Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUISHI ILI ULE…
Simba, pamoja na ukali wake wa mwituni, anaishi kwa sababu mbili tu, kula na kuzaliana.
Ndiyo maana pamoja na ukali wa simba, hutasikia historia ya simba fulani aliyefanya makubwa sana.
Tembo pamoja na ukumwa wa mwili wake, twiga na urefu wake, wote wanasukumwa kufanya vitu viwili kwenye maisha yao, kula na kuzaliana.
Lakini sisi binadamu tunao uwezo mkubwa wa kwenda zaidi ya hayo mawili. Ndiyo kula na kuzaliana ni moja ya majukumu yetu makubwa, lakini tunao uwezo wa kwenda zaidi ya hapo.
Hatuna ukali kama wa simba, hatuna ukubwa kama wa tembo na wala hatuna urefu kama wa twiga, ila tuna akili, ambayo ina nguvu na uwezo mkubwa sana kuliko sifa nyingine zote za wanyama tunaowajua.
Akili hii kama tukiitumia vizuri, tunaweza kufanya makubwa sana, tunaweza kuyafanya maisha yetu na ya wengine kuwa bora zaidi na tunaweza kuja na njia za kibunifu za kuyafanya maisha yawe bora zaidi.
Lakini hiyo ni kama tu tutaweza kutumia akili zetu vizuri, kama tutaweza kufikiria zaidi ya kula na kuzaliana.
Na hii ina maana kwamba, kama kinachokusumbua wewe kwenye maisha ni utakula nini au watoto watakula nini, familia itaishaje, bado hujaweza kujitofautisha na wanyama wengine, ambao nao wanapambana wapate kula na familia zao ziwe vizuri.
Kula kwetu na maisha bora ya familia zetu ni hitaji la msingi, lakini hatupaswi kuishia hapo. Wote waliokufa na mpaka leo tunawakumbuka hawakuishia kwenye kula kwao na familia zao. Bali walikwenda mbali zaidi, walifanya makubwa zaidi.
Usikubali kuishi maisha yako yote ukikimbizana na chakula na kuzaliana, kazana kuweka alama kwenye hii dunia, kwa kufanya mambo makubwa zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujitofautisha na wanyama wengine, kwa kutumia akili yako kwa ufanisi zaidi.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #JitofautisheNaWanyama
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha