Kuna watu ambao huwa wanapata utajiri mkubwa, halafu wanafanya makosa fulani kwenye maisha yao, kisha wanapoteza kila kitu walichokuwa nacho, na kurudi sifuri kabisa. Kinachotokea baada ya kupoteza kila kitu ndiyo kinatuambia kama mtu alikuwa tajiri wa kweli au alikutana na utajiri kwa bahati.

Tuanze na mfano, kuna mtu ambaye hajawahi kuwa na kipato kikubwa, kisha siku moja akashinda bahati nasibu, au akapata urithi kutoka kwa wazazi, au akapata mafao kutoka kwenye ajira yake. Ghafla anakuwa na fedha nyingi kwa haraka, ambazo hajawahi kuzishika kwenye maisha yake. Sasa anaanza kufanya maamuzi makubwa na fedha hizo, anajaribu biashara ambazo hazijui kwa kina ila ameambiwa tu zinalipa, anaweka fedha nyingi, anapata hasara, kisha utajiri unapotea.

Sasa, bahati nasibu huwa mtu anashinda mara moja tu, urithi unapata mara moja tu, na mafao ya kazi ni mara moja, na tena unapewa ukiwa umeshachoka. Hivyo chanzo cha mwanzo cha utajiri ambao mtu anakuwa ameupata kinakuwa hakipo tena. Hivyo anashindwa kurudi tena kwenye utajiri, anabaki kwenye umasikini aliokuwa nao yangu awali.

Watu wa aina hii, na yeyote anayepata utajiri, halafu ukapotea na akashindwa kuupata tena, siyo matajiri wa kweli, ni watu waliobahatisha utajiri na ukawaponyoka.

Matajiri wa kweli huwa hawafilisiki, na hata wanapopoteza kila walichonacho, haiwachukui muda wanakipata tena.

Tuchukue mfano wa mtu aliyeanzia chini kabisa, kaanza biashara yake kwa kujidunduliza, kakuza biashara yake kwa misingi imara, anajua kusimamia fedha yake, kubana matumizi, kuweka akiba na kuwekeza. Anajenga mtandao wake kwenye biashara hiyo na anajua watu muhimu wa kushirikiana nao. Anaijua biashara yake kwa kina, anajua kila kinachohusiana na biashara hiyo.

SOMA; Maajabu Ya RIBA MKUSANYIKO (COMPOUND INTEREST) Katika Kujijengea Utajiri.

Chochote kinachotokea kwa mtu huyo, na akapoteza kila alichokuwa nacho, haiwi shida kwake, kwa sababu msingi anao, anaweza kuanza tena. Na kwa kuwa ana mtandao mkubwa, anajuana na wengi na anajua vizuri biashara aliyokuwa anafanya, haimchukui muda anarudi kwenye utajiri wake.

Kinachoamua utajiri wa mtu siyo fedha alizonazo benki, wala mali anazomiliki, wala kipato anachoingiza. Kinachoamua utajiri wa mtu ni fikra alizonazo juu ya fedha, tabia alizojijengea juu ya fedha na misingi anayoiishi kwenye eneo la fedha na maeneo mengine ya maisha yake.

Unataka kuwa tajiri wa kweli? Jua misingi ya utajiri na iishi wakati wote. Hutakuwa na wasiwasi iwapo utapoteza utajiri ulionao, kwa sababu unajua misingi itakupatia kila unachotaka.

Kwa wale wasiojua, misingi yote ya utajiri inapatikana hapa; ELIMU YA MSINGI YA FEDHA.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog