zipo juu na hawawezi kuzimudu kwanza kabisa usiumie, na pili washukuru kwa kukuambia gharama zipo juu. Halafu waambie kwa nini gharama hizo zipo juu, sababu ya gharama kuwa juu utajifunza hapo chini.

Lakini unapaswa kujua kitu kimoja muhimu sana, hakuna kitu chochote watu wanaweza kukimudu, ni mpaka pale wanapokuwa na uhitaji hasa.

Chukua mfano huu, unazama kwenye maji, umeshajitahidi kuogelea mpaka umechoka na sasa unaanza kuzama, anatokea mtu anauza maboya, je utakuwa tayari kulipa kiasi gani ili upate boya? Je utaanza kuomba kupunguziwa bei ya boya, ambalo unajua ndiyo uhai wako? Jibu ni hapana, utalichukua boya kabla hata hujajua gharama yake ni kiasi gani, kwa sababu usipofanya hivyo utakufa.

Hapa kuna kitu muhimu sana cha kujifunza, ukiona mtu anasema kitu ni ghali au hawezi kukimudu, anachosema ni kwamba bado hajaona thamani halisi ya kitu hicho katika kumtoa pale alipo sasa. Maana akiiona thamani, ataweza kumudu.

Hivyo kwa huduma yoyote unayotoa, badala ya kuwabembeleza watu wakuonee huruma na kukubaliana na kiasi unachotoza, waoneshe watu thamani ambayo wanakwenda kuipata. Na thamani hiyo, iwe angalau mara kumi ya kiasi cha fedha ambacho unawataka walipe.

Kwa asili, sisi binadamu ni wabinafsi, pale ambapo tunajua tunapata zaidi, huwa tunachukua hatua. Kama kwa mtu kukulipa elfu moja anaweza kupata elfu kumi, elfu moja siyo kitu kwake, hata kama hana, ataitafuta.

Hivyo kila mtu anaweza kumudu chochote kama ataielewa thamani halisi ya kitu hicho.

SOMA; Najiwasha Moto, Njoo Unione Nikiungua (Azimio La Miaka Kumi Ijayo Ya Maisha Yangu).

Swali la pili; vigezo vya kutumia kupanga bei.

Tumeianza makala hii kwa kauli kutoka kwa Thoreau na hadithi ya Picasso, hivi viwili vinaonesha thamani ya muda kwenye kile ambacho unakifanya.

Kigezo kikuu cha kutumia kupanga bei za huduma zako ni muda ambao umetumia kwenye kujifunza na kujiandaa kutoa huduma hizo.

Nilisema hili kwenye makala ya unastahili kulipwa na nalisema hapa pia; wakati wewe unajifunza mambo hayo unayojua, wakati wewe unatengeneza mafunzo au ushauri unaotoa na kujaribu au kuupima kwako binafsi, watu wengine walikuwa wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Walikuwa wanafanya kazi zao na kulipwa, walikuwa wanastarehe na mengine mengi. Lakini wewe ulipoteza sehemu hiyo ya maisha yako, je nani anailipa sehemu hiyo ya maisha uliyowekeza katika kuandaa huduma hiyo?

Hivyo kigezo kikuu cha bei ni muda uliotumia katika kujifunza na kutoa huduma zako, ujuzi na uzoefu ambao unaendelea kujijengea, kadiri unavyoweka muda kwenye kitu, ndivyo unavyopaswa kutoa thamani kubwa zaidi na hivyo kutoza gharama za juu zaidi.

Kigezo kingine muhimu ni thamani ambayo mtu anaipata kwa ile huduma ambayo unampatia. Hakikisha kiwango chochote unachotoza, basi mtu anakwenda kupata thamani ambayo ni mara kumi ya gharama anayolipa.

Usianze kuweka gharama zako kwa kujiuliza watu wanaweza kumudu kiasi gani, inapokuwa kwenye fedha, hakuna mtu anaweza kumudu chochote. Lakini kila mtu anaweza kumudu thamani ambayo anaitaka, hivyo anza na thamani, weka bei na watafute watu sahihi wanaoielewa thamani hiyo na washawishi kufanya kazi na wewe.

SOMA; Mambo 40 Kuelekea Miaka 40 Ya Maisha Yangu (Na Vitabu Vitano Muhimu Unavyopaswa Kusoma Kwenye Maisha Yako).

Swali la tatu; unatoza gharama kwa sababu ya njaa na utapeli.

Sasa kuna wale ambao kejeli huduma zako, na kukuambia hustahili kutoza watu, tena siyo kiwango cha juu kama unavyotoza.

Chukua mfano huu; umekaa chini na kutafiti kisha ukaandika makala bora sana kuhusu kilimo cha nyanya, mwisho wa makala ukaweka maelezo kwamba anayetaka ushauri wa karibu na hata usimamizi katika kilimo cha nyanya awasiliane na wewe.

Unapokea simu ya msomaji, anakushukuru sana kwa maarifa ambayo umetoa kuhusu kilimo cha nyanya, na kukwambia amekuwa anafanya makosa huko nyuma. Hivyo anataka ushauri wako na umfuatilie kwa karibu katika kilimo chake cha nyanya. Unamwambia sawa, una huduma ya aina hiyo na kumweleza gharama anazopaswa kulipa. Kusikia gharama anapigwa na butwaa na kuanza kusema, unatozaje gharama kubwa hivyo, mimi ni mkulima mdogo tu, nilijua upo kwa ajili ya kutusaidia watu kama sisi, kumbe na wewe una njaa kama wengine tu, kumbe na wewe ni sehemu ya matapeli.

Maneno kama hayo yanaweza kukuumiza sana, ukifikiria kwamba hukumfuata mkulima huyo shambani kwake kumlazimisha akupe fedha, badala yake umeandaa maarifa yanayoweza kumsaidia, na kuyashirikisha. Amekutana nayo, ameona yanaweza kumsaidia, lakini hayupo tayari kulipa gharama.

Katika hali kama hii, jibu lako linapaswa kuwa moja; mwambie mtu akupe fedha na ufanye naye kazi, au akuachie muda wako na ufanye nao mambo mengine.

Tumeshaona kwamba maarifa uliyonayo hujayaokota, umepoteza sehemu ya maisha yako kupata maarifa hayo. Halafu kirahisi tu mtu anakuja kukuambia una njaa au ni tapeli.

Muda ambao wewe ulikuwa unatafiti na kupata maarifa bora ya kilimo cha nyanya ni muda ambao yeye alikuwa anaendelea na maisha yake mengine. Muda ambao anataka wewe uwe unamfuatilia kwenye kilimo chake, anatengeneza thamani kwenye kilimo chake na wewe huwezi kutumia muda huo kwenye mambo mengine, je nani ataulipa muda huo?

Ndiyo maana nakuambia uwape watu machaguo mawili, amekutana na maarifa yako, ameyapenda na anataka zaidi kutoka kwako, basi anapaswa kulipa gharama ambazo ni maisha uliyowekeza katika kuandaa maarifa hayo. Hawezi kulipa gharama hizo basi akuachie muda wako na uutumie kwenye mambo mengine. Usiruhusu muda wako utumike na wale ambao hawathamini kile ambacho unakifanya.

Muda ndiyo kipimo halisi cha maisha yako, usikubali kuupoteza, ulinde na kwa yeyote anayetaka muda wako, basi lazima awe tayari kugharamia muda huo.

Nikikumbushia hapa vitu vingine nilivyoshauri kwenye makala ya unastahili kulipwa;

  1. Kuwa na mafunzo ya aina mbili, ya kwanza ni ya bure kabisa ambayo kila mtu anaweza kuyapata. Na ya pili ni ya kulipia ambaye mtu akitaka kuyapata ni mpaka alipe. Ambaye hawezi ya kulipia mshauri apate yale ya bure, ayatumie mpaka atakapoweza kulipia.
  2. Kuwa na viwango mbalimbali vya huduma, kuanzia gharama za chini mpaka za juu. Mfano unakuwa na blog ambayo ina makala za bure, halafu una kitabu/vitabu ambacho mtu akisoma atajifunza mengi, gharama yake inakuwa kiasi kidogo, halafu una kundi la wale ambao wanataka kujifunza zaidi ambapo kuna ada wanalipa, halafu kuna huduma ya ushauri au usimamizi ambayo ni ya mmoja mmoja na gharama zake zipo juu. Kama mtu anakuja moja kwa moja kwenye huduma ya juu na kusema hawezi kumudu, mshauri aanze na huduma za chini.

Kama umeamua kufanya biashara ya utoaji wa huduma za mafunzo na ushauri, lazima ujue ni thamani gani hasa unayoitoa na unawalenga watu gani na kisha uwe tayari kutoza kulingana na thamani unayotoa. Usiyumbishwe na wakatishaji tamaa au wabezaji wa huduma zako, simamia kile unachofanya kwa kukiamini na kukithamini, na ambaye anaona hawezi kukupa fedha unazotaka, basi mwambie asichezee muda wako.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania