“There is almost one time that is important – Now! It is the most important time because it is the only time when we have any power.” — Leo Tolstoy
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SIKU PEKEE UNAYOIMILIKI…
Siku pekee unayoimiliki ni leo,
Na muda pekee unaomiliki ni sasa.
Muda wako na siku yako ndiyo vitu muhimu sana unavyomiliki kwenye maisha yako.
Chochote unachotaka kweye maisha yako, utaweza kukipata kama utatumia vizuri muda huu ulionao, ukianza na sasa, ukianza na leo.
Imiliki siku yako ili uweze kuyamiliki maisha yako.
Ipangilie siku yako, pangilia kila saa yako ya siku.
Usiache uwazi kwenye muda wa siku yako, utakaribisha matatizo makubwa kwenye maisha yako.
Mambo muhimu sana ya kuzingatia leo;
👉🏼Chochote muhimu ulichopanga kufanya leo kifanye, usiahirishe.
👉🏼Anza kufanya vile ambavyo ni muhimu zaidi kabla hujafanya vingine.
👉🏼Chochote unachofanya, weka akili yako na nguvu zote hapo, kama hakistahili kupata akili na nguvu zako zote, usikifanye.
👉🏼Muda ulionao sasa ukishapita haurudi tena, ukipotea umepotea moja kwa moja.
👉🏼Unaowaona na mafanikio makubwa wana muda sawana wewe, masaa 24 ka siku, wameyapangilia na kuyaishi vizuri.
👉🏼Kama unasema huna muda wakufanya kitu ambacho ni muhimu, lakini unapata muda wakuangalia tv, kutembelea mitandao ya kijamii na kubishana kuhusu jambo lolote, hujui unafanya nini na maisha yako.
Rafiki, muda ulionao ni sasa, siku pekee unayomiliki ni leo.
Hakikisha unatumia vizuri kila muda unaokuwa nao, na ukiangalia nyuma uone kitu cha msingi ulichofanya na muda wako.
Ukawe na siku bora sana leo, siku ya kufanya makubwa.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha