Muda una ukomo na nguvu zetu zinakwisha haraka pale tunapozitumia.

Hivi ni vitu viwili ambavyo vinatuzuia kufanya kila tunachotaka kufanya.

Kwa sababu muda ukishapita na nguvu zikishaisha, hatuwezi kufanya tena, hata kama tunataka kiasi gani.

Hivyo kama tunataka kupangilia vizuri maisha yetu, kama tunataka kupiga hatua, basi tunahitaji kutumia vizuri vitu hivyo viwili.

Muda Unaotumia

Na swali muhimu kujiuliza katika kupangilia vitu hivyo ni je itasaidia?

Kabla hujafanya kitu chochote kile na muda au nguvu zako, chukua dakika moja na jiulize je utasaidia?

Kabla hujakasirika kwa chochote kilichotokea, jiulize je kukasirika kwako kutasaidia kitu hicho kuwa sawa? Au kutakupotezea muda na nguvu zako?

Kabla hujaanza kulalamika na kuwalaumu wengine, jiulize je itasaidia, je itafanya kilichotokea kibadilike au kisitokee tena? Au unatumia muda na nguvu, ambazo kama ungeziweka kwenye kuchukua hatua, ungepata matokeo tofauti?

SOMA; UKURASA WA 662; Msingi Huu Wa Fedha Haujabadilika Na Hautakuja Kubadilika…

Kabla hujawa na chuki na mtu, kabla hujawa na wivu, jiulize je itasaidia?

Je itasaidia ni swali unapaswa kujiuliza kwenye hatua unazochukua pia. Kila siku unapaswa kujikumbusha kwa kuandika malengo yako makubwa. Na kila unachofanya kwenye siku yako, jiulize je itasaidia?

Mfano unapotaka kufungua facebook, au unaponunua gazeti usome, kabla hujaendelea jiulize je hilo litasaidia wewe kufikia malengo yako makubwa?

Usikubali kufanya chochote kabla hujajiuliza swali hilo, na halitachukua muda wako mwingi, lakini litaokoa sana muda na nguvu zako zisipotee hovyo.

Kama kitu hakisaidii, usifanye, hata kama kila mtu anafanya. Kumbuka malengo yako makubwa, kumbuka wapi unakwenda na kila unachofanya, kipime kwa kule unakokwenda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog