“Expect nothing, and you will enjoy everything!”
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USITEGEMEE CHOCHOTE, ILA WEKA JUHUDI…
Kinachotuangusha kwenye maisha, kinachotufanya tukate tamaa, kinachopelekea tukose hamasa, ni mategemeo yetu.
Huwa tunategemea hatua moja tunayochukua ilete matokeo makubwa sana.
Huwa tunategemea kila tunachowafanyia watu wakikubali mara moja na kutupa kile tunachotaka.
Huwa tunategemea dunia iende kama tunavyotaka sisi iende.
Lakini hivi sivyo dunia inavyofanya kazi,
Dunia haijiendeshi kama yeyote anavyotaka, bali yenyewe inavyoenda.
Watu hawatafanya kama unavyotaka wewe, bali wanavyotaka wao.
Kila unachofanya hakitaleta matokeo ya haraka kwako, bali kinajenga matokeo makubwa ya baadaye.
Hivyo mwanamafanikio, njia bora ya kwenda na hii dunia, njia bora ya kuhakikisha hatujiangushi na kukata tamaa ni kutokutegemea chochote.
Usitegemee chochote, bali wewe fanya kwa juhudi zako zote, fanya kile ambacho umechagua kufanya, na jua kitatokea kitakachotokea.
Usitegemee dunia iende kama unavyotaka,
Usitegemee watu wafanye vile unavyotaka wewe,
Usitegemee kupata matokeo kwa wakati unaotaka,
Usitegemee kila unachofanya kilipwe kwa namna unavyotaka.
Lakini usiache kuweka juhudi,
Usiache kuwa na ndoto kubwa,
Usiache kujifunza kila siku,
Usiache kujaribu mambo mapya na makubwa kila siku.
Kutokutegemea chochote haimaanishi kukata tamaa, au kuwa mvivu au kwenda tu na mambo yanavyoenda.
Bali kunamaanisha umeshakomaa na unajua juhudi unazoweka siyo lazima zilete matokeo unayotaka kwa wakati unaotaka, lakini unajua juhudi hizo ni nzuri.
Kila unapokuwa na mategemeo makubwa na ukakatishwa tamaa, angalia asili inavyoenda, angalia mti wa mwembe ambao kila msimu unazalisha maembe, lakini hakuna anayeuambia asante.
Angalia ng’ombe ambao kila siku wanazalisha maziwa lakini hakuna anayewaambia asante.
Kisha gundua kwamba, uko hapa duniani kufanya vitu, kuzalisha thamani, kutoa kile ulichonacho.
Matokeo, yasikusumbue sana, wewe fanya.
Kadiri unavyofanya kilicho sahihi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi kubwa ya kifanikiwa.
Uwe na siku bora sana leo,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha