“Talent is insignificant. I know a lot of talented ruins. Beyond talent lie all the usual words: discipline, love, luck, but, most of all, endurance.” — James Baldwin

Amka mwanamafanikio,
Amka siyo tu kutoka kitandani,
Bali Amka kutoka kwenye ndoto na nenda kaweke juhudi.
Amka kutoka kwenye kuahirisha mambo na anza kuchukua hatua sasa.
Amka kutoka kwenye uzembe na anza kuwa makini sasa.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA unaweza kufanya makubwa sana kwenye siku hii nzuri ya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari KIPAJI PEKEE HAKITOSHI…
Kuna watu ambao wana vipaji vikubwa sana, vipaji vya kipekee ambavyo wengine hawana.
Lakini cha kushangaza siyo watu ambao wanakuwa na mafanikio makubwa.
Na wapo watu ambao hawana vipaji vikubwa sana, lakini wana mafanikio makubwa.

Ukiangalia kwa nje unaweza kuona kama kipaji ndiyo kina kisirani, kwamba kipaji ndiyo kikwazo kwa wengi.
Na ukweli ni kwamba, wengi wanaojua wana vipaji vikubwa, huwa wanajisahau, huwa wanaona tayari wana kila wanachohitaji, huwa wanafanya kwa mazoea na hawajifunzi zaidi.
Hilo hupelekea kuahindwa kufanya makubwa.

Lakini wale ambao wanajijua hawana vipaji vikubwa, wanajua kabisa kwamba kitakachowatoa ni juhudi zao. Wanajua hawana kingine cha kitegemea bali nguvu zao, jitihada, kujifunza zaidi na kuchukua hatua zaidi.

Kipaji pekee hakitoshi, kazi inahusika sana, uvumilivu unahitajika mno, na pia bahati ina nafasi yake.
Chochoe ambacho mtu unacho, ambacho kinaweza kukuweka upande wa faida zaidi, kinaweza kuwa kikwazo kwao kama usipojua mengine muhimu yanayohitajika.
Kijue vizuri kipaji chako, lakini kuwa tayari kuweka kazi kubwa sana, kuwa tayari kujifunza na kuvumilia ili kupata chochote unachotaka.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha