Ni vitu viwili tofauti kabisa, visivyo na uhusiano wa karibu.

Wengi hufikiri wakiwa bize, wakionekana wana mambo mengi basi ndiyo wanakuwa na uzalishaji mkubwa.

Lakini uhalisia ni kwamba, kuwa bize ni kiashiria cha uzalishaji mdogo. Watu wanaokuwa bize mara nyingi huwa wanashindwa kupangilia vipaumbele vyao, na hilo linawafanya kuwa na ufanisi mdogo.

Huhitaji kuwa bize ili kufanikiwa, na mara nyingi ukiwa bize wala hufanikiwi, unaishia kuchoka, unaishia kuwa na msongo wa mawazo na hata kushindwa kupiga hatua kubwa.

Kila Changamoto

Unachohitaji ni kuwa na kipaumbele, kujua ni kitu gani muhimu zaidi kwenye maisha yako, kisha kuacha vingine vyote mpaka kile ambacho ni muhimu kikamilike.

Kipaumbele ndiyo kanuni muhimu ya mafanikio. Kwa sababu muda wetu ni mdogo, na nguvu zetu zina ukomo. Kujaribu kufanya kila kitu kunamaliza nguvu zetu na kupoteza muda wetu. Lakini tunapochagua kufanya machache muhimu, tunatumia vizuri nguvu na muda wetu.

Usikazane kuwa bize, usitake kufanya kila kitu na usijaribu kutaka kuonekana unafanya zaidi ya kawaida. Chagua yale machache kabisa, kisha weka juhudi zako zote kwenye ufanyaji huo.

SOMA; UKURASA WA 804; Kama Kila Kitu Ni Kipaumbele, Huna Kipaumbele….

Kama una orodha ya vitu kumi vya kufanya, unahitaji kupanga vitu hivyo kulingana na umuhimu wake. Kwa kuanza na kile ambacho ni muhimu zaidi kisha kuelekea kisicho muhimu. Baada ya hapo unaanza kufanya kile ambacho ni namba moja kwenye umuhimu. Na hapo huendi kwenye kitu namba mbili kama namba moja bado hakijaisha. Unaona jinsi ambavyo huhitaji kuwa bize, maana unafanya kile muhimu zaidi, kikiisha unaenda kwenye kingine kinachofuatia kwenye umuhimu.

Mwisho kabisa, ili kuepuka ubize, sema hapana mara nyingi uwezavyo, kwa kifupi usiogope kusema neno hapana. Maana neno hapana ndiyo mkombozi wako wa kukuepusha na ubize usio na umuhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog