Rafiki yangu mpendwa,

Nachukua nafasi hii kukukumbusha jambo moja muhimu sana kuhusu chochote unachofanya kwenye maisha yako.

Kazi yoyote unayoifanya, iwe umeajiriwa, umejiajiri au hata kama unasaidia, thamini sana kile unachofanya.

Kama unaruhusu muda wako utumike kwa kuchagua kufanya chochote, basi kifanye kitu hicho kwa thamani ya hali ya juu sana.

Fanya kitu hicho kwa kujitoa kweli na fanya kwa kuweka alama, kwa namna ambayo hakuna mwingine anayeweza kufanya.

Chochote unachokubali kichukue muda wako, basi tenga muda wa kukifanya, na kifanye kwa viwango vya juu sana.

Usifanye ukiwa na haraka,

Usifanye ukikimbilia kumaliza,

Usifanye ili muda wa kufanya uishe,

Usifanye ili kuonekana unafanya.

Bali fanya kwa sababu unathamini kitu hicho, fanya kwa sababu ni kitu muhimu kufanya.

Na fanya kwa sababu unataka kufanya, umechagua kufanya na siyo kwa sababu inakubidi ufanye.

Sikiliza rafiki yangu, kama kuna kitu hutaki kufanya usifanye, wala usimwogope mtu yeyote, wewe usifanye.

Kuliko kufanya chochote kwa sababu hutaki kuwaumiza wengine, ni vyema ukawaumiza kwa ukweli, kwamba hufanyi, na wakapata ambaye atafanya kweli.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Nakukumbusha hili rafiki kwa sababu nawaona watu wengi wakipoteza muda wao na hata maisha yao, kwa kufanya vitu ambavyo hawataki kuvifanya, na hivyo kuvifanya hovyo kwa sababu hawavithamini.

Ambacho hawajui ni kwamba, chochote unachokifanya hovyo, unatuma ujumbe kwa dunia nzima kwamba wewe ni mtu wa hovyo.

Nimewahi kukutana na mtu mmoja ambaye hakuwa anaweka viwango kwenye kazi zake, alikuwa anaifanya kwa hovyo sana. Nilipomuuliza ni kwa nini, akanijibu wale waliomwajiri hawamjali, na hivyo hajali kazi yao. Na pia akaniambia hatakaa kwenye kazi hiyo kwa muda, anapita tu, hivyo kwenye mambo mengine atakuwa makini zaidi.

Nilichomwambia ni kimoja, na naomba nikisisitize sana kwako rafiki yangu; JINSI UNAVYOFANYA KITU CHOCHOTE, NDIVYO UNAVYOFANYA KILA KITU. Andika kauli hiyo na iweke mahali ambapo unaweza kuiona kila siku. Jinsi unavyofanya kitu chochote, hata kama ni kidogo kiasi gani, ndivyo unavyofanya kila kitu kwenye maisha yako. unaweza kukataa na kusema kuna maeneo uko makini, lakini kama kuna uzembe wowote kwenye maisha yako, ni dhahiri kwamba kuna uzembe kwenye kila eneo la maisha yako.

vitabu softcopy

Eneo la pili ninalotaka kukukumbusha wewe rafiki yangu kwenye kuthamini kazi yako, baada ya kuwa umeifanya kwa viwango vya juu sana, ni kuwafundisha watu kuithamini kazi yako.

Usiwaruhusu watu kudharau kazi yako, usiwaruhusu watu kuchukulia kawaida kazi yako. Kazi ambayo umeweka maisha yako yote pale, ambapo ndiyo damu ya maisha yako, usikubali watu wakaichezea kirahisi.

Na hapa naanza na kuwafundisha watu kukulipa kile ambacho unastahili kulipwa, kile unachopanga wewe kulipwa. Kwa sababu kwa vyovyote vile, hakuna anayeweza kukulipa kulingana na thamani yako, ila kwa kuwa unataka pia kuwasaidia watu, basi wanapaswa kukulipa kile unachotaka wao wakulipe.

Usikubali kuwa rahisi kwenye maisha yako, usikubali watu wakuchukulie wewe ni mtu wa rahisi, mtu unayekubali kulipwa chochote. Usikubali watu wakuchukulie kwamba wewe ni mtu unayeweza kukopwa nguvu zako, wakatumia nguvu zako watakavyo halafu wakakuambia wanakulipa baadaye.

Wafundishe watu thamani sahihi ya kile unachofanya, na wao wawe tayari kukulipa kile unachotaka wakulipe.

Na elewa kwa makini sana, unaanza kutengeneza thamani kubwa, kisha unawataka watu wakulipe kile unachotaka. Huanzi kutaka kulipwa zaidi wakati bado hujatengeneza thamani zaidi.

Na kama kwa muda mrefu hulipwi kile unachotaka, jua ni kwa sababu hutoi thamani kubwa. Anza kutoa thamani kubwa sasa, na anza kuwafundisha watu kuona thamani hiyo na utalipwa chochote unachotaka.

Neno la mwisho kwa wale walioajiriwa kwenye kazi ambazo hawazipendi au haziwalipi kama watakavyo. Unaposoma hapa fanya maamuzi kabisa, kama utaendelea kufanya kazi hiyo, basi utaifanya kwa viwango vya hali ya juu sana. Utaifanya kwa kujitoa mno hata kama unalipwa kidogo, na weka muda ambao utaifanya kazi hiyo. Kama hilo unaona huwezi, basi sasa hivi fanya maamuzi ya kuachana na kazi hiyo, wala hata usijiulize mara mbili, wewe acha tu na angalia wapi unaweza kuweka thamani kubwa na maisha yako.

Fanya maamuzi rafiki yangu, sitaki uondoke hapa ukiendelea na kufanya mambo nusu nusu, fanya kwa kujitoa moja kwa moja au usifanye kabisa. Usiwe katikati na ukichagua kuwa katikati basi usitupigie kelele kwa malalamiko kwamba kazi yako haikufai.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji