Unapokuwa na shaka na maisha yako, simama mbele ya kioo na utamwona mtu ambaye anapaswa kuyasimamia maisha yako.
Unapokuwa na malalamiko au lawama, simama mbele ya kioo na utamwona mtu anayepaswa kubeba lawama na malalamiko hayo.
Unapokuwa hujui nani atakusaidia kutoka hapo ulipo sasa, simama mbele ya kioo na utamwona anayepaswa kukuondoa hapo ulipo sasa.
Unapoona wengine wamepiga hatua kubwa ila wewe umekwama, simama mbele ya kioo na utamwona mtu sahihi wa kushindana na kujilinganisha naye.

Mbele ya kioo ndipo ukweli wa maisha yako ulipo, mbele ya kioo itajiona na wewe, na utapata nafasi nzuri ya kujua kwamba maisha yako ni wewe na yataenda kwa namna utakavyoyaendesha wewe.
Unaposimama mbele ya kioo, unahitaji kukubaliana na kile unachoona mbele yako. unaponyoosha kidole kwa unachoona mbele ya kioo, utaona kidole kinarudi kwako. Huo ndiyo uhalisia wa maisha.
SOMA; UKURASA WA 866; Kinachokuzuia Kuona Mbele… … ni kuangalia nyuma.
Ukinuna mbele ya kioo taswira inayorudi kwako ni ya kununa.
Unapocheka mbele ya kioo taswira inayorudi kwako ni ya kucheka.
Kioo ni mfano halisi wa maisha yako na jinsi dunia inavyokupeleka.
Unapokuwa kwenye changamoto, unapoona kama mambo hayaendi, simama mbele ya kioo, halafu ona kile kinachokuangalia. Jaribu kutabasamu na kucheka na utaona taswira inayokuangalia nayo ikitabasamu na kucheka.
Kioo ndivyo dunia yetu ilivyo, tunapata kile tunachotoa, na mbele ya kioo tunamwona mchawi wetu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog