Siku mpya, siku bora na siku ya kipekee,
Ni nafasi nzuri kwetu wanamafanikio kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA.
Kwa kutumia msingi huu tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UTAFANYA AU UTATOA SABABU…
Kama kuna kitu ambacho unakitaka kweli, kitu ambacho ni muhimu sana kwenye maisha yako, utafanya kila unachopaswa kufanya ili ukipate.
Kama ni kitu ambacho kinahusu kufa na kupona, yaani usipofanya au kupata utakufa, utapata msukumo wa kufanya hata kama ni kigumu kiasi gani.

Lakini kama ni kitu ambacho hukitaki sana, kitu ambacho hata usipofanya maisha yanaendelea, utakuwa na sababu kwa nini huwezi kufanya au kwa nini utafanya baadaye.
Hata kama ni kitu muhimu, lakini siyo hatari na hakina haraka, utapata kila aina ya sababu kwa nini usifanye sasa.

Hivyo mwanamafanikio, angalia vizuri kila unachofanya kwenye maisha yako, na ona kwenye yale unayokwepa kufanya, yale unayoahirisha, yale unayojipa sababu za kutokufanua, je ndiyo mambo muhimu zaidi kwako?

Njia pekee ya kujipa hamasa ya kufanya, ya kuhakikisha unafanya na hujipi sababu ni kujiweka kwenye nafasi ambayo lazima ufanye.
Nafasi ambayo usipofanya basi maisha yako yanakuwa kwenye hatari kubwa.

Usiruhusu sababu yoyote iwe mbadala wa kufanya, kuwa mtu wa kufanya. Unapopanga kufanya kitu, basi anza kukifanya. Unapotaka kitu basi kitake kweli na weka juhudi kukipata, usikubali kujipa sababu yoyoe ya kuacha kufanya ili kupata unachotaka.

Uwe na siki bora sana ya leo rafiki, siku ya kufanya kweli na siyo kutoa sababu.
#JiwasheMoto, #IngiaMzimaMzima, #Fanya, #HakunaSababu

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha