Maisha ni mchezo, najua unajua hilo, ila kukumbushana ni muhimu.

Kila mchezo una sheria zake, ni muhimu kuzijua kabla hujaendelea na mchezo. Maana kuvunja sheria, hata kama  huzijui unapata adhabu kubwa.

Sasa kuna hili muhimu sana kuhusu mchezo huu wa maisha, ambalo ni upande upi wa mchezo ambao umechagua kucheza.

Kila mchezo una pande mbili. Upande wa kwanza ni kushinda na upande wa pili ni kuepuka kushindwa.

Muda tulionao

Upande wa kushinda ni pale mchezaji au timu inapocheza ili kupata ushindi. Hapa timu inashambulia na kujaribu mbinu mpya za kuweza kushinda.

Upande wa kuepuka kushindwa ni upande ambao timu inacheza kujiepusha na kushindwa. Hapa timu inazuia isishindwe, na hivyo haishambulii ili kushinda, bali inazuia mashambulizi ya upande wa pili yasiwe na madhara kwao.

SOMA; UKURASA WA 869; Kama Haiumizi, Haina Thamani…

Sasa ukiangalia pande hizo mbili, ipo wazi kwamba upande unaoshinda ni ule unaocheza ili kushinda. Na upande unaozuia kushindwa, huwa unashindwa, na hata usiposhindwa, basi haushindi.

Kwenye maisha pia ndivyo watu wanavyochagua kuendesha maisha yao. Kuna wale ambao wanaoendesha maisha yao kushinda, hawa ndiyo wanaojaribu mambo mapya hata kama ni hatari, wanakutana na changamoto na vikwazo lakini mwishowe wanashinda.

Lakini pia wapo wale ambao wanaendesha maisha yao kuepuka kushindwa, hawa ndiyo wanaokazana kufanya kile walichozoea kufanya, kile walichojiaminisha kwamba ndiyo chenye uhakika. Wanaweza wasishindwe kweli, lakini pia hawatapata mafanikio makubwa. Hivyo maisha yanakuwa ya mazoea na yanakuwa ya hovyo, hayana cha kusisimua.

Maisha ni yako, ni mchezo wako, wewe ndiye kocha wako wa kwanza na pia ndiye refa wako wa kwanza, chagua kukaa upande wa kucheza ili kushinda. Hutashinda mara zote, lakini kwa hakika utashinda, na ushindi kwenye maisha ndiyo kila kitu rafiki yangu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog