Rafiki yangu mpendwa,

Endelea kusoma hapa kama ulishawahi kukutana na hali za aina hii;

Moja; umepewa kazia mbayo unapaswa kumaliza ndani ya siku tano. Siku ya kwanza unaanza kuifanya, lakini hujisikii sana kufanya, unaona haupo tayari na hata hivyo siku bado zipo. Siku ya pili unagusa kidogo sana, lakini hufanyi. Siku ya tatu unagundua muda umeenda na hujaanza hata kufanya, unaweka mkakati mpya, mkakati wa kufa mtu na unauona ni mzuri, unajipa nafasi ya kutafakari zaidi mkakati huo. Siku ya nne, unaanza kupatwa na wasiwasi mkubwa, imebaki siku moja na hujaanza kufanya, unaanza kufanya kwa kasi ya ajabu, lakini hufiki mbali, unajiambia kesho ipo. Siku ya tano inafika, ndiyo siku ya mwisho ya kufanya na wewe hujapiga hatua kwenye ufanyaji, unasimamisha kila kitu na unafanya kitu hicho, na kabla siku haijaisha unakuwa umemaliza kukifanya, japo kwa kuchoka na mateso makubwa. Unamaliza ndani ya muda, kazi ya siku tano, unakuwa umeifanya kwa siku moja tu. Je hapo ni muda huna kweli?

Mbili; kuna kitu kila siku umesema utafanya ukipata muda, lakini hupati muda, kila siku kuna kitu kinachojitokeza cha kufanya, ambacho kinachukua muda wako na hivyo hufanyi. Unajiambia unapenda sana kufanya, lakini muda ndiyo hupati. Lakini kwenye siku hiyo hiyo ambayo unasema huna muda, unapata nafasi ya kuangalia, kusikiliza na hata kusoma habari, una nafasi ya kuweza kujua kila mtu anafanya nini. Unaweza kuperuzi mitandao mbalimbali ya kijamii na kujua kila kinachoendelea. Je kweli hapo ni muda huna?

Muda Unaotumia

Rafiki, endelea kusoma hapa kama hali hizo mbili nilizoeleza hapo juu zinaendana na wewe, yaani zimewahi kukutokea kwenye maisha yako. Maana nina ujumbe mkali sana kwako leo, ujumbe ambao unaweza kukufanya ujisikie vibaya, lakini sitajali sana maana ninachotaka ni wewe uweze kuchukua hatua na uache kutafuta sababu zisizo za msingi.

Mwanafalsafa Seneca kwenye kitabu chake cha On The Shortness Of Life anatuambia tatizo la muda siyo kwamba hatuna wa kutosha, bali tunao muda mwingi sana kiasi cha kuchagua kuupoteza muda huo. Kwa kuwa muda tunao mwingi, tunaona siyo vibaya tukautapanya kadiri tuwezavyo. Na hapo ndipo tunapokuja kulalamika baadaye kwamba tatizo ni muda.

Maneno haya ya Seneca, aliyaandika zaidi ya miaka 2000 iliyopita, lakini yana ukweli mkubwa kwenye zama tunazoishi sasa kuliko zama nyingine zozote zile.

Ukweli ni kwamba muda unao mwingi sana rafiki yangu, mwingi mno, lakini wewe mwenyewe unachagua kuupoteza, unachagua kuutumia vibaya na hapo ndipo unaingia kwenye mtego wa kuona muda hautoshi.

Muda ni mwingi sana ukishajua ni nini hasa unataka kufanya au kufikia kwenye maisha yako, kisha ukajiwekea vipaumbele vya mambo gani utaanza kuyafanya kwanza na yapi yatafuata baadaye. Lakini kama huna vipaumbele, kama ukiamka unafanya chochote kinachokuja mbele yako, siku zote hutakuwa na muda na hutaweza kufanya makubwa.

SOMA; Jifunze Na Wafundishe Wengine Kuthamini Kazi Yako (Na Maamuzi Muhimu Sana Ya Kufanya Kuhusu Kazi Yako Leo).

Katika kuuona muda mwingi ulionao na kuweza kuutumia vizuri, zingatia yafuatayo;

  1. Kuwa na vipaumbele unavyofanyia kazi.

Kamwe usiianze siku yako kabla hujapanga vitu gani muhimu unavyokwenda kufanya kwenye siku yako. Vitu hivyo visizidi vitatu na viwe ndiyo vitu muhimu kuliko vyote kabisa. Unapoanza kufanya kitu namba moja kwa umuhimu, usiende kwenye kitu namba mbili kabla namba moja hakijaisha.

  1. Kama hakuna anayekulipa usifanye.

Hatua muhimu ya kukuwezesha kuona wingi wa muda wako ni kuupa muda wako thamani ya fedha, tena kubwa sana. Halafu kwenye kila unachofanya, jiulize nani anakulipa kiasi kile cha fedha ulichoweka kwenye muda wako. Kama umechukua gazeti usome kwa nusu saa, jiulize nani atakulipa kwa hiyo nusu saa unayosoma gazeti? Kama umeingia kwenye mitandao kuperuzi ili ujue nini kinaendelea, jiulize je yupo atakayekulipa? Kama hakuna anayekulipa usifanye, hivyo tu.

  1. Kilicho muhimu kinafanywa kila siku.

Hakuna kitu muhimu ambacho kinafanywa mara moja tu. Nikumbushe mara ya mwisho kula chakula ilikuwa lini? Nafikiri unaona umuhimu wa kila siku kwa yale muhimu. Hivyo kama kuna kitu muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako, basi hakikisha unakifanya kila siku. Tenga muda kwenye kila siku yako kufanya yale muhimu. Kama unapenda kuandika, tenga muda wa kuandika kila siku. Kila siku tenga muda wa kujifunza na kupata maarifa zaidi. Na kazi yako, hakikisha unaifanya kila siku.

  1. Epuka kelele.

Tunaishi kwenye zama za kelele, zama ambazo kila mtu ni kama ana spika kubwa na anakazana kupata sauti zaidi. Kama unataka kuona wingi na thamani ya muda wako, epuka na kaa mbali na kelele. Na kelele hasa ni zipi? Chochote ambacho unafanya lakini hakuna anayekulipa ni kelele kwako, achana nacho.

  1. Usitake kujisifia kwa uzembe wako.

Kila ninapokutana na mtu na akaanza kuniambia angependa sana kufanya kitu fulani lakini hana muda, huwa namwambia wazi, au najiambia mwenyewe mzembe mwingine huyu hapa. Kama neno hili mzembe limekuumiza wala usinilaumu, pale juu nimekuambia kama muda siyo shida wako usisome, hivyo umesoma kwa sababu muda ni shida kwako  na unataka suluhisho na sehemu ya suluhisho hilo ni kukubali kwamba wewe ni mzembe na inabidi uache uzembe huo ili uweze kutumia vizuri muda wako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Power Of Motivation (Jinsi Unavyoweza Kufanikiwa Katika Mazingira Yoyote Yale)

Kwa nini nakuita mzembe? Hebu iangalie siku yako, ina masaa 24, hata kama utalala masaa nane, unabaki na masaa 16, sasa hebu niambie tu rafiki, masaa 16 kila siku huwa unayatumia kufanya nini? Unaweza kutupa saa kwa saa ya jinsi unavyoutimia muda huo mpaka unabaki huna muda kabisa wa kufanya yale muhimu? Maana kazi yako hata kama unaifanya masaa mengi kiasi gani, itakuchukua masaa 10 mpaka 12, hayo mengine zaidi ya manne unayatumia kufanya nini?

Rafiki yangu, muda unao mwingi sana, ni wewe kuchukua hatua ya kurudisha umiliki wa muda kwako na kuuondoa kwenye mambo yasiyo muhimu.

Na kama utahitaji kujifunza mbinu bora zaidi za kupata masaa mawili ya ziada kwenye kila siku yako, basi soma kitabu PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU. Kitabu hichi ni softcopy na kinatumwa kwa njia ya email. Kukipata tuma fedha tsh elfu 5 kwenye namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma ujumbe wenye email yako na jina la kitabu na utatumiwa kitabu mara moja.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Rafiki yangu, niendelee kukukumbusha kwamba muda unao mwingi, shika hatamu ya muda wako, jua unaelekea wapi na maisha yako na kama hakuna anayekulipa, usipoteze muda wako kufanya.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha