Kwenye safari ya mafanikio, utakutana na kila aina ya ugumu, vikwazo na changamoto. Utapanga vizuri na kujua kila hatua ya kuchukua, lakini utakutana na ugumu, ambao utakufanya uone hakuna namna nyingine.

Kinachowatofautisha wale wanaofanikiwa na wale wanaoshindwa, siyo magumu wanayokutana nayo, bali wao wenyewe. Kwa kuwa kila mtu anakutana na ugumu, wachache wanavuka ugumu huo na kufanikiwa, huku wengi wakishindwa, hatuwezi kusema ugumu ndiyo umewazuia watu wasifanikiwe.

Maisha Hayajawahi

Bali tunaweza kusema, bila ya shaka kwamba ulaini wa watu wenyewe ndiyo unawazuia wasifanikiwe. Pale mtu unapokutana na ugumu, halafu wewe ukawa laini, ukawa huwezi kupambana na ugumu huo, ukawa haupo tayari kuumia, lazima utashindwa.

Dawa ya ugumu kwenye safari ya mafanikio ni wewe kuwa mgumu zaidi. Kutokubali kushindwa kirahisi, kutokubali kuzuiwa na chochote.

SOMA; UKURASA WA 1129; Ili Dawa Ifanye Kazi…

Ndiyo maana unapochagua kufanya na kupata kitu chochote, unahitaji kujiahidi hili muhimu, utapata unachotaka au utakufa ukikifanyia kazi. Ukishajiwekea ahadi hiyo, na ukaishi ahadi hiyo kila siku, hakuna ugumu utakaokutisha.

Unapokutana na ugumu wowote kwenye maisha yako, usikimbilie kuangalia ugumu na kuona kama utauvuka au la, bali jiangalie wewe mwenyewe na jiulize umejitoa kiasi gani kuweza kuvuka ugumu huo uliokutana nao.

Ni muhimu sana wewe mwenyewe kuwa mgumu, kwa sababu ukivuka ugumu mmoja, unajiandaa kukutana na ugumu mkubwa zaidi.

Siyo ugumu wa nje unaokuzuia kufanikiwa, bali ulaini uliopo ndani yako mwenyewe. Kazana kuwa mgumu, na hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog