“If you want to improve, be content to be thought foolish and stupid” – Epictetus

Siku mpya, siku bora na siku ya kipekee sana kwetu.
Hii ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUBALI KUONEKANA MJINGA NA MPUMBAVU…
Ili kujifunza zaidi,
Ili kupiga hatua zaidi,
Kubali kuonekana mjinga na mpumbavu.

Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anajua kila kitu.
Hakuna asiyetaka kuonekana hajui.
Na hata kama mtu hajui, anafanya aonekane anajua.
Hili linawafanya wengi wasijue na wasijifunze mambo mapya.

Kubali kwamba kuna vitu hujui, na chukua muda wako kujifunza.
Kubali kwamba kuna vitu wengine wanajua kuliko wewe na kuwa mnyenyekevu kuomba ufundishwe na kuelekezwa.

Usijali kwamba watu watakuchukuliaje wakiona hujui,
Iwe watakuchukulia mjinga na mpumbavu, wewe usijali, maana ukishajifunza ujinga na upumbavu waliouona awali hawatauona tena.

Kila siku hakikisha kuna kitu kipya umejifuna.
Kwenye kila unachofanya hakikisha kuna kitu kipya umejifunza.
Na kila unayekutana naye, usikubali kuachana naye ukiwa hujajifunza kitu ambacho ulikuwa hujui.

Kila mtu unayekutana naye, kuna kitu muhimu sana anajua lakini wewe hujui.
Sasa ukijijua mjuaji, hutajifunza chochote.
Lakini ukikubali kuonekana mjinga na mpumbavu, utajifunza mengi sana kwa kila mtu.

Uwe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, iwe siku ya kujifunza yale usiyoyajua, ambayo ni mengi sana.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha