Amka mwanamafanikio,
Amka leo uende ukafanye kile ulichosema utafanya leo.
Amka leo uende ukakamilishe kile ulichoanza lakini hukumaliza.
Amka leo uende ukaanze kufanya kile ambacho umekuwa unasema utafanya.
Amka sasa, na amka ukiwa na hamasa ya kwenda kufanyia kazi ndoto kubwa ya maisha yako.

Ni siku mpya, siku nzuri na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HUJAFANYA KITU…
Huwa tunapenda kuangalia yale tuliyofanya siku za nyuma na kujisifia nayo.
Leo ikiwa ngumu, huwa tunatamani jana ingejirudia, huwa tunasema afadhali ya jana.
Na pale tunapokuwa wazembe kupitiliza, tunabaki tukisema enzi hizo bwana…..

Rafiki, ukilinganisha na uwezo wako mkubwa wa kufanya makubwa, ulichofanya mpaka sasa ni kidogo sana.
Ili kuweka mambo sawa tunaweza kusema tu ni sawa na hujafanya kitu.
Haijalishi wanaokuzunguka wanaona umefanya makubwa kiasi gani,
Haijalishi ukijiangalia wewe halafu ukawaangalia wao unajiona mbali kiasi gani.
Ukitumia kipimo cha wengine, unaweza kujiona mshindi mkubwa sana.

Lakini ukitumia kipimo chako mwenyewe,
Ukiangalia yale ambayo umeshafanya, na yale ambayo ungeweza kufanya, tukiwa wakweli, hujafanya chochote.
Yaani umegusa gusa tu juu juu.
Kama ni mgodi basi umekitana na vumbi la dhahabu, hujaikuta dhahabu yenyewe.

Nakukumbusha hili siyo kukukatisha tamaa na ujione hufai au hujafanya chochote,
Bali nakukumbusha hili ili uqche kujibwetesha, ili uache kulala kizembe, ukijiambia hata hivyo haupo pabaya sana.
Upo pabaya, na kila siku mpya unayoianza unazidi kujiweka pabaya.
Na ukiweka mazoea, na ukijisifu kwamba sikunza nyuma ulifanya makubwa sana, unazidi kujiweka pabaya leo.

Nikutakie siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kwenda kufanya makubwa na kuacha kujidanganya kwa lolote ulilofanya huko nyuma.
#OneLife, #AllIn, #JustDoIt, #DayOne, #SkinInTheGame,

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha