AMKA mwanamafanikio,
Na siyo tu uamke kutoka kitandani, bali amka kutoka ndotoni, amka kutoka kwenye mawazo duni ya kifanya vitu kw mazoea, kufanya vitu kwa kawaida.
Amka kutoka kwenye kujiandaa kuishi na amka uanze kuishi leo.
Maana muda pekee ulionao ni huu, na unaweza kufanya chochote unachotaka na maisha yako, kama utatumia muda wako vizuri.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, na mwongozo wetu kwa mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA. Hivi viwili vinapaswa kutuongoza kwenye kila maamuzi tunayofanya kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NJIA SAHIHI YA KIFANYA KISICHO SAHIHI;
Jibu fupi; HAIPO.
Hakuna njia sahihi ya kufanya kitu ambacho siyo sahihi.
Kama kitu siyo sahihi, hata ukifanyeje, hakitabadilika, kitaendelea kutokuwa sahihi.
Haijalishi unakimbia mbio kiasi gani, kama uelekeo wako siyo sahihi hutafika unakotaka kufika.
Haijalishi unaweka juhudi kiasi gani, haijalishi unatumia muda wako kwa ufanisi kiasi gani, kama malengo unayofanyia kazi siyo sahihi kwako, juhudi na muda havitakusaidia.
Jambo la kwanza muhimu kabisa kujiuliza na kuangalia kabla hujafanya chochote ni kuangalia kama ni kitu sahihi kwako kufanya. Na kama ni sahihi unahitaji kujua kama ndiyo kitu muhimu zaidi kwako kufanya.
Haijalishi hata kama kila mtu anafanya,
Haijalishi hata kama kuna watu wananufuaika na kitu hicho,
Kama siyo sahihi, usifanye.
Maisha yanakuwa rahisi sana, pale unapoweza kufanya maamuzi ya aina hii kwenye maisha yako, kwa kutumia misimamo yako na malengo uliyonayo.
Maisha yanakuwa magumu pale unapofanya maamui ya aina hii kwa kuangalia wengine wanafanya nini au wanasemaje.
Kila unapojikuta njia panda, iwe ufanye au usifanye kitu, jiulize je ni sahihi kufanya? Na kama ni sahihi kufanya, je ni sahihi kwako kufanya ukizingatia malengo makubwa uliyonayo? Kama majibu ni hapana, usifanye. Ni hivyo tu, huhitaji kupoteza muda mwingi kujishawishi kwamba hakuna ubaya ukifanya. Kama siyo sahihi usifanye.
Ukawe na siku bora sana ya leo mwanamafanikio, siku ya kufanya kilicho sahihi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha