Rafiki yangu mpendwa,

Kila mmoja wetu kuna vitu ambavyo anavitaka kwenye maisha yake. Iwe ni vitu vidogo au vikubwa, maisha yetu yanakuwa na mahitaji mengi ili yaweze kwenda kama tunavyotaka yaende.

Lakini inaonekana kama kuna watu ambao wanaweza kupata chochote wanachotaka, huku wengine wakiwa hawana uwezo huo. Ni kama vile wale wanaopata wanachotaka wana bahati au wanapendelewa, na wale ambao hawapati kama wanakuwa na bahati mbaya.

Kama umewahi kukosa chochote kile unachokitaka sana, huku wengine ukiona wanakipata, unachopaswa kujua ni kwamba bahati haihusiki hapo kabisa. Bali kuna vitu wenzako wanavijua, na wewe huvijui, ndiyo maana wao wanapata wanachotaka na wewe unakosa.

Leo tunakwenda kujifunza maamuzi manne ambayo yatakuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. Ukifanya maamuzi haya manne, na ukayasimamia kweli, hakuna chochote kitakachoweza kukuzuia usipate unachotaka.

Kabla hatujaingia kwenye maamuzi haya nikukumbushe kwamba, tunaposema maamuzi tunamaanisha maamuzi kweli. Kwamba ukishaamua basi kila kitu kinapaswa kwenda kwa maamuzi hayo. Usiamue kwa ajili ya kujifurahisha, bali amua kwa sababu ndiyo kitu unakwenda kufanya kwenye maisha yako.

maamuzi

Karibu kwenye maamuzi manne muhimu ya kukuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Moja; amua ni nini hasa unataka (usibabaike).

Maamuzi ya kwanza muhimu kabisa kufanya ni kuamua nini hasa unataka kwenye maisha yako. Hapa unachagua kile hasa unachotaka kupata, au pale unapotaka kufika. Maamuzi haya ni muhimu sana kwa sababu mambo ni mengi, vitu vizuri na vya kuvutia ni vingi.

Kama hutafanya maamuzi hasa ya nini unataka, utajikuta unakimbizana na kila kitu kipya, kila kinachoonekana kwa nje ni kizuri. Utakimbizana na vitu vingi lakini mwisho wa siku hutakuwa umepiga hatua yoyote.

Amua nini hasa unachotaka na maisha yako, kisha peleka nguvu zako, muda wako, akili zako, ubunifu wako na kila ulichonacho kwenye kufikia kile unachotaka. Usiangalie pembeni na usishawishike na vingine vinavyoonekana ni vizuri. Unachokitaka wewe ndiyo muhimu na kama utaweka juhudi basi utakipata.

Kile unachochagua, kiwe ndiyo muhimu zaidi kwako na isiwe tu umechagua kwa sababu kila mtu anafanya. Ukitumia kigezo cha kila mtu kufanya au kutaka, hutafika mbali, maana watu hawatabiriki, haitachukua muda wataachana na hicho na kuanza kutafuta vitu vingine.

SOMA; Sheria Tatu Za Kimafanikio Ambazo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuzijua.

Mbili; fanya kila kinachohitajika kufanya (kuwa mbunifu).

Kuna kauli moja watu huwa wanatumia, ambayo ni kauli ya kushindwa. Kauli hiyo ni kwamba nitafanya kila kilicho ndani ya uwezo wangu, au hicho hakipo ndani ya uwezo wangu. Sikiliza rafiki, mafanikio hayaji kwa kufanya kilichopo ndani ya uwezo wako, au kufanya kile unachoweza, mafanikio yanatokana na KUFANYA KILA KINACHOHITAJIKA KUFANYA.

Maamuzi ya pili muhimu kufanya ni kuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanya. Utakapochagua nini hasa unataka kwenye maisha yako, utakutana na vikwazo vingi kwenye njia ya kupata kile unachotaka. Njia pekee ya kuvuka vikwazo hivyo na kupata unachotaka siyo kufanya unachoweza au kinachowezekana, bali kufanya kinachopaswa kufanya.

Swala siyo kuweza, kuwezekana au kuwa ndani ya uwezo wako. Dunia itakuletea kila aina ya kikwazo, unahitaji kuweza kukabiliana na kila kikwazo unachokutana nacho. Na hilo halijalishi inawezekana au haiwezekani, haijalishi kama ipo ndani ya uwezo wako au haipo. Unachohitaji ni kuchukua kila hatua unayopaswa kuchukua, ili kufika pale unapotaka kufika.

Tatu; fanya kwa kufuata maadili yako (usivunje misimamo yako).

Utakapoanza kufanya ili kupata unachotaka, watu watakuja kwako na njia rahisi na za mkato za kupata chochote unachotaka.  Watakuonesha jinsi ambavyo ilivyo rahisi kutumia njia hizo za mkato kupata unachotaka. Na kwa kuwa unakitaka sana, utajiambia kwani shida ipo wapi?

Kosa kubwa, shida ipo, tena ipo kubwa sana kama utaamua tu kufanya chochote ili upate unachotaka. Lazima uwe na misingi ya maadili ambayo inakuongoza. Lazima uchague tangu awali, vitu gani utafanya na vitu gani kamwe hutavifanya.

Kwa sababu haina maana kukazana kupata unachotaka, kwa kutumia njia zisizo sahihi, kwa kuwa chochote utakachopata kwa njia zisizo sahihi utakirudisha, hutakaa nacho kwa muda mrefu.

Kuwa na misingi ya maadili, kuwa na misimamo ambayo unaifuata na kuiishi, na kila unachokifanya, kiendane na misingi hiyo ya maadili. Hufanyi hivyo ili kuonekana, na wala hufanyi hivyo kwa sababu ndiyo dini inasema au jamii, bali unafanya kwa sababu zako binafsi.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kuyafanya Maisha Yako Kuwa Rahisi Bila Ya Kuyarahisisha.

Nne; fanya kama haya ndiyo maisha yako pekee (ishi kama kila siku ni ya mwisho).

Pamoja na kujua kile ambacho mtu unataka, pamoja na kujitoa kufanya kila kinachopaswa kufanyika, bado kuna kitu kimoja kinachowazuia wengi kupata wanachotaka. Kesho.

Ni mara ngapi umekaa na kupanga kitu, ukapata hamasa kubwa sana ya kuanza kufanya kitu hicho, ulipoanza ukakutana na changamoto kidogo, na ukajiambia utaendelea kufanya kesho?

Maamuzi ya nne unayopaswa kufanya ni haya rafiki yangu, HAKUNA KESHO, maisha uliyonayo ni haya ya leo, hivyo chochote linachopaswa kufanyika, inabidi kifanyike leo. Usikimbilie kusema utafanya kesho, hakuna mwenye uhakika na kesho. Na kwa kuwa kila mtu atakufa, kuna siku utasema kesho na hutaiona.

Sasa kama wote tunajua hatuwezi kukwepa kifo, kwa nini tunaendelea kujidanganya na kesho? Kama kipo kitu muhimu kabisa ulichopanga kufanya leo, kifanye leo. Si ndiyo kitu muhimu? Hata kama vingine vitasubiri na viendelee kusubiri, hicho si ndiyo muhimu zaidi?

Una maisha haya tu, yaishi kwa ukamilifu wake, una leo tu, itumie kwa ukamilifu wa hali ya juu. Kila dakika unayopoteza jua ni maisha yamepotea. Kuwa makini na jali muda wako, na chochote unachopanga kufanya, kifanye, usiwe mtu wa kuahirisha.

MIMI NI MSHINDI

Rafiki, hayo ndiyo maamuzi manne muhimu unayopaswa kufanya kwenye maisha yako, ili kuweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. Kwa kufanya maamuzi hayo, haimaanishi utapata kila kitu haraka, bado utakutana na kushindwa, bado vitu vingine vitakuchukua muda, lakini kama utasimamia maamuzi hayo bila ya kuyavunja, utakuwa na uhakika wa kupata chochote unachotaka, ni swala la muda pekee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog