Maisha ni magumu, lakini ni magumu zaidi ukiwa mpumbavu, hii ni kauli ambayo imebeba ujumbe mzito sana pale unapoielewa vizuri.
Wapo watu ambao wanateseka sana kwenye maisha, lakini ukiangalia sehemu kubwa ya mateso yao inatokana na wao kukimbia uhalisia wa maisha yao.

Watu wanatengeneza maumivu zaidi kwenye maisha yao, wakijaribu kuondokana na maumivu. Mfano mtu mwenye changamoto fulani kwenye maisha yake, anaamua kutumia kilevi ili changamoto hizo zisimsumbue, anajikuta anatengeneza matatizo zaidi kwenye maisha yake.
Ukishajiona unaanza kuukataa uhalisia wa maisha, jua unakimbilia kwenye maumivu zaidi. Kama huna fedha, na kila njia ya kupata fedha unayokutana nayo ni ngumu na yenye changamoto na kuhitaji subira, kisha ukajiambia hizo siyo njia sahihi, bali ipo njia rahisi, ya mkato na isiyohitaji kazi kubwa kupata fedha, jua unaelekea upande wa maumivu. Utakazana kufanya vitu ambavyo mwisho wa siku vitakuwa vimekupotezea muda na nguvu zako.
SOMA; UKURASA WA 1135; Ujasiri Ni Uvumilivu…
Kushindwa kwenye maisha, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya kutokukubaliana na uhalisia wa maisha, kutamani mambo yangekuwa tofauti na kushindwa kuwa tayari kuchukua hatua ngumu kukabiliana na uhalisia wa maisha.
Kwa upande wa pili, mafanikio kwenye maisha ni matokeo ya kukubaliana na uhalisia wa maisha haraka, na kisha kuchukua hatua sahihi kwenye uhalisia huo. Hujaribu kuukimbia au kukataa uhalisia huo, bali unaukubali na kisha unachukua hatua zinazotatua uhalisia huo.
Chochote unachotaka kukimbia au kukataa kwenye maisha yako unajisumbua, kwa sababu popote unapokimbilia, utaenda kukutana nacho, kwa sababu chochote unachojaribu kukimbia, kipo ndani yako. Kubaliana na uhalisia wa maisha ili mambo yako yaende vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog