Hasira ni nusu ya ukichaa, unapokuwa na hasira kali, unakuwa huna tofauti na mgonjwa wa akili.
Hii ni kwa sababu hasira ni hisia kali, na wakati wowote akili yako inapotawaliwa na hisia kali, unaacha kufikiri kwa kina.
Hakuna hasira nzuri, hata kama mtu amekufanyia nini.
Hii ni kwa sababu hasira inachukua nguvu kubwa za mwili wako, kufanya jambo ambalo halina msingi wowote.
Unapokuwa na hasira, unatumia nguvu zako kufanya mambo yanayohusu watu wengine na siyo kuhusu wewe mwenyewe.

Utasumbuka na vitu ambavyo havikufanyi wewe kuwa bora, havikuwezeshi kupiga hatua na hapo ndipo unapozidi kuumia.
Usiwe na hasira juu yako mwenyewe, kama kuna makosa umefanya yajue, jifunze na kisha chukua hatua kuwa bora zaidi.
Kama kuna wengine wamekukosea, elewa kwamba wamekukosea na wasamehe kisha songa mbele.
SOMA; UKURASA WA 1010; Hasira Za Kurushiwa…
Usijenge hasira na yeyote, wengine wanakufanyia makosa kwa makusudi ili wakukasirishe na kukuondoa kwenye lengo lako. Wengine wanakukasirisha ili uingie kwenye mitego yao na wapate wanachotaka. Na wapo wanaokukasirisha kwa ujinga wao tu, hawajui hata kama wamekukasirisha.
Usikubali kutawaliwa na hasira, pale hasira inapokuja usiizuie, bali ikubali, jifunze kuhusu hasira hiyo na chukua hatua ili kuwa bora zaidi.
Kama unajua unakokwenda, na kama unataka kufanya makubwa na maisha yako, basi huwezi kupata muda wa kuwa na hasira juu yako au juu ya wengine, maana unahitaji kutumia nguvu zako vizuri kuweza kufanya yale ambayo ni makubwa.
Hakuna hasira nzuri, nguvu zako ni muhimu na zina ukomo, ziweke sehemu sahihi na siyo kwenye hasira.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog