Rafiki yangu mpendwa,

Watu wanaokuzunguka ndiyo wanaochangia sana kila kitu kwenye maisha yako. Kama utafanikiwa wanaokuzunguka wanahusika kwenye mafanikio yako. Na pia kama utashindwa, basi wanaokuzunguka wanahusika kwa kiasi kikubwa.

Leo tunakwenda kushirikishana tabia tano muhimu sana unazopaswa kujua kuhusu watu kwenye safari yako ya mafanikio. Hizi ni tabia ambazo siyo nzuri sana, na kama hutazijua utaishia kuwa mtumwa wa watu na kushindwa kupiga hatua kwenye maisha yako.

Na kabla hatujaingia kuangalia tabia hizi kwa undani, nikukumbushe tu, iwe utafanikiwa au hutafanikiwa, wa kwanza kubeba jukumu na hata lawama ni wewe. Ndiyo tabia za wengine zinaweza kuwa kikwazo kwako kufanikiwa, lakini unapaswa kuzijua ili zisiwe kikwazo. Ndiyo maana makala kama hii ni muhimu sana kwako kuisoma leo na kujikumbusha tabia hizi mara kwa mara.

vitabu softcopy

Tabia Ya Kwanza; Watu Hawajiamini, Na Wanawachukia Wanaojiamini.

Watu wengi sana hawajiamini, naweza kusema sehemu kubwa sana ya watu, hata wale unaowaona wanajua sana na wanafanya makubwa, wengi hawajiamini. Na siyo tu kwamba hawajiamini, pia hawapendi wengine wajiamini. Hivyo wewe utakapojiamini, utakaposema unataka kufanya makubwa na una uhakika utafikia makubwa, wataanza kutafuta vitu vya kukufanya usijiamini.

Ndiyo maana ukiwaambia watu unataka mafanikio makubwa, unataka utajiri watakuja na sababu kwa nini huwezi au haiwezekani, watakuonesha ni kwa namna gani unachotaka ni kibaya, na kwamba kukubali maisha ya kawaida ni vizuri.

Watu wanaokukosoa, wanaokukatisha tamaa na wanaotafuta makosa kwenye chochote unachofanya ni watu ambao hawajiamini na hawataki wewe ujiamini. Utakutana na watu hawa kwenye maisha yako, na wengi watakuwa watu wa karibu kwako. Jua hili na usikubali kutokujiamini kwa mwingine kuwe kikwazo kwako.

Jua nini unataka kwenye maisha yako, jua unapaswa kufanya nini ili kupata unachotaka kisha jitoe kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili kupata unachotaka. Maoni ya wengine yasiwe kikwazo kwako kwa namna yoyote ile.

SOMA; Usikubali Mtu Yeyote Akushinde Kwenye Maeneo Haya Kumi(10) Muhimu Kwa Mafanikio Ya Maisha Yako.

Tabia Ya Pili; Watu Watakuja Kwako Wakiwa Wanataka Kitu Kutoka Kwako.

Kuna mtu ambaye hamjawahi kuwasiliana kwa miaka mingi, siku moja anakupigia simu, anakuambia nakusalimia tu, halafu kwenye simu hiyo hiyo anakuomba umfanyie kitu, au umsaidie kitu. Hii ni tabia ya watu ambayo unapaswa kuijua, kwamba watu watajaribu kukutumia, watu watakuja kwako wakiwa wanataka kitu kutoka kwako.

Watu watakupa kitu fulani wakijua baadaye watavuna zaidi kutoka kwako. Na wapo ambao hawatakuwa na aibu ya kukuambia jinsi walivyokupa vitu fulani au kukusaidia kwa namna fulani, na hivyo kukutaka wewe ufanye kile wanachotaka wao ufanye.

Jua hili rafiki, lijue mapema sana na litegemee kwa wengi, hasa watu wa karibu kwako. Utakapoanza kufanikiwa, utawavuta watu wengi kuja kwako, na kila anayekuja, ana kitu unataka ufanye kwa ajili yako. Ukifanikiwa utakuwa na wajomba wengi, utakuwa na mashangazi wengi na utakuwa na marafiki wengi.

Unapaswa kujua hili ili ujue kwamba ni kwa kiasi gani upo tayari kufanya. Unapaswa kujua kwamba watu wengi wanakuja kwa ajili ya kupata kitu kutoka kwako, na wengi watatumia mbinu za kuufanya wewe ujisikie vibaya kama hutafanya wanachotaka.

Rafiki, usikubali kuwa mtumwa wa yeyote, kama kuna kitu hutaki kufanya usifanye, hata kama mtu anakuambia kumbuka nilifanya hivi au vile kwa sababu yako. Kama alifanya kwa nia njema kweli, hapaswi hata kukukumbusha, lakini kama mtu anakukumbusha alifanya kitu kwa ajili yako, jua huyo anataka kukutumia, na usikubali kutumika kwa kitu usichotaka.

Tabia Ya Tatu; Watu Hawapendi Kukosolewa.

Watu huwa hawapendi kukosolewa, hakuna mtu anayekubali kirahisi kwamba hapo nilikosea au sikuwa sahihi. Kila mtu anapenda kuwa sahihi na kila mtu anapenda kutafuta sababu ya kuelezea kama hakuwa sahihi.

Hivyo jua watu watakosea na hawatakubali kwamba wamekosea, wakati mwingine watatafuta mtu wa kulaumu kwa makosa yao. Wakati mwingine watu watakulaumu wewe kwa makosa yao wenyewe.

Unahitaji kujua hili ili kuokoa muda wako, hasa pale unapotaka watu wakubali wamekosea. Ukiona mtu amekosea, na unajaribu kumsahihisha lakini hakubali, achana naye, wala usipoteze muda wako. Kwa sababu hatakubali kwamba amekosea, na hata ikiwa wazi, atakuwa na sababu kwa nini hakufanya inavyopaswa kufanywa.

Chukua hatua zilizo sahihi, kama kilichokosewa ni kitu muhimu sana, lakini usitegemee mtu akubali kirahisi kwamba amekosea.

SOMA; Tabia 7 Zitakazo Kufanya Uendelee Kuwa Maskini, Hata Kama Una Kipato Kikubwa.

Tabia Ya Nne; Watu Watakugeuka Kwenye Wakati Ambao Unawategemea Zaidi.

Watu watakuambia tupo pamoja na wewe, tupo nyuma yako, usihofu tunakuunga mkono, lakini utakapohitaji uwepo wao kweli, hutawaona, kabisa. Watu watakugeuka katika wakati ambao hukutegemea wafanye hivyo, watakugeuka katika wakati ambao uliwategemea wawe msaada kwako.

Elewa hili ili usiumizwe au kuangushwa pale unaowategemea wanapokupa mgongo. Pale wale waliokuambia watakuwa na wewe kwa shida na raha, wakafurahia raha na zinapokuja shida wakakuacha, usiumie. Jua ni tabia za watu, maisha ni magumu tayari, na hivyo wengi hawapo tayari kubeba mizigo ya wengine.

Kama una mzigo kwenye maisha yako, jiandae kuubeba mwenyewe, wanaweza kutokea watakaokusaidia kuubeba, lakini ukikosa kabisa wa kukusaidia wala usiumie, maana siyo wengi walio tayari kubeba mizigo yao na mizigo ya wengine.

Kwa kifupi jua watu watakusaliti, lakini wala hupaswi kuita usaliti, bali jua ndivyo watu walivyo.

Tabia Ya Tano; Huwezi Kumridhisha Kila Mtu.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, kutakuwa na makundi matatu ya watu. Wapo ambao watakubaliana na wewe, wapo ambao watapingana na wewe na wapo ambao hawatajali hata unafanya nini.

Kama kuna chochote unachofanya kwenye maisha yako, kwanza kifanye kwa sababu unataka kukifanya, na kwa sababu ni muhimu sana kwako, na kwa sababu upo tayari kukisimamia kwa maisha yako yote.

Usifanye chochote kwa sababu unataka kuwafurahisha watu, au unataka kila mtu akubaliane na wewe, utaishia kuumia na kusumbuana na wengi. Sehemu kubwa ya watu hawatakubaliana na wewe hata kama unafanya kitu kizuri kiasi gani.

Fanya kitu kwa sababu ni muhimu kwako kufanya, kwa sababu ndiyo kitu sahihi kufanya, kwa sababu upo tayari kufanya hata kama dunia nzima haifanyi. Katika kufanya huko kuna ambao watakubaliana na wewe, wapo watakaopingana na wewe, na wengi sana, hawajui hata kama unafanya unachofanya.

Hizi ndiyo tabia tano muhimu tunazopaswa kujua kuhusu watu, ili wasiwe kikwazo kwetu kufanikiwa. Ukiangalia tabia hizo tano, kama huzijui vizuri, na watu wakazitumia kwako, utaishia kuwa mtumwa kwao kwa chochote wanachotaka.

Usiishi maisha yako kwa kutaka kumfurahisha kila mtu, kumridhisha kila mtu au kupendwa na kila mtu, fanya kilicho sahihi, fanya unachotaka kufanya na jua kwa sehemu kubwa, utabaki kusimama mwenyewe pale mambo yatakapokuwa magumu, lakini mambo yanapokuwa mazuri utakuwa na ndugu na marafiki wa kila aina.

Kujua tabia za watu ni muhimu, kwa sababu hawa tutaenda nao maisha yetu yote, mpaka kufa. Jikumbushe tabia hizi kila siku na itakusaidia kutatua changamoto nyingi kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji