Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 24 la mwaka huu 2018 linatupa mkono, juma limekwisha, hatutakuwa nalo tena kwenye maisha yetu. Lakini kuna kitu kimoja tunachoweza kuchagua kubaki nacho, yale tuliyojifunza na hatua tulizopiga kwenye juma hili.

Ndiyo maana kila mwisho wa juma, nakushirikisha mambo matano muhimu, ambayo kwa kukaa chini a kuyatafakari, kisha kuangalia jinsi gani unaweza kuyatumia kwenye maisha yako, unapata nafasi ya kupiga hatua zaidi.

Juma hili namba 24 lilikuwa juma bora sana, na ninaamini lilikuwa juma bora pia kwako kama uliishi kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA. Chochote kigumu ulichokutana nacho kichukulie kama darasa, na popote ulipoanguka usibaki hapo, bali jifunze na kisha piga hatua.

MIMI NI MSHINDI

Ni wakati sasa wa kupata yale matano muhimu niliyokuandalia kwa juma hili, karibu ujifunze na kuchukua hatua ili maisha yako yawe bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SHERIA 22 ZA MASOKO AMBAZO KILA MTU ANAPASWA KUZIFAHAMU.

Juma hili nimepata nafasi ya kusoma vitabu vitatu, na kitabu kimoja muhimu sana napenda kukushirikisha ni kitabu kinachoelezea sheria 22 za masoko. Kitabu kinaitwa THE 22 IMMUTABLE LAWS OF MARKETING. Kitabu kimeandikwa na waandishi Al Ries na Jack Trout.

Waandishi wamekuja na sheria hizi kwa kuangalia mwenendo wa biashara nyingi, hasa makampuni makubwa, ambayo yamekuwa yanawekeza fedha nyingi sana kwenye matangazo, lakini bado yanashindwa kuwashawishi wateja kuhusiana na kile wanachouza.

Waandishi wanasema sheria hizi 22 hazibadiliki vizazi na vizazi, na kama utaamua kuzivunja, basi jua umechagua mwenyewe kuumia. Ni sheria rahisi sana, kama sheria za asili, lakini wengi wanafanya makosa kwenye biashara kwa kutokujua sheria hizi na kuzifuata.

Kwa sababu ya nafasi na muda, nitakushirikisha sheria 10 muhimu katika zile 22, ambazo wewe rafiki yangu usijaribu kabisa kuzivunja. Sheria hizi kumi ninazokushirikisha ninachagua katika zile 22, lakini nitazitaja kwa namba ya mtiririko wa waandishi walivyopanga kwenye kitabu chao.

Sheria ya 1; sheria ya uongozi.

Biashara inayofanikiwa siyo ile inayokuwa bora, bali ile inayokuwa ya kwanza kwenye akili za wateja. Hivyo unapaswa kuifanya biashara yako kuwa ya kwanza, kuwa kitu cha kwanza ambacho wateja wanafikiria wanapotaka huduma au bidhaa unayouza wewe.

Sheria ya 2; sheria ya kitengo/aina.

Kama siyo wa kwanza kwenye kitengo au aina ya biashara unayofanya, basi usipoteze muda wako kuhangaika na kitengo au aina ambayo wengine wameshakuwa wa kwanza. Badala yake tengeneza kitengo au aina mpya ya biashara na kuwa wa kwanza. Wateja wanakumbuka kitu cha kwanza kuliko kinachofuata.

Sheria ya 5; sheria ya lengo/mkazo.

Biashara yako inapaswa kujulikana kwa kitu kimoja au vitu vichache ambavyo inafanya kwa ufanisi mkubwa sana. kutaka kuonekana unafanya kila kitu kunafanya wateja washindwe kukuweka wewe wa kwanza. Chagua eneo moja au maeneo machache ambapo mteja wako ataweza kukutambua kwa neno moja.

Sheria ya 7; sheria ngazi.

Kwenye soko kuna ngazi ya bidhaa na huduma, kuna ambayo ni ya kwanza na ya pili na ya tatu na kuendelea. Wateja huwa wanajua namba moja na namba mbili, zaidi ya hapo huwa hawajui. Hivyo kama umeshindwa kuwa wa kwanza, basi angalau kuwa wa pili, zaidi ya hapo, usiingie kwenye aina au kitengo hicho cha biashara.

Sheria ya 12; sheria ya uenezi.

Wafanyabiashara wengi hufanya kosa moja, wanaanza biashara moja, inapata mafanikio, kisha wanatumia jina lile lile la biashara kuanzisha biashara ya aina nyingine. Wanakuwa wanafikiria kwa vile jina hilo limekuwa na mafanikio kwenye aina fulani ya biashara, basi linaweza kuwa na mafanikio kwenye eneo jingine. Kinachotokea ni biashara mpya inayoanzishwa haifanikiwi na inaua biashara ya mwanzo.

Kama unataka kueneza biashara yako kwenye vitengo vingine, anzana jina jingine, jina ambalo litakuwa la kwanza kwenye aina hiyo.

Sheria ya 13; sheria ya kutoa kafara.

Ili biashara yako ikue, unahitaji kutoa kafara baadhi ya vitu unavyofanya sasa. Biashara nyingi hufa kwa sababu zinakazana kufanya vitu vingi ambavyo havina faida kubwa.

Kuna vitu vitatu vya kutoa kafara kwenye biashara; kuacha aina fulani bidhaa au huduma, kuacha sehemu fulani ya soko na kuacha kubadilika badilika kila wakati.

Sheria ya 17; sheria ya kutokutabirika.

Hakuna mtu yeyote anayeweza kutabiri kwa uhakika kuhusu kesho. Kutengeneza mipango ya biashara kwa kutabiri kitakachotokea kesho ni kujidanganya. Badala yake ni bora kuangalia mwenendo wa biashara ulivyo kisha kuchukua hatua muhimu za kuifanya biashara yako kuwa bora zaidi. Na kumbuka, mara zote yale yasiyotegemewa huwa yanatokea, hivyo kuwa tayari.

Sheria ya 18; sheria ya mafanikio.

Mafanikio huwa yanaleta kiburi na kiburi huwa kinaleta kushindwa. Watu wanapofanikiwa huwa wanajiona wameshajua kila kitu, wanaacha kuweka juhudi walizoweka mwanzo na wanaanza kushindwa.

Haijalishi umefanikiwa kiasi gani, epuka sana kuwa na kiburi, epuka kujiona umeshajua kila siku, na kila wakati endelea kujifunza na kuchukua hatua kama vile ndiyo unaanza.

Sheria ya 19; sheria ya kushindwa.

Kushindwa ni kitu kinachopaswa kutarajiwa na kukubaliwa. Pale unapokutana na kushindwa, usikazane kuficha vitu au kujifanya kama vile hushindwi, wengi wanaanguka kwa kujaribu kufunika kushindwa kwao. Kubali kwamba kuna eneo umeshindwa na chukua hatua haraka, hasa ya kuachana na eneo hilo ili lisilete madhara makubwa kwenye biashara yako.

Sheria ya 20; sheria ya sifa.

Mara nyingi kinachoonekana nje ni kinyume kabisa na uhalisia. Pale ambapo biashara inaenda vizuri, makampuni huwa yanakuwa yametulia na kuendesha biashara. Lakini mambo yanapoanza kwenda vibaya, ndipo utasikia makampuni yakiwa yanapiga kelele, kutengeneza sifa zisizokuwepo na mwishowe yanaanguka.

Kama unahitaji kutengeneza sifa za uongo za biashara yako, jua kuna makosa makubwa unayofanya, na ni swala la muda tu kabla biashara yako haijaanguka. Ijenge biashara yako kwenye misingi sahihi, ambapo hutahitaji kutengeneza sifa za uongo ili kuwafikia wateja.

Rafiki, hizo ni sheria tano katika zile sheria 22 za masoko ambazo hupaswi kuzivunja kama unataka biashara yako ifanikiwe. Nitaendelea kukushirikisha sheria nyingine kadiri tunavyokwenda.

#2 MAKALA YA WIKI; TABIA TANO MUHIMU UNAZOPASWA KUJUA KUHUSU WATU.

Watu wanaotuzunguka wana mchango mkubwa sana wa pale tulipo sasa na hata tutakapokuwepo kesho. Tunapaswa kuwachagua watu wanaotuzunguka kwa umakini sana. Lakini pia hata tukiwa makini kiasi gani kuwachagua, bado zipo tabia za watu ambazo kama hatutazijua tutakuwa kwenye wakati mgumu mno.

Kuna vitu ambavyo watu wanaweza kufanya ukajiuliza kwa nini wamefanya na usipate jibu. Unaweza kufikiria wanafanya kwa makusudi, lakini ukweli ni kwamba hizo ni tabia za asili za watu, na watu hawajui kwamba kwa kufanya hivyo wanakukwaza.

Pia usipozijua vizuri tabia za watu, unaweza kuishia kuwa mtumwa wa wengine.

Kwenye makala ya wiki hii, nimekushirikisha tabia tano unazopaswa kuzijua kuhusu watu kwenye safari yako ya mafanikio. Zisome na jua hatua sahihi za kuchukua pale watu wanapoonesha tabia hizo kwako.

Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Tabia Tano Muhimu Unazopaswa Kujua Kuhusu Watu Kwenye Safari Yako Ya Mafanikio.  (https://amkamtanzania.com/2018/06/14/tabia-tano-muhimu-unazopaswa-kujua-kuhusu-watu-kwenye-safari-yako-ya-mafanikio/)

#3 TUONGEE PESA; UMUHIMU WA MIFEREJI MINGI YA KIPATO.

Kama kipato cha kuendesha maisha yako kinatoka eneo moja pekee, haijalishi ni kikubwa kiasi gani, nikuambie tu wazi wewe rafiki yangu kwamba umechagua kuwa mtumwa wa eneo hilo linalokupa kipato.

Kwa mfano umeajiriwa, kazi ambayo inakupa mshahara mkubwa sana, na kupitia mshahara huo umechukua mkopo ambao unaulipa kwa miaka kumi, na mkopo huo umetumia kujenga nyumba unayoishi. Hii ina maana kwamba kwa miaka kumi inayofuata, huna usemi kuhusu maisha yako.

Kwa sababu huna namna nyingine, umeshajiweka kwenye kifungo, ambacho kuondoka ni kugumu.

Na hata ukijiambia kwamba unahitajika sana na aliyekuajiri, bado ndani yako kuna hali fulani ya kutokuwa salama unaisikia. Kwa mfano linapotokea tatizo kazini na ukaambiwa upo kwenye uchunguzi, au ukapewa barua ya onyo, hutakaa sawa. Utaanza kupata wasiwasi maisha yanaendaje kama kazi hiyo itapotea ghafla. Ndani yako utajifunza kuwa na adabu zaidi, kukubali hata kama siyo sahihi, ili tu usipoteze kazi hiyo.

Rafiki yangu, nimekuwa nakusisitiza sana uwe na mifereji mingi ya kipato, siyo tu kwa sababu ya kipato, bali kupata ile amani ya moyo. Unakuwa na amani wakati wowote kwamba maamuzi ya mtu mmoja, hayawezi kuvuruga maisha yako. Na hata kama utapoteza kazi hiyo, wakati unasubiri kupata kazi nyingine, una miezi sita mpaka mwaka mmoja wa maisha kuendelea bila kutetereka, familia ikaishi, watoto wakaenda shule na watu wasijue kama kuna lolote limetokea kwako.

Huu ndiyo uhuru ninaotaka uwe nao rafiki, uhuru ambao ulizaliwa nao, lakini kikundi fulani cha watu kikakukalisha chini kwa miaka karibu 20 (darasani) kikikuambia maisha yako hayawezi kwenda bila ya kuwa na mtu anayekuwezesha yaende.

Ni wakati sasa wa kuvunja uongo wa kikundi hicho cha watu, na kudai uhuru wako. Kama upo kwenye ajira, hata kama unalipwa fedha nyingi mno ambazo hakuna mtu anaweza kuzipata, kazana kupata uhuru huo.

Hivyo basi, hakikisha huingii kwenye madeni yoyote yale kwa kutumia mshahara wako. Usikope kwa kutumia mshahara, utaambiwa unakopesheka, lakini usifanye hivyo. Pili weka akiba ya dharura, isipungue miezi sita ya gharama zako za maisha. Tatu, kuwa na njia za pembeni za kukuongezea kipato. Tengeneza mifereji ya ziada ya kipato, fanya chochote unachoweza kufanya, kuongeza thamani kwa wengine na wao wawe tayari kukulipa.

Na usiniambie kwamba huna muda, kwamba umebanwa, kama kazi yako inachukua zaidi ya masaa 10 ya siku yako, basi jipe mwaka mmoja au miwili ya kufanya kazi zako mchana na biashara zako usiku mpaka ununue uhuru wako. Uhuru wako ni muhimu kuliko kitu kingine chochote kwenye maisha yako, ulinde kwa nguvu zako zote.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KAMA BADO HUJAJIUNGA NA KISIMA,UNAKOSA MENGI.

Kadiri ninavyokazana kuweka juhudi kwenye kazi za uandishi ninazofanya, ndivyo marafiki wengi mnanitafuta mkitaka niwasaidie kwenye changamoto mbalimbali mnazokutana nazo kwenye maisha yetu. Cha kushangaza ni kwamba, mtu anataka kunieleza tatizo lake ndani ya dakika moja, halafu ndani ya dakika nimpe majibu ambayo yatatatua kila kitu kwenye maisha yako.

Sikiliza rafiki, umekuwa kwenye kazi au biashara kwa miaka 5 mpaka kumi na hujaweza kupiga hatua, halafu unataka mimi nikupe muujiza wa kupiga hatua ndani ya dakika moja! Kwa kweli sina muujiza huo. Lakini nina kitu kimoja, ambacho kwa uhakika wa asilimia 100 najua kitakusaidia, tena kitakusaidia sana.

Kitu hicho ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ukiwa ndani ya KISIMA, kila siku utajifunza vitu ambavyo vitakujenga upya kifikra, utajifunza jinsi ya kufanya maamuzi sahihi, utaianza kila siku ukiwa na hamasa kubwa na baada ya muda utaanza kuona mambo yako yanabadilika.

Nakuambia hivi nikiwa ninajiamini kabisa kwa sababu nawajua wengi ambao walikuwa na mambo magumu, nikawaalika wajiunge, na baada ya miezi michache wao wenyewe wakaniambia wanaona mambo yao yanabadilika, wanaona changamoto zilizokuwa zinawakatisha tamaa zinajitatua zenyewe.

Hivyo rafiki yangu, kama unapitia magumu yoyote kwenye maisha yako, kama hujafika pale unapotaka kufika, nakuambia karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717396253.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITAKACHOTOKEA MIAKA 20 IJAYO.

“Twenty years from now you will be more disappointed by the things that you

didn’t do than by the ones you did do. So throw off the bowlines. Sail away

from the safe harbour. Catch the trade winds in your sails. Explore. Dream.

Discover.” – Mark Twain

Miaka 20 ijayo utajutia zaidi vitu ambavyo hujafanya leo kuliko vitu ambavyo umevifanya. Hivyo acha sasa kuahirisha kufanya viti kwa sababu yoyote ile, acha kuogopa changamoto au kushindwa na jaribu vitu vingi uwezavyo. Ni bora ukashindwa ukiwa umejaribu, kuliko usifanye kabisa halafu ukajiambia umeshindwa.

Wakati maisha yako yanaelekea ukingoni, utakumbuka kila ndoto kubwa uliyowahi kufikiria kwenye maisha yako lakini hukuchukua hatua, na wakati huo utakuwa huwezi kuchukua hatua. Utaishia kuwasumbua watu na hadithi zako kwamba KAMA NINGE.

Usisubiri mpaka muda upite uanze kusema KAMA NINGE, anza kufanya leo. Usiogope changamoto, usiogope kushindwa na usisikilize wanaokukatisha tamaa. Kama kuna kitu unakitaka kweli kwenye maisha yako, anza kukifanya sasa. Na miaka 20 ijayo, utajishukuru sana kwa kufanya.

Rafiki, nakutakia kila la kheri kwenye juma namba 25 tunalokwenda kuanza, nenda kaziishi sheria za masoko, zijue tabia tano za watu na ongeza mfereji mmoja wa kipato kwenye juma unalokwenda kuanza. Na kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, labda ujiunge sasa hivi, hapo ulipo, au kesho mapema kabisa uchukue zoezi hilo. Ukizidi kesho, miaka 20 ijayo utajutia sana kukosa nafasi hii, na hutajisamehe kwa namna utakavyokuwa umeipunja nafsi yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji