Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 27 la mwaka huu 2018 linakwisha kama lilivyoanza.

Imani yangu ni kwamba japo juma hili linaisha, hatua ulizopiga na yale uliyojifunza yataendelea kuwa na manufaa kwenye maisha yako.

Maana kanuni pekee ya mafanikio unayopaswa kuiishi ni hii; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

Kila juma lazima ujifunze kitu ambacho hukuwa unajua huko nyuma. Na ukishajifunza lazima uchukue hatua kubwa sana kwenye kile ulichojifunza na kwa kufanya hivyo viwili, lazima utafanikiwa.

Utakutana na magumu na changamoto, lakini hivyo ni vitu vya kuwarudisha nyuma wale ambao hawajajipanga, ila kwa waliojipanga kama wewe, unapaswa kusonga mbele zaidi.

Pamoja na mengi uliyojifunza juma hili, hapa nakuongezea matano muhimu, ambayo utayachukua kama mjumuisho wa juma lako hili na pia kwenda kuanza kuyafanyia kazi mara moja ili uone matokeo yake kwenye maisha yako.

Karibu rafiki yangu kwenye tano za juma, ujifunze na kuondoka na mambo matano ya kwenda kufanyia kazi ili maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; UZA AU UTAUZWA

Kuna kazi moja ambayo kila binadamu anaifanya iwe anajua au hajui. Kazi hiyo ni mauzo, kila mtu kuna kitu anauza, iwe yupo kwenye biashara au ameajiriwa, iwe ni kiongozi wa siasa au wa dini, wote tunauza.

Tofauti ya watu wanaofanikiwa na wanaoshindwa inaanzia kwenye mauzo, wale wanaojua kazi yao ni kuuza na kujifunza kuuza vizuri chochote wanachouza ndiyo wanaofanikiwa sana. Wale wanaofikiri kwamba hawapo kwenye mauzo, hivyo hawawezi kuuza vizuri, wanaishia kushindwa.

Grant Cardon, mwandishi na mjasiriamali ambaye amekuwa anatoa mafunzo mengi sana kuhusu fedha na hata mauzo, ameandika vitabu kadhaa kwenye eneo la mauzo. Moja ya vitabu alivyoandika ni kitabu SELL OR BE SOLD, ambapo Grant anatushirikisha mambo muhimu ya kuzingatia ili kufanikiwa kwenye kuuza na hata kwenye maisha kwa ujumla. Kitabu kimebeba jina la mauzo, lakini mimi naweza kusema ni kitabu cha mafanikio kwenye maisha kwa ujumla, na kama nilivyokuambia, kila mtu anauza.

sell or be sold

Grant anasema kwenye maisha yako kila kitu ni mauzo, hivyo itakuwa labda ni wewe unamuuzia mtu kitu, au mtu anakuuzia wewe kitu, au hata unauzwa kabisa. Upande mzuri wa kuwa kwenye maisha yako ni upande wa kuuza.

Yapo mengi sana sana nimejifunza kwenye kitabu hichi kuhusu mauzo na maisha kwa ujumla, na ni moja ya vitabu ambavyo nashauri kila mmoja akisome.

Hapa nitakushirikisha mambo kumi muhimu ambayo wewe unapaswa kwenda kuyachukulia hatua mara moja kwenye maisha yako na shughuli zako ili uweze kuona mafanikio makubwa.

  1. Mauzo ndiyo njia ya maisha, mauzo ni hitaji muhimu la maisha, ili ule lazima uuze, na lazima pia watu wakuuzie kitu. Kama kuna kitu kimoja unapaswa kujifunza sana kwenye maisha yako, ni jinsi gani unaweza kuuza vizuri chochote unachouza. Kama umeajiriwa unauza muda wako na ujuzi wako pia. Kama upo kwenye biashara unauza bidhaa na huduma ulizonazo. Maisha yanaendeshwa kwa kamisheni ambazo tunazipata kwenye mauzo yetu, inategemea tu jina gani unaita, kwenye biashara utasema ni faida, kwenye kazi mshahara, kwenye mauzo ni kamisheni. Tambua, hakuna kitakachotokea kwenye maisha yako mpaka umuuzie mtu kitu. Amka sasa na anza kuuza kile unachouza kwa kuwa maisha yako yanategemea wewe kuuza.
  2. Uchumi unaendeshwa na watu wanaouza. Ukiangalia, uchumi mzima wa dunia, unaendeshwa kwa mauzo. Watu wanaouza vitu ndiyo wanasukuma mzunguko wa fedha na uchumi kwa ujumla. Usijidharau kama muuzaji, jua mchango wako ni mkubwa sana kwenye jamii yako, nchi na dunia kwa ujumla. Kwa maneno mengine, kama huuzi vizuri basi unaidhulumu dunia, maana unazuia mzunguko wa fedha usiende vizuri. Uza kwa kujiamini, ukijua unachangia kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.
  3. Je wewe ni mbobezi au mchanga? Kwenye kila tasnia kuna wale ambao ni wabobezi, ambao wanafanya na kutoa matokeo, halafu kuna wale wachanga, ambao hawafanyi na wanaishia kutoa sababu. Unapokuwa mbobezi kwenye mauzo unauza, haijalishi uchumi ni mzuri au mbaya, wewe ni muuzaji na unauza. Lakini wale wachanga watakuwa na kila sababu, mara oh uchumi siyo mzuri, hali ngumu, watu hawana fedha na kadhalika. Acha uchanga wa kutoa sababu, kuwa mbobezi kwenye chochote unachouza na uza, usisikilize wale wanaojidanganya kwamba hali ni ngumu. Hata hali iwe ngumu kiasi gani, watu hawataacha kununua. Na wauzaji wabobezi huwa wanauza zaidi hali inapoonekana ngumu kuliko hali ikiwa kawaida. Kwa sababu wakati hali ni ya kawaida, wauzaji wachanga wengi wanavamia soko, ila hali ikiwa ngumu wanakimbia, na hapo ndipo wabobezi wanapouza vizuri. Kuwa mbobezi na uza kwenye kila hali, kwa sababu mauzo yako ndiyo yanachochea uchumi uendelee.
  4. Kitu kimoja unachohitaji ili kuwa muuzaji mkuu ni kujitoa kweli kweli kwenye mauzo. Kuamua kwamba utauza maisha yako yote na kisha kuuza. Watu wengi huwa hawajitoi kwenye chochote wanachofanya, wanajaribu na kuacha vitu vingi, hivyo hawabobei popote. Wewe jitoe kwenye vile ambavyo umechagua kuuza na vijue nje ndani na uza maisha yako yote. usijaribu, uza.
  5. Mauzo muhimu kabisa kwako kufanya ili ufanikiwe ni kujiuzia wewe mwenyewe. Kama wewe huwezi kununua kile unachouza, basi jua hutaweza kumuuzia yeyote. Kama huwezi kutoa fedha kumnunulia mtu wako wa karibu kitu hicho, kama siyo kitu unaweza kutumia wewe basi jua hutaweza kuuza kitu hicho. Ili ufanikiwe kwenye chochote unachouza, unapaswa kukikubali sana, kukijua kwa undani na kuona mtu yeyote ambaye hatakinunua basi ana bahati mbaya kwenye maisha yake. Je hivi ndivyo ilivyo kwenye unachouza? Kama siyo, unapoteza muda wako.
  6. Watu hawanunui kwa sababu ya bei, wananunua kwa sababu ya thamani na mapenzi. Kwenye mauzo watu wamekuwa wanajidanganya kwamba sababu watu hawanunui ni kwa kuwa hawana fedha, au kitu ni bei ghali. Hivyo wengi hukimbilia kupunguza bei wakiamini ndiyo watauza zaidi. Kinachotokea, wanapunguza bei na bado watu hawanunui. Kinachowasukuma watu kununua siyo bei, bali thamani ambayo unawapa na mapenzi yao juu ya kitu hicho. Hivyo hapa tunarudi kwenye wewe kukijua kweli na kukipenda unachouza kiasi kwamba humwelezi mtu ambaye hajanunua bado. Pia mwoneshe mteja thamani anayoipata kwa kununua. Na pia lazima ujue wateja unaowalenga, kwa sababu kama mtu hana hata hela ya kula halafu unakazana kumuuzia kitu cha bei juu, hatanunua hata iweje. Tafuta wateja wenye kuweza kumudu na wauzie thamani na mapenzi ya kile unachouza.
  7. Hakuna uhaba wa fedha kwenye dunia, bali kuna uhaba wa watu wenye mawazo mazuri ya kutengeneza fedha zaidi. Wanaoshindwa kuuza wanakuwa wanasingizia uhaba wa fedha, kitu ambacho siyo kweli. Kadiri thamani inavyoongezeka duniani ndivyo fedha zinavyoongezeka pia. Usifikiri kwamba fulani akipata basi wewe unakosa, fedha ni nyingi sana. na kumbuka hizi fedha ni makaratasi na tarakimu kwenye kompyuta ambazo watu wanatengeneza, hivyo ukitoa thamani zaidi, unapewa makaratasi na tarakimu nyingi zaidi. Ondokana na uhaba, uza na utapata fedha kulingana na thamani unayotoa.
  8. Biashara yako ya kwanza ni watu kabla hata hujauza kile unachotaka kuuza. Unahitaji kuwashawishi kwanza watu wakubaliane na wewe, kabla hawajakubaliana na kile unachouza. Hivyo mbinu za mafanikio ni muhimu sana kwenye mauzo yako. Lazima uwe na ushawishi, uweze kuwaelezea watu kitu wakakuelewa na kuhamasika kuchukua hatua. Weka kuwajali watu mbele kabla hata ya bidhaa au huduma unayouza.
  9. Mara zote kubaliana na mteja, kisha mpe njia mbadala ambayo ni bora zaidi kwake. Kosa moja ambalo wengi wamekuwa wanafanya kwenye mauzo ni kupingana na wateja wao mwanzoni kabisa. Ukishapingana na mteja jua kabisa kwamba hatanunua tena, hata umshawishi kiasi gani. Kwa sababu ukishapingana naye, ataanza kukazana kupinga na kukuonesha kwa nini yeye yupo sahihi na wewe ndiyo unakosea. Si unajua hakuna anayependa kukubali amekosea? Mteja akikuambia bei yako ni kubwa, mwambie ni kweli ni kubwa, kisha mweleze sababu kwa nini ni kubwa, kwa kumwonesha thamani kubwa anayopata kuliko akinunua pengine kwa bei ya chini. Kwa namna hii una nafasi kubwa ya kumuuzia kuliko kumwambia siyo kweli kwamba bei ni kubwa.
  10. Tengeneza uaminifu kwa wateja wako kwa vitendo na siyo maneno. Kila mtu anaweza kusema, lakini wachache sana wanaoweza kufanya. Katika kumweleza mteja kuhusiana kile ambacho unamuuzia, mwoneshe kwa vitendo. Watu wakiona wanaamini zaidi kuliko kuambiwa pekee. Wasaidie wateja wakuamini, kwa sababu bila mteja kukuamini, ni vigumu sana kwake kuchukua hatua ya kununua.

Haya ndiyo mambo kumi muhimu unayoweza kufanyia kazi kwenye mauzo yako na ukaweza kupiga hatua sana. Angalia unawezaje kuyatumia kwenye kile unachouza na anza kuchukua hatua.

#2 MAKALA YA WIKI; SABABU 7 KWA NINI NAANDIKA KILA SIKU.

Nimekuwa naandika makala kila siku bila kuacha hata simu moja kwa siku 1285 sasa, kila siku. Hapo kuna kama siku nyingine zaidi ya 1000 ambazo nilikuwa naandika kabla ya hizi, lakini kipindi hicho sikuwa naandika kila siku.

Siku moja mtu aliniandikia tafadhali punguza kunitumia makala unazoandika, ni nyingi sana mpaka nashindwa kufanya kazi. Nikamwomba samahani kwa usumbufu mkubwa anaoupata kutokana na wingi wa makala zangu za kila siku.

Wengine ambao ni waandishi wamekuwa wananiuliza inakuwaje naandika kila siku, wengine wanauliza vya kuandika haviishi?

Kwenye makala ya wiki hii nimetoa sababu saba kwa nini naandika kila siku na kwa nini nitaendelea kuandika maisha yangu yote. siku yoyote nitakayoamka na nikawa napumua, kitu cha kwanza ninachofanya ni kuandika, na nitaendelea kufanya hivi.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki hii, yenye sababu hizo sana, unaweza kuisoma hapa; Sababu Saba (07) Kwa Nini Naandika Kila Siku Na Nitaendelea Kufanya Hivyo Kwa Maisha Yangu Yote. (https://amkamtanzania.com/2018/07/04/sababu-saba-07-kwa-nini-naandika-kila-siku-na-nitaendelea-kufanya-hivyo-kwa-maisha-yangu-yote/)

#3 TUONGEE PESA; UHURU WA KIFEDHA KWAKO UNA MAANA GANI?

Neno uhuru wa kifedha ni neno ambalo wapo watu wengi wanaolitumia, lakini wachache sana wanaelewa maana yake. Wengine wanatumia neno utajiri lakini hawaelewi maana yake. Siku moja nilikuwa naongea na mtu, akaniambia tayari amefikia uhuru wa kifedha, nikamwambia wewe bado sana. Akauliza kwa nini. Maana aliniambia ana nyumba tatu, ana kazi inayomlipa vizuri na pia ana biashara za magari. Kwa kifupi anaweza kupata fedha ya kununua chochote anachotaka kununua.

Nilimuuliza swali moja, sasa hivi ikatokea kazi unayofanya haipo tena, na biashara unayosimamia moja kwa moja imekufa kabisa, je maisha yako yanaweza kwenda bila shida? Je unaweza kuendelea hivi unavyoenda sasa, ukawa na uwezo wa kununua chochote unachotaka? Jibu alilotoa ni hapana.

Kuna aina mbili za kipato rafiki, kipato cha moja kwa moja ambacho unakipata pale unapohusika moja kwa moja kwenye shughuli hiyo inayozalisha kipato, iwe ni kazi au biashara unayoisimamia.

Kisha kuna kipato ambacho siyo cha moja kwa moja, hapa unaingiza kipato bila ya wewe kuwepo moja kwa moja kwenye shughuli inayozalisha kipato hicho. Mfano mzuri hapa ni uwekezaji.

Sasa unakuwa umefikia uhuru wa kifedha, unakuwa umefikia utajiri kweli, pale ambapo kipato chako ambacho siyo cha moja kwa moja kinakuwezesha kuendesha maisha yako kwa namna unavyotaka wewe, uweze kununua chochote unachotaka.

Kama hujafikia hatua hiyo, kama bado kipato cha kuendesha maisha yako ni kile unachozalisha moja kwa moja, haijalishi ni kikubwa kiasi gani, wewe bado unaishi karibu na kuishiwa, hujafikia uhuru wa kifedha au utajiri wa kweli bado. Weka nguvu zako kwenye kujenga kipato kisicho cha moja kwa moja na hichi kitakusaidia kuweka maisha yako huru.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; ONGEZEKO LA BEI KWENYE HUDUMA ZOTE ZA UKOCHA.

Ninapenda kukutaarifu kwamba, huduma zote za ukocha ninazotoa, zimeongezeka gharama na kuwa mara mbili ya ilivyokuwa awali. Mfano kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA ilikuwa elfu 50, sasa hivi ni laki moja. Gharama ya PERSONAL COACHING ilikuwa laki moja kwa mwezi, sasa hivi ni laki mbili. Gharama ya GAME CHANGERS ilikuwa laki mbili kwa wiki 5, sasa hivi ni laki 5. Gharama ya LEVEL UP ilikuwa milioni moja kwa wiki 10, sasa hivi ni milioni mbili.

Sababu pekee ya kuongeza gharama hizi ni nataka kuongeza thamani mara 10 ya ninayotoa sasa. Lakini bei itakuwa mara 2 tu. Nataka kutoa thamani kubwa sana, kwa wale ambao wamejitoa kweli kufanikiwa. Kwa sababu kama unavyojua, mafanikio ni magumu na mtu anapaswa kulipa gharama kubwa, siyo tu kwenye fedha, bali kwenye nguvu, muda na hata kutoa kafara.

Hivyo kwa ongezeko hili la bei, wale ambao bado hawajaamua kujitoa hasa kufanikiwa, watakaa pembeni kuwapisha wale walioitoa hasa, na nitapata muda mwingi wa kufanya kazi na waliojitoa badala ya kusumbuka na wengi ambao bado hawajaamua kufanikiwa kweli.

Karibu sana kwenye huduma za ukocha, ambapo utajifunza na kuchukua hatua na kwa hakika utafanikiwa. Kwa maelezo zaidi ya huduma hizi tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; SHINDA KWELI AU TESEKA KWELI.

“Far better it is to dare mighty things, to win glorious triumphs, even though

chequered by failure, than to take rank with those poor souls who neither

enjoy much nor suffer much, because they live in the grey twilight that

knows neither victory nor defeat.” – Theodore Roosevelt

kuna mstari kwenye biblia unasema ni heri kuwa moto au kuwa baridi, lakini usiwe vuguvugu, maana kuwa vuguvugu ni kubaya kuliko hata kuwa baridi.

Kwenye mafanikio pia, ni heri uweke juhudi zako, zote kabisa na ufanikiwe kwa uhakika au ushindwe kabisa, kuliko kutokuweka juhudi zako zote halafu ukawa mahali fulani katikati, hujafanikiwa na wala hujashindwa. Yaani unakuwa upo upo tu na hakuna maisha ya mateso kama hayo.

Hatua yoyote utakayochukua kwenye maisha yako, ina hatari ya kushindwa, hivyo wengi wanahofia kuchukua hatua na wanabaki katikati. Hivyo wanaishi maisha fulani ya matamanio muda wao wote, wasipate wanachotaka lakini pia wasikose kabisa.

Rafiki yangu, ninachotaka kukuambia ni hichi, chukua hatua kubwa sana kwenye maisha yako, fanya kila unachoweza kufanya na kama utafanikiwa basi ufanikiwe kweli, na hata kama utashindwa, basi ujue umeshindwa kweli, lakini ulifanya kila ulichoweza kufanya.

Hakuna kitu kitakuja kukuumiza, siku ukiwa umelala kwenye kitanda cha mauti yako, na kukumbuka ungeweza kufanya zaidi lakini hukufanya. Sasa hivi unaweza, fanya.

Rafiki, hizi ndiyo tano za juma namba 27, zisome na jifunze kisha chukua hatua kwenye maisha yako. Kama kuna kitu muhimu kwako, basi kifanye, na kifanye kweli, usiguse guse, fanya.

Nakutakia kila la kheri kwenye juma namba 28, likawe juma la kufanya makubwa sana kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha