Kila mtu alizaliwa akiwa huru kabisa, hakuna na kifungo chochote na mtu yeyote, hakuwa anadaiwa chochote na yeyote.
Na wakati wa utoto kila mtu alikuwa huru kabisa, hakuwa na vifungo vyovyote wala kudaiwa kokote.
Lakini sehemu fulani kwenye maisha ya utu uzima, mtu anajikuta ameingia kwenye vifungo ambavyo hajui hata ameingiaje. Anajikuta tayari yupo kwenye kifungo, tayari amepoteza uhuru wake na hajui anaondokaje kwenye kifungo hicho.

Lipo neno ambalo wengi wamekuwa wanapenda kulitumia, ni neno rahisi na lenye kuwaridhisha wengi, ambalo limewaingiza watu wengi sana kwenye vifungo na kupoteza uhuru wao.
Neno hili ni NDIYO. Kila unaposema ndiyo kwenye jambo au kitu chochote, maana yake kuna sehemu ya uhuru wako unaipoteza. Unaposema ndiyo kwenye kazi fulani, maana yake muda wako na nguvu zako zitaenda kwenye kazi hiyo, na hutaweza kuzitumia kwenye kazi nyingine kwa wakati huo.
Unaposema ndiyo kwa tabia fulani, maana yake unakubali tabia hizo ziongoze maisha yako. unaposema ndiyo kwa kilevi, maana yake unakubali akili zako ziendeshwe na vilevi na siyo fikra zako sahihi.
SOMA; UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…
Sasa tunafanyaje? Tuishi maisha bila ya kusema ndiyo?
Jibu ni hapana, hatuwezi kuishi maisha bila ya kusema ndiyo kabisa.
Lakini tunapaswa kuwa makini na matumizi ya neno ndiyo. Kama ambavyo unatumia moto kwa umakini, basi tumia neno ndiyo kwa umakini mkubwa sana.
Kabla hujasema ndiyo, jiulize ni uhuru gani unakwenda kupoteza kwa ndiyo hiyo na je ni thamani halisi ya uhuru wako.
Sema ndiyo kwa yale mambo ambayo ni muhimu zaidi kwako, yale mambo ambayo yanayafanya maisha yako kuwa bora kabisa.
Na kama ndani yako hujisikii kusema ndiyo, usiseme tu kuwaridhisha watu, maana hapo utakuwa umenunua utumwa mkubwa mno kwenye maisha yako. Kama kuna kitu hutaki kufanya, sema hapana, na unaposema ndiyo, sema NDIYO kubwa na itekeleze kwa viwango vya juu sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog