“Who has Why live can bear with any how”

Habari za asubuhi mwanamafanikio?
Ni siku nyinyine nzuri sana kwetu, siku bora na ya kipekee kwetu.
Tumepata nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa maingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNAPOKWAMA RUDI HAPA.
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, utakutan na wakati mgumu.
Kwanza itaanzia ndani yako binafsi, utapanga kufanya kitu lakini muda wa kufanya itakapofika unafikiria kuahirisha, au unaona ni vigumu kufanya.
Itatokea kwa wengine pia, ambao hata hujawaomba ushauri, lakini watakuwa wa kwanza kujitolea kukushauri, na watataka ufuate ushauri wao.
Hapo bado wale ambao wanakukatisha tamaa, wakikuambia huwezi au itashindwa.
Halafu sasa, unakutana na kushindwa kwenyewe.

Kwa hayo yote, huu mchezo wa mafanikio unaweza kuwa mgumu sana.
Lakini ili kuendelea kwenda, ili kuepuka kuishia njiani, unapokwama, rudi kwenye KWA NINI yako.
Unahitaji kuwa na KWA NINI unafanya chochote unachopanga kufanya.
Na kwa nini hiyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa, nguvu ya kukusukuma hata mambo yanapokuwa magumu.
Nguvu ya kukufanya uone yale wanayosema wengine ni kelele tu.

Unahitahi kuwa na kwa nini itakayokusukuma kutoka kitandani pale unapojiuliza uamke au la.
Unahitaji kwa nini ya kukufanya uendelee pale unapokutana na ugumu.

Ijue kwa nini yako, na mara kwa mara rudi kwenye kwa nini hiyo ili usiishie njiani.
Ukiwa na kwa nini kubwa, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia.
Na mwamuzi wa mwisho inapaswa kuwa kwa nini yako, na siyo ugumu au maneno ya yeyote.

Uwe na siku bora leo, siku ya kuiishi kwa nini yako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha