Siku mpya, siku bora na siku ya kipekee sana kwako mwanamafanikio.
Siku hii haitakuja kujirudia tena kwenye maisha yako.
Siku hii ni zawadi kubwa kwako, ambapo unaweza kufanya makubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SABABU HAINA NAFASI…
Unapokuwa mtu wa kufanikiwa,
Unapokuwa mtu wa kufanya makubwa,
Basi huwezi pia kuwa mtu wa kutoa sababu.
Huwezi kuwa mtu wa kuanza kueleza kwa nini hujafanya au kwa nini umeshindwa.

Kama utafanya matokeo yataonekana na hivyo huna haja ya kutoa sababu au kueleza, kila mtu anaona mafanikio.
Kama hutafanya au utashindwa huna haja ya kutoa sababu wala maelezo, kwa sababu kwanza inaonekana hujafanya na pili, huo muda unaotumia kutoa sababu unapaswa kuwa unautumia kwenye kufanya.

Hii ina maana kwamba, ukishajiona unatoa sababu yoyote ile, ukishajiona inabidi ujieleze, jua tayari wewe umeshakuwa mpotezaji, umeshakuwa ‘loser’ na nafasi ya wewe kufanya makubwa ni ndogo sana.

Mwanamafanikio, fanya kile ambacho umepanga kufanya, fanya kile ambacho umeahidi kufanya na matokeo yatajionesha yenyewe.
Na kama hutafanya, basi hupaswi hata kupoteza muda wa wengine kuanza kuwaambia kwa nini hujafanya.
Kila mtu anaweza kusema kwa nini hajafanya, tunawataka wachache ambao ni wafanyaji na matokeo yanaonekana.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafii, siku ya kufanya, na usipofanya basi usijisumbue kutoa sababu, badala yake tumia muda huo kufanya.

#Fanya, #UsitoeSababu #WachaManenoWekaKazi, #HatuaYaZiada #IngiaMzimaMzima, #NiLeoTu

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha