“Freedom is not procured by a full enjoyment of what is desired, but by controlling the desire” – Epictetus
Siku mpya, siku nzuri na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UHURU NI KUDHIBITI TAMAA…
Watu wengi wanaotafuta uhuru kwenye maisha yao, huwa wanafikiri uhuru ni kufanya na kupata chochote ambacho mtu anataka kwa wakati ambao anataka yeye.
Wanapokazana kupata kila wanachotaka, wanagundua wamezidi kuwa watumwa wa vitu hivyo kuliko walivyofikiria kwamba watakuwa huru.
Uhuru haupatikani kwa kupata kila ambacho mtu anataka,
Bali uhuru unapatikana kwa kuweza kudhibiti matakwa na tamaa zako.
Pale unapohitaji vitu vichache zaidi kufanya maisha yako yaende, ndivyo unavyokuwa huru zaidi.
Na kwa wale wanaoondoka kwenye utumwa fulani, labda wa ajira, wakiamini wanaenda kuendesha maisha wanayotaka wenyewe, wengi huanguka kwa kushindwa kujisimamia na kujidhibiti wao wenyewe.
Dunia haitakupa kila unachotaka,
Na chochote unachotaka hakitakuja kirahisi,
Badala ya kusukumwa na matakwa na tamaa zisizoisha,
Jua yapi ni muhimu zaidi kwako, na weka juhudi kupata yale muhimu zaidi.
Yasiyokuwa muhimu, yale unayotaka kwa tamaa tu, kwamba na wewe uonekane unayo au kwa sababu kila mtu anayo, usikubali yakufanye kuwa mtumwa.
Kuwa huru zaidi kwa kudhibiti tamaa na matakwa yako. Maisha bora yanahitaji vitu vichache sana, ni anasa ndiyo zinawatesa wengi.
Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kudhibiti matakwa na tamaa zako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha