Kila mtu anapenda kufanikiwa, kila mtu anatamani kufanikiwa.

Lakini mwisho wa siku, wachache sana ndiyo wanaoishia kufanikiwa. Wengi waliotamani kufanikiwa wanaishia kuwa kawaida na hata wengine kushindwa kabisa.

Katika wale wanaoshindwa, siyo wote ambao hawajakazana, wapo ambao wamekazana na kujitoa sana, lakini bado wanakuwa hawafanikiwi. Hawa ndiyo wanaoishia kufikiri kwamba huenda mafanikio ni bahati na kwao haikuwa bahati.

Ukweli ni kwamba, mafanikio siyo bahati, na kama bahati inachangia kufanikiwa, basi inakuwa ni matokeo ya maandalizi kukutana na fursa. Mafanikio hayaanguki tu kwa mtu aliyelala na kutamani mafanikio yatokee. Bali mafanikio yanatokea kwa yule anayetaka kufanikiwa, anajua kanuni za mafanikio, anajua ufunguo muhimu wa mafanikio na anaweka juhudi kupata mafanikio hayo.

key2success

Kanuni za mafanikio ni nyingi na tumekuwa tunajifunza kila mara. Wengine wanaziita siri za mafanikio, licha ya kwamba hazina usiri wowote. Kanuni za mafanikio zipo wazi, kujua kile ambacho mtu unataka hasa, kuweka kazi kwa juhudi kubwa, kujifunza kila siku na kujaribu mambo mapya ni muhimu sana ili kufanikiwa.

Leo nakwenda kukushirikisha ufunguo muhimu sana wa mafanikio. Huu ni ufunguo ambao utakufungulia mafanikio yako popote pale unapotaka kufanikiwa. Iwe ni kwenye kazi, biashara, au huduma yoyote, kwa kuwa na ufunguo huu, hakuna kitakachokushinda. Huu ni ufunguo ambao unafungua kila aina ya kufuli.

Ufunguo muhimu wa mafanikio tunaokwenda kujifunza hapa ni KUTATUA MATATIZO MAGUMU NA YALIYOSHINDIKANA.

Iko hivi rafiki, watu wana shida, watu wana uhitaji, watu wana changamoto na watu wanapenda maisha yao yawe bora zaidi. Mambo ambayo yanafanya maisha ya wengi kukwama ni magumu, ambayo yanawasumbua sana. Kwa jinsi mambo hayo yalivyo magumu, watu hao wanakuwa tayari kulipia suluhisho linalofanya maisha yao kuwa rahisi zaidi.

SOMA; Sheria Tatu Za Kimafanikio Ambazo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuzijua.

Na hii ndiyo sababu kwa nini teknolojia imeweza kuboresha maisha ya wengi na kila aliyetumia teknolojia vizuri ameweza kufanikiwa sana. Kwa mfano watu wanahitaji kufanikiwa kwa haraka, ujio wa simu umerahisisha sana hilo, watu wanapenda kujua kila kinachoendelea kwenye maisha ya wengine na dunia kwa ujumla, mitandao ya kijamii imetatua hilo vizuri. Utaona jinsi makampuni ya simu na mitandao ya kijamii yanavyokuwa na mafanikio makubwa.

Wewe unaanzia wapi?

Kwenye kila eneo la maisha ya watu, kuna maumivu ambayo watu wanayo, iwe ni kwenye afya, chakula, mahusiano, kazi, biashara, kuna changamoto ambazo wengi wanapitia.

Unaweza kuanzia popote ambapo unajali wewe, yaani una uwezo na uelewa wa matatizo ya eneo gani la watu. Iwe ni kwenye afya, elimu, chakula, mahusiano na kadhalika. Anzia lile eneo ambalo wewe una ujuzi au uzoefu nalo. Kisha angalia ni shida gani kubwa kabisa ambayo watu wanayo, shida ambayo inawakwamisha wengi kupiga hatua, kisha angalia ni kwa namna gani unaweza kutatua changamoto hiyo.

Itumie akili yako kufikiri kwa kina, angalia suluhisho ambalo kwa sasa linapatikana kisha ona ni kwa namna gani unaweza kuboresha zaidi. Angalia kipi kipya ambacho unaweza kukifanya na watu wakapata ahueni zaidi.

Kwa kuwa matatizo ya watu bado yako, kwa kuwa watu bado wanalalamika kuna changamoto, basi kuna fursa kubwa ya kila mmoja wetu kufanikiwa sana. Fursa hiyo ni kuja na suluhisho la changamoto za watu, kuja na njia ya kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na wao watakuwa tayari kukulipa chochote unachotaka kulipwa.

MIMI NI MSHINDI

Angalizo, kuelewa hili na kupanga ni rahisi, lakini kutekeleza kunahitaji kazi. Kuna sababu kwa nini mpaka sasa hakuna mtu aliyekuja na suluhisho la tatizo ambalo umeona linawasumbua watu. Ni kazi ngumu, inayohitaji kujitoa hasa. Hivyo kama unachofikiria ni njia ya mkato na ya haraka ya kufanikiwa, kutumia hii ni kujidanganya. Unahitaji muda, unahitaji kazi yenye maana ili kupata kile mafanikio makubwa.

Chagua tatizo kubwa na gumu lililowakwamisha wengi, kisha weka maisha yako kwenye kutafuta suluhisho la tatizo hilo, na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog