Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari CHOCHEA MOTO UENDELEE KUWAKA…
Kuwasha moto ni hatua moja muhimu,
Kuufanya moto uendelee kuwaka milele, hi hatua nyingine muhimu zaidi.
Ni rahisi sana kuuwasha moto, lakini kuufanya moto uendelee kuwaka kila siku, bila ya kufifia, kunahitaji kazi.
Moto tu wa kawaida, ili uendelee kuwaka unahitaji vitu viwili, nishati na hewa ya oksijeni.
Tunapokuja kwenye moto wa maisha yako, kujiwasha moto ni rahisi,
Kupata hamasa ya mara moja ni rahisi,
Kujiambia nitakwenda kufanya makubwa siyo kazi kubwa.
Kupanga kwamba utaamka mapema kila siku na kufanya yako siyo kitu kigumu.
Ugumu unakuja pale unapohitaji kufanya hayo uliyojiambia utafanya, na kuyafanya kila siku ya maisha yako.
Kila siku kuamka na kufanya, bila ya kuahirisha, bila ya kujiambia nitafanya kesho.
Kuendelea kufanya pale ambapo unakutana na ugumu na changamoto pia ni kazi nyingine kubwa, kitu ambacho wengi hawawezi kufanya.
Hivyo rafiki yangu, asubuhi hii tafakari kwenye kila moto uliowasha, ni upi umeendelea kuchochea na upi ambao umezima kabisa wenyewe.
Kwenye kila makubwa uliyosema utafanya, ni mangapi unayafanya hasa?
Kama kuna makubwa ulijiambia utafanya, na sasa hivi hufanyi, hebu jiambie uache uzembe, hebu jiambie uache kutaka mambo yawe rahisi.
Washa moto na uchochee moto huo kila siku.
Kuchochea moto wa maisha yako unahitahi vitu viwili vikuu;
Kwanza unahitaji kuwa na KWA NINI, unahitaji kuwa ja msukumo unaokutoa kitandani kila siku. Hii ndiyo oksijeni ya maisha yako. Kama huna ndoto kubwa, ambayo umeiandika chini na kila siku unarudia kuiandika, hujui unachotaka na huna mpango wa kufanya makubwa kwenye haya maisha.
Pili unahitaji kuwa na nguvu binafsi, hapa ndipo afya yako inahitajika sana. Haijalishi una mipango mikubwa kiasi gani na unaiandika na kuiimba mara ngapi kwa siku, kama huna nguvu za kuamka na kuchukua hatua, utakuwa unajidanganya tu.
Afya yako ni kipaumbele muhimu kwako,
Ulaji wako, ulalaji wako na namna unavyouchukulia mwili wako ni muhimu sana kwako.
Uwe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuchochea zaidi moto uliouwasha kwenye maisha yako, na usikubali ufifie hata dakika moja.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha