Tumezaliwa kama watu, binadamu ambao tunaweza kufikiri kwa kina na kubadili mazingira yetu, tofauti na wanyama ambao wanayapokea mazingira kama yalivyo.

Lakini hatujawahi kuelezwa kwa kina ipi gharama halisi ya kuwa mtu.

Gharama kubwa kabisa ya kuwa mtu ni hisia, tunapenda kufanya mengi kwa kutumia fikra zetu, lakini hisia zetu zinaingilia na zinatufanya tushindwe kufanya kila tulichopanga.

Njia Panda

Kwa hakika, hutaweza kukamilisha kila ulichopanga kufanya, hutaweza kupata kila unachotaka na kikwazo cha kwanza ni hisia zako mwenyewe.

Sisi ni viumbe wa kifikra, lakini tunasukumwa sana na hisia, na maamuzi mengi tunayofanya kwenye maisha yetu yanaongozwa na hisia na kudhibitishwa na fikra.

SOMA; UKURASA WA 957; Ongea Unavyotaka, Lakini Watu Watasikia Wanachotaka Kusikia…

Kama watu tunasukumwa na hisia na kuendeshwa na mihemko.

Kama watu tunatamani kuwafurahisha wengine, tunapenda kukubalika na wengine.

Kama watu tunakata tamaa pale tunaposhindwa na kuangushwa na wengine.

Na kama watu tunachoka pale tunapofanya kazi na kupata msongo wa mawazo pale mambo yanapokwenda tofauti na tunavyotarajia.

Gharama halisi ya ubinadamu ni hisia, ambazo pia ndiyo uimara wetu. Mashine zinaweza kufanya kazi masaa 24, lakini haziwezi kuweka hisia kwenye kile ambacho zinafanya. Na sehemu kubwa ya mahusiano ya watu ni hisia.

Tunapaswa kujua gharama hii ya ubinadamu na jinsi ya kuitumia vizuri ili isiwe mzigo kwetu. Tuelewe kwamba hisia ambazo ndiyo zinatufanya kuwa watu, ndiyo kikwazo kwa mafanikio yetu. Hivyo tuhakikishe tunakwenda vizuri na hisia zetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog