Hivi ni vitu vitatu ambavyo kila mtu anavipigania, vitu vitatu ambavyo vinayafanya maisha ya yeyote kuwa bora sana.

Kila mtu anapenda kuwa huru, kufanya maamuzi yake, kuendesha maisha yake, kufanya kile ambacho ni muhimu kwake. Lakini uhuru hauji bure, uhuru unahitaji kufanyiwa kazi na pia unakuja na majukumu. Wakati mwingine uhuru ni mgumu kuliko hata utumwa, ndiyo maana wengi wakipewa nafasi ya kuonja uhuru na utumwa, wengi hujipeleka kwenye utumwa. Maana kwenye utumwa huhitaji kufanya kazi ngumu ya kufikiria, lakini kwenye uhuru, usipofanya kazi hiyo ngumu ya kufikiri, unapotea.

Mitandao

Utu ni kitu muhimu kwa kila mtu, kuheshimiwa kama mtu, kutambuliwa na kuthaminiwa kwa mchango ambao mtu anatoa ni kitu ambacho kila mtu anapenda. Lakini utu pua hauji kirahisi, utu unafanyiwa kazi. Utu unatengenezwa, kupitia juhudi ambazo mtu anaziweka, katika kujitengeneza kuwa mtu bora na kutoa thamani kwa wengine. Hukai chini na kusema natengeneza utu wangu, bali unafanya kile ambacho ni muhimu, na watu wanakutengenezea utu wako.

SOMA; UKURASA WA 1170; Maisha Yakiwa Mteremko Sana Unasahau Maono Yako…

Utajiri ni muhimu kwa kila mtu, fedha ni muhimu sana kwa mambo yanayohusu fedha, ambayo kwa dunia ya sasa, ni pumzi pekee, na ukiwa hujaumwa, ndiyo unapata bure. Utajiri unapatikana kwa kazi na juhudi, kwa mipango na utekelezaji, kwa kujua kwenye unataka utajiri na kufanyia kazi kuupata. Utajiri haupatikani kwa kujifanya hujali fedha au utajiri siyo mzuri. Utajiri ni mzuri na unayafanya maisha kuwa mazuri. Hata kama utajiri haununui furaha, unapojikuta katikati ya kula na kulala njaa, swala la furaha halina nafasi.

Mambo haya matatu yafanyie kazi kila siku kwenye maisha yako, uzuri yanaanza na maamuzi yako mwenyewe, yanaanza na juhudi zako mwenyewe. Chagua kuwa huru kwa kuwa tayari kulipa gharama za uhuru, chagua kufanya wengine wakupe utu wako kwa kuwa bora kila wakati, na hakikisha unakuwa tajiri, kwa sababu fedha ni muhimu kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog