Maisha ni mchezo, na ili ufanikiwe kwenye mchezo wowote ule, lazima kwanza uzijue sheria za mchezo, ujue yapi unapaswa kufanya, yapi hupaswi kufanya, na yapi unategemea kupata.

Moja ya sheria zisizosemwa za kila mchezo ni maumivu, kila mchezo una aina fulani ya maumivu. Ambapo mchezaji yeyote anayeshiriki mchezo huo, anajua atakutana na maumivu hayo.

Maisha Bora

Mchezaji wa mpira anapata maumivu ya misuli baada ya kumaliza mchezo, na hapo ni kama hatapata majeraha mengine kama ya kuumia au kuvunjika akiwa uwanjani.

Mchezaji wa ngumi anapigwa ngumi kali, ambazo zinamuumiza na atakaa na maumivu hayo kwa muda baada ya mchezo.

Hivyo pia kwenye mchezo wa maisha, maumivu ni lazima, kuna maumivu mengi ambayo utakutana nayo kwenye maisha yako ya kila siku.

SOMA; UKURASA WA 1158; Haki Yako Ya Kuteseka…

Kuna watu ambao watakuahidi vitu halafu hawatatimiza ahadi zao, kuna vitu utategemea na havitatokea, kuna watu unawaamini na watakuangusha, kuna watu utawategemea na watakuangusha. Kuna ambao watakuibia, wengine watakudhulumu, wengine watakukana. Na bado wale watakaokukatisha tamaa, watakaokusema vibaya na kukuzushia yasiyo ya kweli.

Unapokubali kushiriki mchezo huu wa maisha, kubali kupokea yote hayo, kwa sababu hutaweza kuyakwepa, na ukijaribu kuyakimbia, utakutana nayo kila unapokimbilia.

Unapokutana na maumivu, jifunze kupitia maumivu hayo, Kila maumivu yanakuja na darasa, na kila maumivu yanakuja na maana.

Maumivu ni sehemu ya maisha, tegemea maumivu, jifunze kupitia maumivu hayo na fanya maumivu yawe na maana kubwa kwako. Kwa sababu maumivu bila ya maana ni mateso.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog