Kitu kimoja ambacho sisi binadamu huwa tunakosea, ni pale tunapopata nafasi ya kujikadiria, huwa tunajikadiria vibaya, mara zote.
Kama umewahi kupanga muda wa kumaliza kitu, au kupanga bajeti, umeshakutana na hili mara nyingi. Mara zote vitu huwa vinachukua muda mrefu kuliko tulivyokadiria, na pia vinachukua gharama kubwa kuliko tulivyokadiria.

Upande wa pili wa hili ni kwenye madhaifu yetu na ubora wetu. Kuna maeneo ya maisha yetu ambayo tunajijua tuna udhaifu, lakini udhaifu tunaojikadiria nao huwa ni mkubwa kuliko uhalisia. Kadhalika kwenye ubora, yapo maeneo ambayo tunajijua tupo bora, lakini pia huwa tunajikadiria zaidi, kwa kufikiri tuna ubora mkubwa kuliko tulivyo kwa uhalisia.
Ili kuepuka makosa haya tunayofanya kwenye kujikadiria, tunapaswa kujiwekea nafasi ya kuwa tumekosea. Tunapaswa kujua mambo hayapo kama vile tunafikiri yapo, na mambo hayataenda kama tunavyotaka yaende. Tunahitaji kuweka nafasi ya mambo ya tofauti.
Usijiumize sana pale unapopata matokeo tofauti na matarajio yako, pale unapotumia muda mwingi kuliko ulivyopanga, au fedha nyingi kuliko bajeti uliyoweka, na unapokuwa unapanga muda au fedha, ongeza kiasi cha kutosha yale usiyotarajia.
SOMA; BIASHARA LEO; Epuka Kosa Hili La Muda Unapoanza Biashara Yako.
Kadhalika kwenye madhaifu na ubora, jipe nafasi kwamba hutakuwa dhaifu kama unavyojifikiria, pia hautakuwa bora kama unavyojiona upo. Hii pia inakupa nafasi ya kuendelea kujifunza na kuwa bora zaidi kila siku. Unapojipa nafasi kwamba haupo dhaifu kama unavyofikiri, unajipa hamasa ya kuwa bora zaidi. Na hata unapojitambua sana unaweza usiwe bora kama unavyojifikiria, utaondoa hali ya kujiona tayari umeshamaliza kila kitu, na hivyo kuendelea kuweka juhudi ili kuwa bora zaidi.
Chochote unachojikadiria kwenye maisha, jipe nafasi ya kujikadiria vibaya na hivyo chukua hatua ili kuhakikisha makadirio unayokosea hayawi kikwazo kwako kupata unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog