Moja ya uhuru mkubwa ambao tunapenda sisi wanadamu ni uhuru wa kuchagua. Tunapenda kuona kwamba tumechagua sisi wenyewe kipi cha kufanya.
Hivyo tunapokuwa kwenye nafasi ambayo inabidi tufanye kitu kimoja, tunaona kama tumelazimishwa kufanya. Lakini vitu vikishakuwa viwili na kuendelea, hapo tunaona tuna uhuru wa kuchagua kipi tunachotaka kufanya.
Ndiyo maana hata kwenye chaguzi mbalimbali, mtu akiwa mmoja, hata kama anapendwa kiasi gani, uchaguzi utaonekana siyo huru. Lakini kukiwa na mgombea mwingine, hata kama inajulikana wazi kwamba atashindwa, watu wanaona uchaguzi huo ni huru.

Tumia hili kwenye maisha yako binafsi na mafanikio yako.
Kwenye kile ambacho unafanya au unataka kufanya, jiulize nini mbadala wake? Kama ingekuwa hutaki kufanya hilo, je kipi mbadala ambacho ungefanya?
Kama kuna kitu hutaki kufanya, jiulize upi mbadala wa kitu hicho? Na hapo sasa utaanza kupima kitu hicho na mbadala wake na kuweza kuchukua hatua sahihi. Badala ya kubaki na kitu kimoja na kukifanya kwa shingo upande, huku ukiwa hutaki kufanya, ni vyema kujua mbadala ni upi na kupima mbadala huo na hicho unachofikiria kufanya.
Iwapo mbadala ni bora zaidi ya unachotaka kufanya basi fanya mbadala, na kama siyo bora basi fanya kile unachotaka kufanya.
SOMA; UKURASA WA 997; Kazi Zetu Ni Watu…
Kwenye kila eneo la maisha yako, jitengenezee uhuru wa kuchagua, jua kila mbadala unaopatikana kabla hujaendelea kufanya kile ambacho hutaki kufanya. Usikubali kujiweka kwenye hali ambayo inakubidi ufanye kitu hata kama hujisikii kufanya.
Kila wakati jiulize mbadala ni upi? Kisha pima ulichonacho sasa na mbadala. Hata mambo yanapokwenda vibaya, usibaki kujiumiza na kilichoenda vibaya, badala yake jiulize mbadala ni upi. Jiulize mambo yangewezaje kuwa mabaya zaidi au kama yangekuwa mazuri yangekuwaje. Kwa kuingiza njia hii mpya ya kufikiri, utajiondoa kwenye mabaya yaliyotokea na kuweza kuona kipi bora kufanya au kipi cha kuepuka zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog