Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio yoyote kwenye maisha siyo rahisi, hayajawahi kuwa rahisi na kamwe hayatakuja kuwa rahisi.

Unapoona watu wamepiga hatua, wamefika kule ambapo na wewe ungependa kufika siku moja, jua kuna gharama ambazo wamelipa.

Unapoona wazazi wamelelea watoto wao vizuri, jua kuna gharama wamelipa mpaka kufika pale.

Unapoona wana ndoa wenye furaha na ushirikiano hata baada ya miaka mingi ya ndoa, jua kuna gharama wamelipa kufika hapo.

Unapoona mtu amefanikiwa kwenye kuanzisha na kukuza biashara yake, jua kuna gharama kubwa amelipa.

Nikukumbushe tu kwamba, hakuna mafanikio kama hakuna gharama iliyolipwa. Kama hakuna machozi, jasho na damu ambavyo vimehusika, mafanikio hayawezi kupatikana.

Hivyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa ni ngumu, lakini ni njia inayowezekana.

Lisha Akili

Moja ya vitu vitakavyokuwezesha kwenye njia hii, ni kujua wapi hasa unapokwenda na kutokukubali chochote kikutoe kwenye njia hiyo.

Iko hivi rafiki, watu wengi huanza wakijua wanataka nini kwenye maisha yao, ni mpaka pale wanapokutana na changamoto ndipo changamoto hizo zinawameza kabisa, zinawavuruga na wanasahau kabisa kwamba walikuwa na ndoto kubwa za maisha yao.

Na kama unavyozijua akili zetu na mawazo yetu, kitu kikishakuwa mbali na mawazo yetu, ni vigumu sana kukileta karibu na hata kukifikia.

Hivyo jambo muhimu sana la kuzingatia ili kufanikiwa licha ya changamoto tunazokutana nazo ni kuhakikisha tunakumbuka ndoto zetu kubwa muda wote, yaani kwa kila wakati tunapofikiri, basi kipaumbele cha kwanza kinakuwa kwenye ndoto zako kubwa.

Kwa kuwa tunasahau haraka, na kwa kuwa maisha yana mambo mengi, tunahitaji kuwa na mfumo mzuri na rahisi wa kujikumbusha ndoto zetu hizi kubwa.

Njia rahisi kufanya hivyo ni kuandika ndoto zetu kubwa kila siku na zaidi ya mara moja kwa siku. Kila siku unapaswa kukaa chini na kuandika kwa mkono wako yale malengo makubwa sana ya maisha yako ambayo unayafanyia kazi. Unapoandika unajiwekea nadhiri na maisha yako kwamba lazima uyafikie.

Kuandika kunakufanya ukumbuke mara zote na pia kunayaweka malengo hayo kwenye akili yako na hutaweza kusahau, hasa pale unapoandika kila siku na zaidi ya mara moja kwa siku.

Lakini najua utakachokuwa unafikiria sasa hivi, utakuwa unafikiria sina huo muda wa kuandika malengo kila siku, niko bize, nina mambo mengi. Halafu tena kuandika zaidi ya mara moja! Hapana, hiyo siyo kwa ajili yangu.

Leo nimekuandalia nafasi tatu kwenye siku yako ambapo unaweza kuyaandika malengo yako makubwa kwenye maisha yako. Kila mtu ana nafasi hizi, na kama akiweza kuzitumia vizuri basi zitamsaidia sana kuweza kufikia malengo yake.

Nafasi ya kwanza; unapoamka asubuhi.

Kitu cha kwanza kabisa unachopaswa kufanya unapoamka asubuhi ni kuyaandika malengo makubwa ya maisha yako. kabla hujafanya chochote, kabla hujagusa simu, kabla hata hujafikiria siku inaendaje, chukua kijitabu chako na dakika 5 za kwanza andika malengo makubwa ya maisha yako. baada ya hapo unaweza kuandika vitu vingine na kupangilia siku yako.

Faida za kuandika malengo yako makubwa kitu cha kwanza asubuhi ni inakuwezesha kuianza siku ukiwa unakumbuka wapi unakwenda. Unaianza siku ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kufanya makubwa. Na pia unaianza siku ukiwa na vipaumbele sahihi kwa maisha yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Own The Day, Own Your Life (Imiliki Siku Uyamiliki Maisha Yako).

Nafasi ya pili; unapoimaliza siku na kuingia kulala.

Nafasi nyingine nzuri kwako kuyaandika malengo makubwa ya maisha yako ni mwisho wa siku yako, pale unapoelekea kulala. Kabla hujalala, tenga dakika tano za kuyaandika malengo yako makubwa ya maisha yako.

Kuandika malengo yako mwisho wa siku kunakupa nafasi ya kuitafakari siku uliyoimaliza, kuangalia umepigaje hatua kuelekea kwenye malengo hayo. Pia inakuandaa na siku inayofuata, akili inalala ikifikiria kuhusu malengo yale na kukuandalia njia bora ya kuyaona mazingira yako kwa namna ya kufikia malengo hayo makubwa.

Nafasi ya tatu; unaposhindwa au kukaribia kukata tamaa.

Kila siku kuna kitu kitakachotokea ambacho hukutegemea kama kingetokea, au hukuwa na maandalizi nacho. Kuna vitu utajaribu na vitashindikana. Kuna watu watakuambia maneno ya kukukatisha tamaa na utaanza kuona labda wapo sahihi.

Unapokuwa kwenye hali kama hizi, iwe ndogo au kubwa, toa kijitabu chako na yaandike tena malengo yako makubwa ya maisha yako. Wala usisubiri mpaka mwisho wa siku ndiyo ufanye hivyo, utafanya kwenye nafasi ya mwisho wa siku, ila wakati ule ambapo upo kwenye hali ya kushindwa na kukata tamaa, yaandike tena malengo yako makubwa.

Kuandika malengo yako makubwa pale unaposhindwa au kukata tamaa kunakupa nguvu mpya ya kupambana. Kunakuzuia usikate tamaa na uone kilichotokea ni kidogo sana ukilinganisha na yale makubwa unayopanga kufanya.

SOMA; Hisia Tatu (03) Unazopaswa Kuzitengeneza Kila Unapoianza Siku Yako Ili Iwe Siku Ya Mafanikio Makubwa.

Tumia kuandika malengo yako maji ya kusafisha akili yako, pale unaposikia kitu hasi na kuanza kuona kama mambo hayaendi kaa chini na andika malengo yako. Pale wengine wanapolalamika kwamba mambo ni magumu, kaa chini na andika malengo yake. Ukiona akili yako inahama kutoka kwenye kuwezekana na kuanza kufikiria labda haiwezekani, hapo hapo andika malengo yako makubwa. Na kama utayaandika mara kumi kwa siku hakuna ubaya, muhimu ni akili yako yote, nguvu zako zote na imani yako yote iwe kwenye kufikia malengo yako makubwa.

Rafiki yangu, hizo ndiyo nafasi tatu, na huenda zitakuwa zaidi ya tatu za kuandika malengo yako makubwa kila siku. Tumia nafasi hizi nzuri na hakikisha hakuna chochote kinachokuzuia wewe kufikia malengo makubwa uliyojiwekea.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha