Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio kwenye maisha huwa hayatokei kama ajali, huwa haitokei tu kwamba kwa mara moja unapata kila unachotaka. Mafanikio ni mchakato, na mafanikio kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku moja moja ambazo umeziishi vizuri.

Kama ilivyo kwenye kupanda mlima, hutaamka na kujikuta umefika kileleni, bali kila hatua unayopiga, inakusogeza karibu zaidi na kilele. Hivyo jinsi unavyoiishi siku moja ya maisha yako, kunasababisha ufanikiwe au usifanikiwe kwenye maisha yako.

Siku moja ni kitu kikubwa sana kwenye maisha yako, ukiweza kuisimamia siku yako vizuri, ukafanya yale ambayo ni muhimu kwako na usiahirishe chochote, kisha ukarudia hivyo kwenye siku zinazofuata, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.

Hivyo jukumu lako kubwa rafiki yangu ni kuhakikisha kila siku yako unaiishi kwa mafanikio. Lakini hilo siyo zoezi rahisi, kuna vitu vingi vinakazana kuitawala siku yako na kukupa hofu pia. Ndiyo maana leo nimekuandalia hisia tatu unazopaswa kuzitengeneza kila unapoianza siku ili iwe siku ya mafanikio makubwa kwako.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Karibu tujifunze hisia hizi tatu, na jinsi ambavyo unaweza kuzitengeneza kwenye maisha yako na kuweza kufanikiwa.

MOJA; HISIA YA KUSUDI.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, kuna kitu ambacho kinakusukuma kufanya. Inaweza kuwa sababu zako binafsi, au kwa sababu kuna mchango unataka kutoa kwa wengine. Ili uwe na siku bora, ili uweze kufanya makubwa, unahitaji kujenga hisia ya kusudi, kwa kila unachofanya, angalia ni kwa namna gani kinayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Angalia ni tatizo au changamoto ipi kubwa ambayo wengine wanapitia na wewe unaitatua.

Watu wabinafsi, wale ambao wanajiangalia wenyewe tu huwa hawapati msukumo hata wa kutoka kitandani, kwa sababu ni rahisi kujidanganya mwamba unaweza kusubiri kidogo. Lakini unapowakumbuka wale wanaokutegemea wewe ili maisha yao yawe bora, utapata hamasa ya kuamka na kwenda kuweka juhudi zaidi.

Hisia ya KUSUDI ni hisia inayokuchochea kuamka na kwenda kuweka juhudi kubwa, na kadiri unavyowasaidia wengi, ndivyo unavyojisaidia wewe mwenyewe pia kufanikiwa.

SOMA; Tofauti Ya Kusudi, Dhumuni Na Lengo La Biashara Na Jinsi Ya Kutumia Hayo Matatu Kukuza Biashara Yako.

MBILI; HISIA YA UDHIBITI.

Umeshawahi kuianza siku yako, halafu siku ikaenda mpaka ikaisha, ukajisikia umechoka sana lakini ukiangalia hakuna kitu kikubwa ambacho umekifanya? Hapo unaweza kuona kama siku imeenda haraka au hujui nini unafanya. Hali kama hiyo hutokea pale unapokosa udhibiti kwenye siku yako, siku inakuendesha wewe badala ya wewe kuiendesha siku. Badala ya kufanya yale uliyopanga kufanya, unafanya yale yanayojitokeza mbele yako. Unachoka sana, lakini hakuna kikubwa unakuwa umekamilisha.

Ili kutengeneza hisia ya UTHIBITI wa siku yako na maisha yako pia, kila unapoamka, panga mambo muhimu unayokwenda kufanya kwenye siku yako hiyo. Kuwa na malengo ya kila siku, weka vipaumbele na andika kabisa mambo hayo. Unapoianza siku yako, fanya yale ambayo umepanga kufanya kwanza kabla hujafanya mengine.

Usikimbilie kufanya yanayojitokeza, fanya yale muhimu kwanza, yale uliyopanga kufanya. Unapofanya yale muhimu, unakuwa unaiendesha siku yako badala ya siku kukuendesha wewe.

Ukianza siku bila ya kuipangilia, ukiwa huna ratiba ya utafanya nini wakati gani, dunia itakuweka bize sana lakini mwisho wa siku hakuna utakachokuwa umekifia. Anza siku yako kwa kuidhibiti, dhibiti kila muda wa siku yako na mafanikio yatakuwa yako.

TATU; HISIA YA MATUMAINI.

Mambo hayatakwenda kama ulivyopanga, na hata kama utafanya kila unachopaswa kufanya, bado matokeo hayatakuwa kama unavyotegemea yawe. Kuna vikwazo, kuna changamoto, kuna magumu. Ukienda kichwa kichwa na ukakutana na magumu hayo, utakata tamaa na kuona mambo hayawezekani.

Hivyo ni muhimu sana kila unapoamka, utengeneze hisia ya matumaini. Unatengeneza hisia hii kwa kuangalia ni ugumu gani unaoweza kukutana nao, kisha kujiandaa ni namna gani utavuka ugumu huo.

Hata kama huwezi kujua kwa hakika ni ugumu upi utakutana nao, jua kwamba mambo yatakuwa magumu, na yatakuwa magumu kweli kiasi cha kufikiria kukata tamaa, na hivyo jiandae kwa ugumu huo na usiwe na wasiwasi unapokutana nao.

Kwa kujua utakutana na magumu, na kuamini utaweza kuyavuka na kufikia malengo yako, ni hisia ya matumaini ambayo itakuwezesha kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Rafiki yangu, hizo ndiyo hisia tatu muhimu, ambazo kila ukiamka asubuhi unahitaji kujijengea, unahitaji kujikumbusha na unahitaji kufanyia kazi yale uliyopanga kila siku. Endesha siku yako na usikubali kuendeshwa na siku, fanya yale ambayo ni muhimu kwako na usikubali kufanya yale ambayo dunia inakuletea kila siku. Na muhimu zaidi, jua utakutana na magumu hivyo jiandae kuyavuka na kusonga mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji