Kama mtu angefanyia kazi kile ambacho anakijua, angefikia mafanikio makubwa sana. Kikwazo kwenye mafanikio siyo mtu kutokujua kilicho sahihi kufanya, karibu kila mtu anajua, bali kukosa utayari au msukumo wa kufanya.

Nani asiyejua umuhimu wa kuweka akiba kwenye eneo la fedha? Je ni wangapi wanaoweka akiba? Nani asiyejua umuhimu wa muda na ulivyo adimu? Lakini angalia jinsi kila mtu anavyopoteza muda.

Ujuzi siyo tatizo sana, hasa kwa zama hizi ambapo maarifa yanapatikana kwa urahisi. Kikwazo ni kuchukua hatua. Na hasara ya zama hizi ni kwamba kadiri maarifa yanavyokuwa mengi, ndivyo msukumo wa kuchukua hatua unavyopungua.

Kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kujijengea nidhamu na udhibiti kwenye maeneo matatu muhimu ya maisha, fedha, muda na mipango unayojiwekea.

Najua tayari tuna maarifa mengi kwenye maeneo hayo, hivyo kwenye ushauri wa leo siendi kukuongezea maarifa hayo, bali naenda kukuambia kipi unapaswa kufanya. Hivyo utachagua uanze kufanya mara moja, au usifanye na iwe mwisho wa kulalamikia mambo hayo.

Kabla hatujaona hatua zipi za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Matumizi na udhibiti mbovu wa muda na fedha, kushindwa kujitoa kwenye malengo ninayojipangia (Poor Commitment) pamoja na kughairisha mambo kila wakati.” – Ramadhani R. S.

Hiyo ndiyo changamoto kubwa aliyonayo msomaji mwenzetu, ambayo inawagusa walio wengi, hata mimi mwenyewe katika nyakati fulani fulani, ila ninapogundua nimeingia kwenye changamoto hizo basi narudi mara moja kwenye mstari sahihi.

Karibu ujifunze hatua za kuchukua kwenye maeneo hayo matatu, uzichukue na uweze kuwa na maisha bora.

Kujijengea nidhamu na udhibiti wa muda.

Tambua muda ndiyo rasilimali yenye uhaba, ambayo ukishapoteza hairudi tena. Katika kujijengea nidhamu na udhibiti wa muda, fanya yafuatayo;

1. Chukua kalamu na karatasi, gawa karatasi yako katika pande mbili, A na B.

2. Upande A orodhesha mambo yote ambayo umefanya kwenye wiki moja iliyopita, kila ulichofanya kiorodheshe, uliingia mtandaoni, orodhesha, uliangalia mpira, weka, ulibishana na watu weka.

3. Upande B orodhesha malengo na mipango uliyonayo, kile unachotaka kufikia ndani ya mwaka mmoja, miaka 5, 10 na mpaka 20 ijayo.

4. Linganisha orodha A na B, piga mstari kile ulichofanya upande A ambacho kinakusaidia kufikia upande B.

5. Baada ya hapo, chukua yale ya upande A ambayo yana mchango kwenye upande B na hayo tu ndiyo utakayoanza kuyafanya kuanzia sasa. Yale mengine uliyokuwa unafanya na hayana mchango kwenye kufikia malengo na mipango yako, achana nayo mara moja.

Yaani jiambie tu kuanzia leo sifanyi tena haya, na acha mara moja. Vitu kama kufuatilia habari, kubishana, mitandao ya kijamii na mengine utapaswa kuachana nayo mara moja.

Manufaa ya zoezi hili ni wewe kupata muda mwingi zaidi wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako. Na hapo hutakuwa tena na tatizo la muda.

Kama unahitaji maarifa zaidi kwenye upande huu wa muda, soma kitabu PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU, kukipata tuma ujumbe kwenda namba 0717396253.

SOMA; Tatizo La Muda Siyo Kwamba Huna Wa Kutosha, Bali Unao Mwingi Mpaka Unaamua Kuupoteza.

Kujijengea nidhamu na udhibiti wa fedha.

Kila pesa inayopita kwenye mikono yako ni mbegu, ambayo ukiitumia vizuri itakuwa na manufaa kwako. Lakini wengi wamekuwa hawana nidhamu na udhibiti mzuri wa fedha zao. Hapa kuna hatua za kuchukua kwenye kujijengea nidhamu na udhibiti wa fedha zako.

1. Nenda kwenye benki unayotumia sasa na fungua akaunti maalumu ambayo unaweza kuweka fedha lakini kutoa siyo rahisi au kuna ukomo. Karibu kila benki ina akaunti ya aina hii.

2. Omba huduma ya fedha kuhamishwa kwenye akaunti yako ya sasa ambayo ndiyo inaingiza kipato chako kikuu, iwe ni mshahara au fedha unazoweka akiba. Kwamba kila mwezi kuna kiasi watakikata kwenye akaunti yako ya akiba kwenda kwenye akaunti yako maalumu.

3. Weka akiba kwenye akaunti hiyo maalumu kila mwezi, bila kuigusa kwa angalau mwaka mmoja. Jiwekee kiwango cha kipato chako ambacho kitaenda kwenye akaunti yako, unaweza kuanza na asilimia 10 au nyingine itakayokufaa wewe.

4. Hakikisha kipato chako kinakatwa kabla ya matumizi, kama unafanya shughuli zako binafsi basi unapolipwa, kabla hujaanza kutumia weka kwanza pembeni kiasi cha akiba na kiweke kwenye akaunti hiyo.

5. Pesa iliyo kwenye akaunti hiyo maalumu isahau kabisa, chukulia kama ulinunua kitu fulani na hivyo usiiweke kwenye mahesabu. Ni mpaka mwaka uishe ndiyo utarudi kwenye fedha hiyo na kuchagua ufanye nayo kitu gani cha kuzalisha zaidi.

Zoezi hili linakulazimisha kujiwekea akiba na baadaye kuiwekeza, kitu ambacho kitakuweka vizuri kwenye eneo la fedha.

Kupata maarifa zaidi kwenye eneo la fedha soma kitabu ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kukipata wasiliana na 0752 977 170.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuituliza Kila Fedha Inayopita Kwenye Mikono Yako Ili Uweze Kujijengea Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Kujijengea nidhamu na udhibiti wa mipango unayojiwekea.

Kupanga ni rahisi, ila kuchukua hatua kwenye kupanga ndipo wengi wanapokwama. Ni rahisi sana kupanga halafu wakati wa kufanya unapofika unaahirisha.

Hata haya uliyojifunza hapa, utafurahia kweli na kujiambia utayafanya, lakini inapofika wakati wa utekelezaji, unaona huwezi kuanza sasa, au unahitaji maandalizi zaidi na sababu nyingine lukuki.

Iko hivi rafiki, mazoea ni rahisi, kufanya kitu kipya kunaumiza, unakimbia kufanya kwa sababu hutaki maumivu.

Hakuna namna utaweza kufanya makubwa wewe peke yako, lazima utaishia kuahirisha na kujiambia haujawa tayari.

Hivyo ili kujijengea nidhamu na udhibiti kwenye kutekeleza mipango yako, unahitaji nguvu ya nje. Unahitaji mtu ambaye atakusimamia kwa karibu, ambayo hatakuachia kirahisi pale unapojipa sababu.

Unaweza kufanya hivyo kwa njia kuu tatu;

Njia ya kwanza ni kujiunga na kikundi cha watu wanaofanya kitu fulani, ukiwa ndani ya kikundi unasukumwa zaidi kufanya kwa sababu hutaki kuwaangusha wengine.

Njia ya pili ni kuwatumia watu wako wa karibu kukusukuma kufanya, hapo unaweza kumwambia mtu kwamba utafanya kitu fulani, na usipofanya basi utapaswa kumlipa kiasi fulani. Unapojua kwamba usipofanya utalipa gharama basi utapata msukumo wa kufanya.

Njia ya tatu ni kuwa na kocha ambaye anakusimamia kwa karibu. Kwa kuwa na kocha, mnaweka mipango na hatua za kuchukua, kisha kocha anakufuatilia kwa karibu kwenye utekelezaji na kuendelea kukupa mwongozo zaidi.

Tumia moja ya njia hizo au zote kwa pamoja kwenye yale unayopanga kufanya na utapata msukumo mkubwa wa kufanya kila unachopanga kufanya.

Kupata huduma ya ukocha katika kutekeleza mipango mikubwa uliyonayo, karibu ujiunge na huduma ya PERSONAL COACHING, tuma ujumbe kwa wasap namba 0717392635 wenye maneno PERSONAL COACHING na utapata utaratibu.

SOMA; Tofauti Ya Mwalimu, Kocha Na Menta Na Jinsi Ya Kuwapata Walio Sahihi Kwako.

Kujijengea nidhamu na udhibiti ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yako, huwezi kufanikiwa kama unayaendesha maisha yako kikawaida. Lazima ujue pia kwamba kujijengea nidhamu na udhibiti kutakuja na maumivu, utakosa baadhi ya uliyoyazoea, lakini utapata yaliyo bora kabisa.

Fanyia kazi haya uliyoifunza hapa na hutaweza kubaki pale ulipo sasa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania